Kitaifa

BARUA YA WAZI KWA RAISI WA BARAZA LA MAASKOFU WA KANISA LA KATOLIKI TANZANIA DR GERVAS NYAISONGA; KUFUATIA SAKATA LA UWEKEZAJI WA BANDARI KATI YA SERIKALI YA TANZANIA NA SERIKALI YA UMOJA WA FALME ZA KIARABU

Imeandikwa na;
*BY LUGETE MUSSA LUGETE*
Na. Comred Mbwana Allyamtu-CMCA

Ndugu Mheshimiwa Baba Askofu Dr Gervas Nyaisonga amani ya Mungu iwe nawe,rehema na baraka zake zikujaze upendo,amani ,utulivu na busara.

Naitwa Lugete Mussa Lugete, mchambuzi wa siasa za Kimataifa, Mwanamajumui wa Afrika na Mwanahistoria, kwa pamoja na Comred Mbwana Allyamtu-CMCA tumeamua kuandika barua hii ya wazi kwako kufuatia waraka kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania kupinga uwekezaji wa Bandari, ambapo wewe ndio Raisi wa TEC.

Ndugu Mheshimiwa Baba Askofu Dr Gervas Nyaisonga, naanza nukuu mbalimbali kutoka kwa Mwalimu mkongwe na mwenye heshima kubwa ndani ya Kanisa la katoliki St Augustine kutoka Algeria.

“Upendo wa Mungu hauna mipaka ya dini, bali unawakumbatia watu wote bila ubaguzi.” – Mtakatifu Augustine

“Kuabudu ni kujitolea kwa Mungu, siyo kujitenga na watu wengine.” – Mtakatifu Augustine

“Uhuru wa kuabudu ni haki ya kila mtu, na hakuna dini inayopaswa kupewa upendeleo.” – Mtakatifu Augustine.

Tarehe 20/8/2023 Baraza la Maaskofu Tanzania lilitoa waraka kupinga uwekezaji wa Bandari kati ya serikali ya Tanzania na serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu yaani U.A.E. Hoja za TEC ni kwamba sauti ya wengi ni sauti ya Mungu,hivyo serikali haipaswi kupuuza sauti ya umma juu ya mapungufu ya mkataba wa Bandari.

Ndugu Mheshimiwa Baba Askofu Dr Gervas Nyaisonga, naomba unisamehe Kwa kuandika barua hii Kwa sababu miezi miwili iliyopita viongozi mbalimbali wa dini waliitwa ikulu na Mheshimiwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano Dr Samia Suluhu Hassan ili watoe maoni yao kuhusu sakata la Bandari, Miongoni mwa waliozungumza ni Baba Askofu Dr Kalikawe Bagonza, Raisi aliwaambia kwamba maoni yao yatafanyiwa kazi Kwa sababu bado kuna nafasi za kujadiliana na kuzungumza kati ya wawekezaji na serikali ya Tanzania.

Kiufupi ni kwamba serikali haijachelewa, nimesikitishwa na usaliti uliofanywa na TEC Kwa serikali Kwa sababu maoni yenu yanafanyiwa kazi na mazungumzo ya utekelezaji wa mkataba bado hayajaanza.

Ndugu Mheshimiwa Baba Askofu Dr Gervas Nyaisonga; naomba nianze kueleza sintofahamu kati ya viongozi wa kanisa la katoliki na makundi kadhaa ya wapigania Uhuru wa Tanganyika tangu mwaka 1920.

Baada ya vita ya kwanza ya dunia mwaka 1918 kundi la Wahafidhina yaani Triple Alliance lilipoteza pambano ambapo wanachama wake kama Ujerumani, Muungano wa Austria na Hungary, Italia na Dola ya Kiislamu ya Ottoman walipoteza na kuadhibiwa kikanuni na mkutano wa Versailles Paris wa mwaka 1919.

Hapa nchini Tanganyika Kleist Mbuwane Sykes mtoto wa shujaa wa Kizulu Mbuwane Sykes, alianza harakati za ukombozi wa Kifikra kutaka Watanganyika wapate kutambua haki zao, baadae akakutana na Dr James Emman Aggrey akiwa mmisheni Dar es Salaam na kumuomba ushauri kuhusu kuanzisha chama Cha Wafanyakazi,kwakuwa Dr James Emman Aggrey alikuwa analinda maslahi ya kanisa la katoliki Afrika Mashariki,akaandika waraka kwenda Vatican kuhusu hofu yake kwamba huenda miaka ijayo Tanganyika ikatumbukia Kwa waislamu,

Wakristo wa kanisa la katoliki wanapaswa kuwa macho Kwa sababu kanisa lina mali nyingi, Kuanzia hapo chama Cha TAA kikaanzishwa tayali vuguvugu za udini kati ya waislamu na Wakatoliki zilianza, mwaka 1949 Kleist Mbuwane Sykes aliaga dunia na kuwaachia chama wanae wa kiume wanne ambao ni Abdulrahd Sykes, Ali Sykes, Ayoub Sykes na Abbas Sykes, Mwaka 1952 Joseph Kasela Bantu alimpeleka Mwalimu Nyerere kariakoo kuonana na familia ya Sykes na mipango ya Nyerere kushika dola ilikuwa chini ya Dr Vedastus Kyaruz.

Uchaguzi wa mwaka 1954 ulikumbwa na sintofahamu nyingi na bila shaka mkono wa kanisa la katoliki ulihusika mpaka Mwalimu Nyerere akamshinda Abdulrahd Sykes.

Mara baada ya Uhuru wa Tanganyika ukazuka mgogoro kati ya kanisa la katoliki na waislamu hasa 1962_1970 ambapo Mwalimu Nyerere alimtumia Mheshimiwa Rashid Mfaume Kawawa kuwadhibiti familia ya Sykes.

Historia ya kanisa katoliki Tanzania imeanza toka mwaka 1880, imekuwa hadi kufikia mwaka wa 1960 Kanisa katoliki likawa taasisi kubwa inayomiliki mamilioni ya dola ya misaada inayopokelewa kutoka wahisani na wafadhili walioko katika ulimwengu wa Kikristo.

Kanisa katoliki sasa hivi linahodhi mahospitali, misururu ya ndege binafsi, viwanja vya ndege, makampuni ya uchapaji na mitambo ya kupiga chapa, stesheni za radio na magazeti.

Kanisa katoliki pia limekuwa na nguvu na udhibiti wa mambo kiasi kwamba wakati mwingine watendaji, hasa Wakristo katika serikali na ndani ya chama tawala CCM hawajui utii wao upo kwa nani, serikalini au katika Kanisa?.

Ni katika kuchanganyikiwa huku kwa watendaji wa serikali kuhusu uhusiano wao na Kanisa na serikali ndiko kulikoamsha kutoaminiana kati ya Waislam na serikali mara tu baada ya uhuru kupatikana.

Serikali ikaonekana kama moja ya taasisi za Kanisa katoliki na Waislam wakiwa ni watazamaji tu, Mara baada ya uhuru Kanisa katoliki likaangalia nafasi yake na serikali mpya iliyokuwa madarakani, Wakati wa kudai uhuru Kanisa lilijiweka mbali na siasa na ikaonekana kuwa Kanisa lilikuwa likiheshim ule mpaka kati ya dini na siasa.

Wakati ule mgongano kati ya Kanisa na serikali haukupata kusikika hata kidogo.

Baada ya uhuru kupatikana tu na serikali ikawa mikononi mwa wananchi, Kanisa katoliki likaanza kusikika likisema kuwa lina haki na wajibu kuwa na ushawishi ndani ya serikali, kuikosoa serikali na kuingooza pale inapoona serikali haifanyi mambo sawa kwa matarajio yake, Katika msimamo huu mpya, Kanisa likajipa fursa ya kuwa msemaji wa watu.

Huu ulikuwa ni mwelekeo mpya katika mambo ya siasa na utawala.

Hapa ndio kanisa katoliki likatengeza mfumo wa kanisa ndani ya serikali, mfano wa hayo ni pamoja na..

Endapo waislam watakuwa na hoja nzito kwa serikali lakini Wakatoliki wakaipinga basi hakuna litalokuwa,
Lakini wakristo wakitaka kwa serikali hata waislam wasipewe habari jambo litakuwa, Kwa mfano mahakama ya kadhi vs Mou.

Pili, kama jambo halijapata ridhaa ya maaskofu wa Katoliki haliwezi kuwa kama ambavyo haikuweza Zanzibar kujiunga na OIC na hivi sasa Tanzania haiwezi kujiunga na jumuiya hiyo kwa sababu maaskofu hawataki, mfumo katoliki hautaki.

Tatu, kanisa katoliki limejiimarisha na kujipa uhalali ambao kiasi cha kuitisha serikali na viongozi wake na wakatishika hadi kuomba radhi, na kuvitisha na hata kuvikemea vyombo vya dola na kusalimu amri.

Nne, kubanwa kwa waislam kupitia Sheria ya Ugaidi, Mkataba baina ya Serikarli na Kanisa (MoU), Mauaji ya Mwembe Chai, Maandamano ya Dibagula, mauaji ya Waislam Zanzibar, Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwaomba radhi maaskofu Sumbawanga, Samuell Malecela kumtaka aliyewaambia maaskofu wa Arusha wavue majoho ya dini na wavae ya siasa awaombe radhi.

Haya yote yamekuwa ni matokeo ya kanisa katoliki kujiona kuwa ndilo lina mamlaka pekee ya kuhodhi mambo yote ndani ya Tanzania.

Ndugu Mheshimiwa Baba Askofu Dr Gervas Nyaisonga, naomba unisamehe Kwa kuandika barua hii ya wazi Kwa sababu tangu zamani kanisa limejipa nguvu ya kuamua hatma ya wengi kuliko uhalisia, nadhani hofu ya kanisa ni juu ya mizigo yao inayopita bandarini Kwa unafuuu wa Kodi wa karibu asilimia 100, ikumbukwe kwamba kanisa la katoliki ndio taasisi yenye mashirika mengi hapa nchini kuliko taasisi yeyote ya kidini hivyo mnamizigo mingi kutoka Ulaya na Amerika.

Hilo jambo linazungumzika kuliko waraka ambao lengo lake ni kuwagawa wananchi ili wasiwe na imani na serikali,huo ni uasi dhidi ya serikali na athari zake ni mbaya na taifa linaweza kuingia kwenye migogoro isiyoisha.Hivyo tunaomba tuitunze tunu yetu ya amani Kwa sababu nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki zinaitegemea Tanzania kama sehemu yenye ustawi wa haki,usawa na amani,ndio maana nchi hizo kila zikikumbwa na machafuko Tanzania ndio kimbilio lao .

Ndugu Mheshimiwa Baba Askofu Dr Gervas Nyaisonga; naomba unisamehe Kwa kuandika barua hii Kwa sababu nataka kueleza Ajenda za Club Bilderberg dhidi ya mataifa ya Kiislamu. Ndugu Mheshimiwa Baba Askofu Dr Gervas Nyaisonga.

Kundi la Bilderberg ni shirika rasmi la watu mashuhuri na viongozi wa kisiasa, biashara, na vyombo vya habari kutoka nchi mbalimbali duniani. Kundi hili lilianzishwa mwaka 1954 na Prince Bernhard wa Uholanzi, ambaye alikuwa mwanachama wa familia ya kifalme ya Uholanzi na alikuwa na uhusiano wa karibu na wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa duniani.

Lengo la kundi hili ni kulinda maslahi ya mabeberu dunia, kuthibiti mataifa ya kijamaa Kwa kivuli na vuguvugu za demokrasia, kulinda uhusiano kati ya Marekani na mataifa ya Ulaya,kutetea taifa la Israel dunia nzima na kupambana na mataifa ya Kiislamu ambayo ni kikwazo kwenye Ajenda yao ya NEW WORLD ORDER.

Lengo lingine la Kundi la Bilderberg ni kujadili masuala muhimu ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii duniani, na kutoa mapendekezo kwa viongozi wa serikali na biashara juu ya jinsi ya kukabiliana na masuala hayo.

Mkutano wa kwanza wa Kundi la Bilderberg ulifanyika katika Hoteli ya Bilderberg huko Oosterbeek, Uholanzi, ambayo ndiyo iliyotoa jina la kundi hilo.

Mkutano wa Kundi la Bilderberg ni siri na wajumbe hualikwa kwa njia ya faragha. Kila mwaka, mkutano hufanyika katika eneo tofauti duniani, na wajumbe huwa ni pamoja na watu mashuhuri kama vile wanasiasa, wafanyabiashara wakubwa, wanahabari, na wataalamu wa masuala mbalimbali.

Kundi la Bilderberg limekuwa likikosolewa kwa kuwa siri na kutokuwa na uwazi, na wengine wanadai kuwa kundi hilo linawakilisha maslahi ya watu wenye nguvu duniani na linaweza kuathiri maamuzi ya kisiasa na kiuchumi duniani. Hata hivyo, wajumbe wa Kundi la Bilderberg wanasema kuwa mkutano huo ni wa kujadili masuala muhimu ya dunia .

Katika mkutano wa Bilderberg kiongozi wa Shirika la Ujasusi la Kanisa la katoliki duniani Black Pope ambaye ni mshauri namba Moja wa Papa , Black Pope au Generali wa kundi la Jesuit Society huingia katika mkutano wa Bilderberg ili kulinda heshima na maslahi ya kanisa duniani.

Mkutano wa Bilderberg na kundi lote haliungi mkono uislamu, mataifa ya Kiislamu na Kiarabu kujitanua kiuchumi na kisiasa nje ya mashariki ya kati, ndio maana kanisa la katoliki hapa nchini kupitia Baraza la Maaskofu limepinga uwekezaji wa Bandari kutoka kwa Umoja wa Falme za Kiarabu yaani U.A.E. Kiongozi mkuu wa Shirika la Ujasusi la Kanisa la katoliki Generali Fr Arturo Sosa aliingia kwenye mkutano wa Bilderberg wa mwaka huu.

Miongoni mwa Ajenda zilizojadiliwa ni pamoja na kuthibiti mataifa ya Kiislamu na Kiarabu yanayojitanua Afrika, Ndugu Mheshimiwa Baba Askofu Dr Gervas Nyaisonga kuna athari mbaya sana Kwa dini Moja kujipa nguvu na mamlaka ya kuishawishi serikali au umma kufuata matakwa yao huku dini zingine zikiwa kimya.Hapo waumini wa dini zingine hujiona wanyonge katika taifa lenye Uhuru wa Kuabudu.Kwa matamko na waraka mbalimbali za kanisa,hii inathibitisha kwamba mmejipa nguvu wenyewe,

Ndugu Mheshimiwa Baba Askofu Dr Gervas Nyaisonga; katika waraka wa TEC unasisitiza kuzingatiwa Kwa sauti ya wengi kwani ni sauti ya Mungu ambapo Kwa kilatini ni Vox Populi Vox dei.

Kuna matukio kadhaa yamewahi kutokea hapa nchini na kanisa au baraza la Maaskofu hawakutoa waraka au kukemea.

Naomba kuuliza maswali yafuatayo.

1. TEC inafahamu kwamba mwaka 1992 wakati Serikali inapitisha mfumo wa vyama vingi ulikuwa umekataliwa na asilimia 77 ya Watanzania? Hata hivyo serikali ikaamua uruhusiwe. Hakuna kumbukumbu za kanisa katoliki kupinga na kusema Sauti ya Wengi ni sauti ya Mungu, na Sauti ya Kanisa la katoliki lilikaa kimya Kwa sababu ajenda ya vyama vingi ulikuwa ni mpango wa mabeberu hivyo kanisa lilipuuza sauti ya umma kukataa mfumo wa vyama vingi hapa nchini.

2. TEC inafahamu kwamba mwaka 2001 baada ya matokeo ya Uchaguzi wa Zanzibar na mauaji ya wafuasi wa CUF mwezi Januari, asilimia 98 ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla walitaka kuwepo na mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na SMZ na SMT chini ya Mkapa haikutaka? Hakuna kumbukumbu za kanisa katoliki kupinga na kusema Sauti ya Wengi ni Sauti ya Mungu.

3. TEC inafahamu kwamba mwaka 2014 maaskofu wote wa Katoliki Tanzania akiwemo Kardinali Pengo na wasaidizi wake walipokea mamilioni ya shilingi pesa taslimu na nyingine kwenye akaunti zao kama Askofu Nzigilwa (milioni 80 benki) na Kilaini (milioni 40 benki). Inajua fedha hizo zilitoka katika kampuni yenye makando kando ya rushwa ya kihistoria Tanzania. Wananchi wengi walipiga kelele lakini fedha hizo hazikurudi wala hakuna kumbukumbu za kanisa katoliki kupinga na kusema Sauti ya Wengi ni Sauti ya Mungu.Kwa maana hiyo TEC iliunga mkono rushwa na kupuuza sauti ya umma.

4. Padri Kitima anasema kwa zaidi ya miaka 60 ama toka tupate uhuru bandari yetu haijawahi kuendeshwa na wageni. Hii ni kauli yake au ya maaskofu wa TEC? Ni kweli TEC haifahamu kwamba kwa zaidi ya miaka 22 Bandari yetu ya Dar imekuwa chini ya kampuni ya TICTS ikiendeshwa kwa ubia na kampuni toka Hong Kong (Hutchsons?). Kama wanafahamu, wanakumbuka wabia wazawa wa kampuni hiyo wanahusika kwenye kuwapa hela maaskofu kama Rugemalira na IPTL yake walivyofanya? Hili wamewahi kuwaambia waumini wao katika mimbari za ibada?

5. TEC wanafahamu kwamba mwaka 1998 kwenye mauaji pale Mwembechai walikufa wasio na hatia na ilikuwa rai ya mamilioni ya Watanzania kutaka kuwepo na suluhu ya kisiasa? Hakuna kumbukumbu za kanisa katoliki kupinga na kusema Sauti ya Wengi ni Sauti ya Mungu.

6. Padri Kitima anasema wananchi wamelikataa Bunge? Ametumia kipimo gani cha Kikatiba? Maana wananchi wanalikataa Bunge kwa kutowachagua Wabunge kwenye Uchaguzi. Hii “Vox Populi Vox Dei” ya TEC imetumia kigezo gani? Wananchi wakikataa Bunge pia si wameikataa Serikali? TEC inaomba vipi busara ya Mheshimiwa Rais ambaye wakati huo huo inasema serikali yake imekataliwa? Kuna kuchanganyikiwa na haraka kubwa kwenye tamko la TEC hata namna lilivyochapwa na kupangiliwa. Inanipa mashaka kwamba chombo hiki muhimu cha Kanisa kimekubali kutumika kwa maslahi binafsi bila tafakari ya kutosha.

Je hii “Sauti ya Wengi ni Sauti ya Mungu” ni wengi wapi hasa? Na mungu anayetajwa hapa ni nani? Usikute mungu anayetajwa na kusemwa asikilizwe ni mungu au miungu watu waliokuwa wanaingiza miamala kwenye akaunti za baadhi ya maaskofu wetu na viongozi wengine wa dini nenda rudi. Tujihadhari. Tusiigawa nchi kupitia madhabahu.

Ndugu Mheshimiwa Baba Askofu Dr Gervas Nyaisonga hayo ni baadhi ya maswali kadhaa nimeyabuni ili kujenga hoja kwamba TEC inalinda maslahi yake kupitia kivuli cha sauti ya umma. Kama taifa tunapaswa kufikiri Kwa kina kama Kobe na kuona mbali kama tai.

Mwaka 2009 kulikuwa na vuguvugu la Tanzania kutaka kujiunga na OIC yaani Organization of Islamic Countries, kanisa lilipinga na Raisi Wa Tanzania Dr Jakaya Kikwete alisemwa na kutukanwa ,nakumbuka kwenye Msiba wa Dr Baba Askofu Anthony Mayala Mwanza, Kadinali Pengo alitoa vijembe na kejeli Kwa serikali na hakuna kumbukumbu ya waraka wa kanisa au TEC kukemea Kwa sababu kwenye Biblia Kuna mstari wa “Heshimuni Mamraka” pia kuhusu waislamu kudai mahakama ya kadhi kwao wenyewe kanisa lilipinga na kupuuza sauti ya umma ambapo ni sauti ya Mungu Kwa mujibu wa Dr Charles Kitima.

Suala la TEC kutumia wino na maarifa yao kulinda maslahi yao bila kujali mpasuko katika taifa letu ni mbaya sana na linapaswa kuzungumzwa na kukemewa kabla ya taifa kuingia kwenye mazonge na songombingo ambazo zinaweza kuliingiza taifa vitani.

Dunia imeshuhudia migogoro mingi kutokana na dini moja kujipa nguvu, mamlaka na propaganda katika kulinda maslahi yao. Mfano nchini Rwanda viongozi wa kanisa la katoliki kama Askofu Ntihinyurwa, Augustine Misago ,Athanase Seromba na wengine zaidi ya therathini walihusika kumpa nguvu dikteka Generali Juvenile Habyalimana na kuanzisha Sheria na kanuni za kudumisha ukabila yaani AKAZU.

AKAZU ni kanuni na Sheria za kibaguzi zilizotungwa mwaka 1973 mara baada ya Meja Generali Juvenile Habyalimana kumpindua Raisi wa kwanza wa Rwanda Gregory Kayibanda.Akazu ililenga kuwapa nguvu na ushawishi Wahutu na kuwakandamiza Watutsi.Baada ya mauaji ya Kimbali Rwanda mwaka 1994 viongozi wa kanisa la katoliki baadhi walikamatwa na kufungwa jela baada ya mahakama kuwakuta na hatia.

Ndugu Mheshimiwa Baba Askofu Dr Gervas Nyaisonga, nchini Burundi Generali Michel Micombero aliwatumia viongozi wa kanisa la katoliki kujiimarisha kidola na akapata uhalali wa kuua na kudhibiti wapinzani Kwa sababu kanisa la katoliki lilimtangaza kama chaguo la Mungu na mkombozi wa wanyonge.

Nchini Nigeria, viongozi wa kanisa la katoliki katika majimbo ya Kusini hasa kabila la Igbo waliunga mkono kuanzishwa Kwa taifa la Biafra,matokeo yake wakafanikiwa kuwashawishi wanajeshi wakristo kuasi na kumuaminisha Emeka Ojukwu kwamba anaweza kuwa mkuu wa taifa la Biafra. Matokeo yake zaidi ya watu 500,000 waliuawa na taifa la Biafra likawa kama ndoto ya mwendawazimu,ashukuriwe Mungu na Generali Yakub Gowon. Hapa nchini Tanzania kuanzia mwaka 1967_1970 viongozi wa kanisa la katoliki walimshawishi Mwalimu Nyerere kuandika barua na msimamo wa serikali ya Tanzania kulitambua taifa la Biafra.

Ndugu Mheshimiwa Baba Askofu Dr Gervas Nyaisonga; Operesheni Condor ilianzishwa na Marekani miaka 1950 Kwa lengo la kupambana na mataifa ya kijamaa Amerika Kusini na visiwa vya Karibeani, Vatican ilitoa tamko la kupinga ujamaa hivyo Kwakuwa Latini Amerika Kuna Wakatoliki wengi ikabidi waraka utumwe makanisani ili wananchi wawakatae viongozi wa kijamaa Kwa kivuli cha kukuza demokrasia.Hivyo kupelekea mapinduzi ya kijeshi nchini Chile, Brazil na mataifa kadhaa ambayo yalikuwa chini ya ujamaa.

Ndugu Mheshimiwa Baba Askofu Dr Gervas Nyaisonga, serikali yetu ni sikivu na itayafanyia kazi mapungufu yaliyopo kwenye mkataba Kwa sababu hata mazungumzo na viongozi wa Bandari na wizara ya ujenzi bado,yale mliyopendeza ikulu yatafanyiwa kazi kuliko kuzua taharuki na kuligawa taifa letu.

Ndugu Mheshimiwa Baba Askofu Dr Gervas Nyaisonga naomba kuhitimisha barua hii Kwa kuchambua walau falsafa na itikadi ya Mheshimiwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr Samia Suluhu Hassan kuhusu R nne ili kujenga maridhiano na demokrasia nchini.(Reconciliation maridhiano, Resilience ustahimilivu,Reforms mageuzi na Rebuilding of the New State na ujenzi wa taifa jipya.).

Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr Samia Suluhu Hassan ana nia njema na taifa letu na ameonyesha uongozi wa kimkakati katika kutoa huduma za kisiasa, kiuchumi na kijamii Kwa Watanzania wote bila kujali dini zao,mila,kabila na tofauti zingine katika taifa letu.

Uongozi wa kimkakati ni mchakato wa kufanya maamuzi muhimu kuhusu malengo na mikakati ya shirika,taifa au taasisi kwa kuzingatia mazingira ya ndani na nje ya shirika hilo. Uongozi huu unahusisha kuchambua changamoto na fursa zinazojitokeza, kuweka malengo ya muda mrefu, kufanya mipango ya utekelezaji na kuchukua hatua za kutekeleza malengo hayo.

Ndugu Mheshimiwa Baba Askofu Dr Gervas Nyaisonga uusomapo ujumbe huu naomba uwe na uvumilivu na ustahimilivu kwani kuna mambo yatakuudhi na kukukera . Ahsante sana Ndugu Mheshimiwa Baba Askofu Dr Gervas Nyaisonga.

Tanzania inataka kulazimishwa kuwa mawazo ya kanisa katoliki ni mawazo sahihi ya kutakiwa kufuatwa na serikali na ya Watanzania wote, iwe kwa kutaka au kutokutaka.

SIGNED BY LUGETE MUSSA LUGETE.
THE GRAND MAESTER.
GURU OF PHILOSOPHY.
MASTER OF HISTORY.
Kayonka Kikenke Kamasa Mwamgongo Kigoma.
22/8/2023.
0755988284.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi