Kitaifa
Huu ndio mwelekeo mpya wa KKKT chini ya Askofu Malasusa
Moshi. Ni mwelekeo mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), baada ya Askofu Alex Malasusa kuchaguliwa kuliongoza.
Suala la kuridhiwa KKKT kuwa na katiba moja na hotuba ya Askofu Fredrick Shoo mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, vinatoa picha ya mwelekeo huo chini ya Askofu Malasusa, anayetajwa kuwa mpenda maendeleo,
Askofu Malasusa alishawahi kuwa mkuu wa Kanisa hilo kutoka mwaka 2007 hadi 2015.
Katika hotuba aliyoitoa mbele ya Rais Samia Agosti 21, mwaka huu katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Makumira (Tuma), jijini Arusha wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya KKKT, Askofu Shoo alizungumzia mijadala inayoendelea kuhusu mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii, kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai (IGA).
Baadaye alisema: “Mheshimiwa Rais, Kanisa lipo pamoja na wewe. Tutaendelea kukuombea na kukuunga mkono katika kulisukuma gurudumu la maendeleo ya nchi kwa masilahi mapana ya nchi yetu.”
Kulingana na katiba ya Kanisa ya mwaka 2015, Askofu Malasusa, ambaye pia ni mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, aliyechaguliwa Agosti 24, mwaka huu ataingizwa kazini katika muda usiozidi miezi sita tangu kuchaguliwa kwake.
Yaliyojiri baada ya uchaguzi
Agosti 26, 2023 kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa uchaguzi huo, Askofu Shoo alizungumzia mijadala inayoendelea katika mitandao ya kijamii, akisema hana shaka na Askofu Malasusa na kwamba ni kawaida watu kuzungumza.
“Ninajua ni kawaida watu kuzungumza mengi baada ya uchaguzi kama huu. Muhimu na wito wangu kwa wanakanisa wote ni kukubali matokeo na kumwombea sana mkuu aliyechaguliwa,” Askofu Shoo aliimbia Mwananchi Digital.
“Sina shaka na Askofu Malasusa; ninaamini chini ya uongozi wake Kanisa litaendelea kukua na kuimarika kwa kiwango kingine, hasa baada ya mkutano mkuu uliomalizika kufanya uamuzi wa kihistoria wa KKKT kuwa na katiba moja.
“Tunamshukuru sana Mungu mkutano mkuu ulienda na kumalizika salama kabisa. Uchaguzi ulienda vizuri kwa kufuata katiba.
“Maaskofu wote walioko kazini isipokuwa mkuu anayemaliza muda wake walipigiwa kura na Halmashauri Kuu, kupata majina matatu ya kupeleka kwenye mkutano kupigiwa kura, ndipo Dk Malasusa akaibuka kidedea.”
Askofu Shoo alisema Kanisa na Dayosisi ya Mashariki na Pwani watapanga muda wa kumwingiza kazini ndani ya muda usiozidi miezi sita kwa mujibu wa katiba.
Rais Samia ni miongoni mwa viongozi waliompongeza Askofu Malasusa kwa kuchaguliwa kuwa Mkuu wa Kanisa hilo, akichukua nafasi ya Askofu Shoo aliyemaliza muda wake wa uongozi.
Juzi Rais Samia alitumia kurasa za mtandao wa kijamii kumpongeza Askofu Malasusa kwa kuaminiwa kuliongoza Kanisa hilo lenye waumini zaidi ya milioni nane nchini, likiwa limetiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake Tanzania.
Alisema kuchaguliwa kwake ni ishara ya imani ya Kanisa juu yake katika kulitumikia na kwamba wito wake huo si tu utumishi katika yahusuyo roho na imani, lakini katika yote yanayofanywa na KKKT kuboresha maisha ya Watanzania.
“Nanukuu kutoka Biblia Takatifu kwenye Kitabu cha Kumbukumbu la Torati 31:8 inayosema: “Naye Bwana, yeye ndiye atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike,” alisema Rais Samia.
Uchaguzi ulilazimika kurudiwa mara tatu na katika duru ya mwisho, Askofu Malasusa alipata kura 167 sawa na asilimia 69.3 ya kura 241 zilizopigwa, huku Askofu Adnego Keshomshahara akipata kura 73 sawa na asilimia 30.3.
Askofu Shoo ambaye pia ni mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, alisema idadi ya wapigakura ilipaswa kuwa 252, ila waliokuwepo ni 248, kati ya hao, 214 walipiga kura za ndiyo sawa na asilimia 86, huku kura za hapana zikiwa 36, sawa na asilimia 14.
Kuridhiwa katiba moja
Kanisa lilifanya uamuzi wa kihistoria pale wajumbe 214 kati ya 248 wa mkutano mkuu wa 21 wa KKKT waliporidhia pendekezo la kuwa na katiba moja.
Kwa mabadiliko hayo, inakwenda kuondoa katiba za dayosisi zake 27 ambazo zinazipa mamlaka kamili ya kujiendesha na sasa KKKT linakwenda kuwa na mkuu wa Kanisa mwenye mamlaka makubwa zaidi kuliko awali.
Kupitishwa kwa pendekezo hilo, mkuu wa kanisa atakuwa na uwezo wa kuwachukulia hatua maaskofu na wachungaji wanaokiuka maadili na hatafanya hivyo peke yake, bali kwa kutumia chombo cha kikatiba kitakachoundwa.
Muundo huu unaelezwa kuwa na tiba iliyotafutwa kwa muda mrefu ya namna ya kushughulikia migogoro na nidhamu katika dayosisi, kwa kuwa kwa katiba ya sasa kila moja ina mamlaka kamili kisheria na ina vyombo vyake vya uamuzi.
Akizungumzia uamuzi huo, Mwanasheria wa KKKT, Azaeli Mweteni alisema baada ya kuwasilishwa kwa mchakato wa katiba moja ya Kanisa na kuridhiwa na wajumbe hao, katiba mpya itaondoa zile za dayosisi.
“Kisheria ni kwamba, mkutano mkuu wa 21 wa KKKT umepitisha mchakato wa katiba moja ya Kanisa kwa sababu lililetwa pendekezo la kuandaa katiba moja ya Kanisa ambayo itaziondoa za dayosisi na kuwa na moja,” alisema na kuongeza:
“Katika katiba hii ni kwamba, imelenga kuliongezea nguvu Kanisa ili liendelee kuwa moja kama ambavyo imekusudiwa.
“Hii italeta mabadiliko ya kiutendaji, lakini pia kuimarisha mfumo wa kiutawala na wa kiuongozi katika Kanisa. Pia kuendelea kuimarisha Kanisa kuwa moja na kuimarisha uwajibikaji.”
Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo kutoka Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk Aneth Mnzava alisema Kanisa kuwa na katiba moja kutasaidia kutekeleza dhana ya umoja na litakuwa na nguvu zaidi kuliko sasa kila dayosisi ina yake.
Vifungu vya rasimu
Miongoni mwa vifungu vipya vilivyopo katika rasimu ya katiba moja ambayo gazeti hili limeviona ni kuanzisha cheo cha katibu mkuu kiongozi na mkuu wa Kanisa kuongoza kwa kipindi cha miaka 10 badala ya minne ya sasa.
“(Mkuu wa Kanisa) Ataongoza Kanisa kwa kipindi cha miaka 10, baada ya hapo anaweza kupigiwa kura ya imani kwa njia ya siri ya kuchaguliwa kipindi kingine mpaka atakapostaafu kwa mujibu wa miongozo ya uchaguzi,” inasema.
Kulingana na rasimu hiyo, mkuu wa Kanisa atatumika wakati wote na asiongoze dayosisi na atachaguliwa kutoka miongoni mwa maaskofu walioko kazini na atatakiwa awe na umri usiopungua miaka 45.
Ibara ya 37 ya rasimu hiyo inayohusu wajibu wa mkuu wa Kanisa, utakuwa ni pamoja na kuwa msemaji mkuu wa kanisa ndani na nje ya Kanisa, atasimamia dayosisi zote za Kanisa na atasimamia maadili ya maaskofu na kuwashauri kiroho. Kulingana na rasimu hiyo, pia ataweza kusuluhisha migogoro ndani ya Kanisa.
Kauli ya Bagonza, Munga
Maaskofu Benson Bagonza wa Karagwe na Stephen Munga ambaye ni Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, wametoa ya moyoni juu ya uchaguzi uliomrejesha Dk Malasusa.
Pamoja na Askofu Shoo kueleza kuwa mkutano ulimalizika salama, maaskofu hao wawili kupitia mitandao ya kijamii, waliandika kuonyesha mambo hayakuwa shwari.
“Wapendwa wangu, nimejizuia sana kuandika au kusema chochote. Lakini mmenisonga sana, nami nimo safarini. Kwa kuwa sijui kama nitafika niendako (Vienna) kabla hamjakata tamaa na kuzimia, naomba msome kwa furaha mambo haya matatu,” aliandika Askofu Bagonza akitumia maneno ya kifalsafa.
“Tumetazamwa na dunia nzima kwa siku nne. Mmoja aliyeona na alikuwa mgeni akaniuliza: “Hivi nyie wenzetu wachungaji na maaskofu mmeishagundua mbingu haipo mkafanya iwe siri yenu tu?” Akaongeza, “Kama mbingu ipo kwa nini mfanyiane haya mabaya hadharani? “Nilizoezwa kuamini kuwa watu wanakataliwa kwa sababu ya ubaya wao na wengine hupendwa kwa sababu ya uzuri wao. Sasa nimeamini wapo wanaoweza kukataliwa kwa uzuri na wakapendwa kwa ubaya wao. Cha msingi, ubaya hauwezi kukaa kwa amani na wema. Tumefundishwa.”
Bagonza akaendelea kuandika: “Katika Agano la Kale, kichafu kikigusana na kitakatifu, kile kitakatifu kinaharibika. Katika Agano Jipya, kichafu kikigusana na kitakatifu, kile kichafu kinatakasika. KKKT ni ya Agano Jipya au la Kale?
“Watu wakatili na waovu hujiandaa kupiga na kuangamiza wabaya wao wakati wote. Watu wema hutafuta kuushinda ubaya kwa wema.
“Hutokea wakati, wapigaji wakapiga na kufurahi kuwa wamepiga. Wakitulia hugundua kuwa kumbe wamepigwa sana. Kutosamehe ni sawa na kunywa sumu ukitegemea afe adui yako. Sumu uliyokunywa bila kukusudia inaua vibaya.”
“Humu kibandani kwetu huwa hatugombei bali tunagombezwa na kuzodolewa,” alisema Askofu Bagonza, ambaye aliingia katika tano bora ya maaskofu waliopendekezwa kugombea ukuu wa Kanisa, akipata kura 15.
Wakati Bagonza akisema hayo, Askofu Munga yeye alisema moja ya kasoro zilizojitokeza ni kufukuzwa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu kwa maaskofu wawili ambao ni Ambele Mwaipopo na Bagonza.
Askofu Munga amesema katika kikao cha Halmashauri Kuu, ambacho hupitisha majina ili yakapigiwe kura kwenye mkutano mkuu, jina la Askofu Bagonza lilipendekezwa, lakini halikupelekwa kwenye mkutano mkuu, kwa sababu Bagonza na Mwaipopo walifukuzwa kwenye kikao hicho.
“Sitaki kuingilia mipango na makusudi ya Mungu, lakini naomboleza kwako Askofu Bagonza kwa kufanyiwa dhuluma ili jina lako lisiteuliwe upigiwe kura na wajumbe wa sinodi ya kanisa. Moyo wangu unaugua. Nimehuzunika sana kwa ajili yako.”
Katika upigaji kura huo ili majina yapelekwe mkutano mkuu, Askofu Keshomshahara aliongoza kwa kura 32, Dk George Fihavango akipata kura 20, Malasusa 16, Bagonza 15 na Andrew Gulle alipata 15 sawa na Bagonza.
Askofu Munga alieleza kuwa licha ya Bagonza kutokuwepo katika orodha ya wagombea, alipigiwa kura zilizotajwa kuharibika.
“Haukuwepo katika chumba cha uteuzi lakini jina lako liliendelea kutajwa. Haukuwepo katika orodha ya wagombea lakini ulipata kura nyingi. Hii ni ishara ya imani kubwa watu waliyonayo kwako. Hata hivyo kwa ajili ya Kanisa nakusihi usamehe hata bila kuombwa msamaha. Amani ya Kristo ikae nawe,” alisema.