Kitaifa
Serikali yaipa ‘tano’ Aga Khan University, yaahidi ushirikiano sekta binafsi
Arusha. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imekipongeza Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) na kuahidi kushirikiana nacho katika kuboresha sekta ya elimu nchini na maeneo yote yenye kugusa jamii kwenye sekta mbalimbali.
Waziri huyo ameyasema hayo jana jijini Arusha alipotembelea eneo ambalo linatarajiwa kujengwa tawi la chuo hicho lililopo wilayani Arumeru, Mkoa wa Arusha.
Katika muktadha huo, Profesa Adolf Mkenda ni Waziri katika wizara hiyo, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji huku akitolea mfano taasisi ya Aga Khan ambayo inatoa huduma mbalimbali ikiwemo elimu na afya.
“Serikali ya Tanzania tunafurahia kazi na huduma mnazotoa na uwekezaji wenu ni wa hali wa juu, serikali inatamani kuona ujenzi wa chuo hiki unaanza na tunaahidi kushirikiana na nyie katika hilo na tuko tayari kufanya kile kinachotakiwa ili kila kitu kikae sawa tuone ujenzi unaanza,” alisema Profesa Mkenda na kufafanua;
“Hili ni eneo ambalo kulikuwa na ahadi ya kujenga tawi la Chuo kikuu cha Aga Khan, na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alimuomba Aga Khan ajenge tawi la chuo na alikubali, kazi yetu ni kuendelea kufuatilia, kuhimiza na kutafuta changamoto ni ipi ili tuitatue na chuo kijengwe.”
Waziri huyo ameongieza kusema: “Rais anaposema anafungua nchi ni pamoja na kuwa na vyuo vikuu ambapo watu kutoka nje ya nchi watakuja kusoma, mnajua Aga Khan hana shughuli ndogo akifanya kitu anafanya kweli,”
Awali Makamu Mkuu wa Chuo hicho hapa nchini, Dk Eunice Pallangyo, alisema chuo hicho kina programu nyingi za elimu na afya na kuwa kwa sasa Arusha tafiti nyingi zinaendelea katika masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na mazingira kwa ujumla.
“Tafiti nyingi zinazoendelea zinahusu mabadiliko ya tabia nchi, ardhi na mazingira kwa ujumla wake. Tunaamini tuna uwezo wa kufanya mambo makubwa endapo tunashirikiana na Serikali,” amesema.
“Tunaendelea na tafiti mbalimbali za kina kwani chuo kinapenda kujibu maswali yaliyopo kwenye jamii ambayo ni ya kitaifa suala la mazingira ni mojawapo,”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa utafiti, Kituo cha Elimu ya Mazingira na Utafiti wa tabia nchi Arusha, Dk Emanuel Sulle, amesema lengo lao kubwa ni kufanya utafiti unaokidhi mahitaji ya watu, hasa yale mtatizo yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa na mazingira.
“Mfano wenyeji wetu katika maeneo haya ya Arusha wametuambia wana changamoto tatu, afya, maji na magonjwa na katika kutafiti tumejua changamoto zote zinatokana na maji kutokuwepo, hii imesababisha wengine wasiweze hata kunawa uso na kupata magonjwa ya macho, ngozi,” amesema.
“Tunataka tufanye utafiti wa kina kuwashirikisha wananchi watupe elimu yao ya asili kuhusu mabadiliko ya mazingira na namna gani sisi tunatatua hizo changamoto zote kwa kujikita katika elimu ya mazingira na kutumia eneo hili kama sehemu ya utafiti wa changamoto wananchi watakuja kujifunza hapa kwetu,” amesisitiza