Connect with us

Kitaifa

Rais Samia amtumia ujumbe Mkuu mpya wa KKKT

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amempongeza Askofu Alex Malasusa kwa kuchaguliwa kuwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) akichukua nafasi ya Askofu Fredrick Shoo aliyemaliza muda wake wa uongozi kwa mujibu wa katiba ya kanisa hilo.

 Askofu Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani aliibuka mshindi wa uchaguzi uliokuwa na mchuano mkali baina yake na Askofu Abednego Keshomshahara wa Dayosisi ya Kaskazini Magharibi uliofanyika Alhamisi ya Agosti 24,2023 jijini Arusha.

Askofu Malasusa aliibuka mshindi kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa 21 wa KKKT kumchagua kwa kura 167 sawa na asilimia 69.3 ya kura 241 zilizopigwa huku Askofu Keshomshahara akipata kura 73 sawa na asilimia 30.3.

Mshindi alipatikana baada ya uchaguzi kurudiwa mara tatu kwa sababu ya kutokufikiwa kwa theluthi mbili ya kura zote zilizokuwa zimepigwa.

Jana Ijumaa, Agosti 25, 2023, Rais Samia alitumia kurasa zake za kijamii kumpongeza Askofu Malasusa kwa kuaminiwa kuliongoza kanisa hilo lenye waamini zaidi ya milioni nane nchini likiwa limetiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake Tanzania.

Ujumbe wa Rais Samia unasomeka:

Nakupongeza Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa kwa kuchaguliwa kuwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Kuchaguliwa kwako ni ishara ya imani ya Kanisa juu yako katika kulitumikia. Kwa hakika, wito wako huu si tu utumishi katika yahusuyo roho na imani, lakini pia katika yote yanayofanywa na Kanisa kuboresha maisha ya Watanzania sehemu mbalimbali.

Nanukuu kutoka Biblia Takatifu kwenye Kitabu cha Kumbukumbu la Torati 31:8 inayosema: “Naye Bwana, yeye ndiye atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike.”

Nakutakia kila la kheri.

Askofu Malasusa amewahi kushika wadhifa huo kati ya mwaka 2007 hadi 2015 na nafasi yake ikachukuliwa na Askofu Fredrick Shoo ambaye naye ameongoza kwa miaka nane na amemkabidhi tena mikoba Askofu Malasusa.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi