Kitaifa
Serikali kufanya marekebisho ya bodi ya mikopo
Dodoma. Serikali itafanya marekebisho ya sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), kuangalia mambo mbalimbali ikiwemo vigezo vya utoaji wa mikopo hiyo.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Agosti 29, 2023 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga wakati akijibu swali la nyongeza Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Rose Tweve.
Akiuliza swali hilo, Tweve amehoji haja ya kufanya mapitio ya sheria ya bodi ya mikopo ili kutatua changamoto nyingi ambazo watoto wa kitanzania wanapata kupata mikopo ya elimu ya juu.
Akijibu swali hilo, Kipanga amesema katika Mradi wa Elimu ya Juu ka Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), wametenga fedha kwa ajili ya kufanya mapitio ya sheria hiyo kwa kuwa wanafahamu sheria hiyo ina miaka 19 tangu itungwe.
“Sasa hivi tunafanya mapitio ili kuangalia vigezo na namna gani ya kuweza kuhuisha taarifa zetu lakini vile vile namna ya utoaji wa mikopo yetu. Naomba niwaondoe hofu wabunge hadi kufika mwisho wa mwaka huu shughuli hii itakuwa imekamilika,”amesema.
Amesema kwa kufanya hivyo kutafanya kuwa na sheria mpya itakayoendana na kasi ya sasa.
Naye Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson amesema suala la mikopo lina changamoto hasa pale mtoto wa masikini anapokosa hata ile asilimia ndogo haipati au anapata asilimia 40 lakini hawezi kupata asilimia 60 inayobakia.
“Katika mchakato wenu mnaendelea wa kufanya mapitio jambo hili mtazame wakati mnatenga hizo fedha kiasi kwa ajili ya watoto ambao mfumo unakuwa haujawatambua lakini kwa kweli wanashida,” amesema.
Spika Tulia amesema kuwa haijalishi wapi mtoto amesoma, lakini pia mwingine huaandika mzazi wake ana kazi lakini anapata mshahara wa Sh100, 000 yeye ni mfagizi ataweza kulipa ada kweli na kesi hizo ni nyingi.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum, Sophia Mwakagenda, alihoji kwa nini kumekuwa na ugumu wa upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi waliosoma shule binafsi wanapojiunga na elimu ya juu.
Akijibu swali hilo, Kipanga amesema kila mwaka Bodi huandaa mwongozo unaopaswa kuzingatiwa na waombaji na kuweka masharti ya utoaji mikopo kwa mwaka husika. Pamoja na vigezo vilivyotajwa.
“Mwongozo huelekeza taratibu za kufuata wakati wa kuomba mkopo pasipo kuangalia mwanafunzi kasoma shule ya binafsi au ya umma,” amesema.