Kitaifa
Samia ashtukia mfumo ya wizi wa mapato halmashauri
Dar es Salaam. Kama ni siku za mwizi zimeshafikia arobaini, ndivyo unavyoweza kuelezea kilichozikuta baadhi ya halmashauri nchini, zilizobuni mfumo mpya wa makusanyo kinyume na ule wa Serikali.
Hatua hiyo, kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan ni mbinu ya wizi wa fedha hizo zinazokusanywa unaohusisha mnyororo mrefu.
Rais Samia ameyabainisha hayo mkoani Pwani leo, Jumapili Agosti 27, 2023 katika hotuba yake ya kufunga mafunzo ya uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa.
Kwa sababu Serikali inapeleka fedha nyingi katika Mikoa, Rais Samia amesema zinatafutwa njia za kuzikwepesha na hilo amelibaini alipokwenda Mbeya katika maonyesho ya Sikukuu ya Wakulima ‘Nanenane’.
“Nilikuwa Mbeya hivi karibuni kwenye Nanenane, nikakuta kadhia pale maofisa kabisa wa halmashauri wametengeneza mtandao wao, mbali na ule unaokusanya fedha za Serikali kiuhalisia kuna mwingine wa pembeni na umekusanya fedha nyingi sana.
“Baada ya wao kufanikiwa wakawapa jirani zao, wakawapa jirani zao, nilikuwa nasubiri ripoti kutoka kwa Waziri (Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-Tamisemi), lakini hajaleta bado na mimi nalijua na naendelea kufuatilia kwa njia zangu, sasa hiyo ripoti ije ikiwa diluted (imechakachuliwa),” amesema.
Ameeleza hayo yanafanyika ilhali eneo hilo kuna Mkuu wa Wilaya, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkaguzi wa Ndani na Katibu Tawala wa Wilaya.
“Unajiuliza hawa watu wote wanafanya kazi kule waliko au wanajifanyia kazi badala ya kufanyia watu, kwa sababu kama wote wapo kazini hili lingeonekana mapema, lakini kinachoonekana kuna mnyororo unaanza huko zinakatwa mapaka kila mtu anapata fungu lake,” amesema.