Kitaifa
KKKT kufumua katiba yake, kuchagua mkuu wa Kanisa
Arusha. Vikao vya juu vya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), vinatarajia kuanzia kesho, huku moja ya ajenda ikiwa ni kuifanyia mabadiliko katiba ya Kanisa hilo ili kuunda chombo cha juu cha kusimamia maadili ya viongozi wakiwamo maaskofu.
Kulingana na katiba ya sasa ya KKKT toleo la mwaka 2007, kila dayosisi ya kanisa hilo ina mamlaka kamili ya kujiendesha ikiwa na vikao vyake vya maamuzi vya halmashauri kuu na mkutano mkuu vyenye mamlaka kamili ya kinidhamu.
Hii imefanya mkuu wa Kanisa hilo na halmashauri yake, kufungwa mikono kuingilia na kutafuta suluhu ya mgogoro wa kiuongozi katika dayosisi zake na hili pengine ndiyo linalisukuma kuunda chombo cha juu cha maadili.
Taarifa katika baadhi ya mitandao, zilidokeza kuwa katika mabadiliko hayo kutakuwa na Askofu Mkuu wa kanisa ambaye hatakuwa mmoja wa maaskofu na kama atachaguliwa kutoka miongoni mwao, basi atalazimika kujiuzulu nafasi yake katika Dayosisi.
Hata hivyo, chanzo kingine kimesema mabadiliko hayo hayalengi kuwa na Askofu Mkuu mwenye uwezo wa kuwachukulia hatua maaskofu, bali hataweza kufanya hivyo peke yake isipokuwa kwa kutumia chombo cha kikatiba.
“Si kwamba mkuu wa Kanisa atakuwa mkuu wa maaskofu na mamlaka ya kuwachukulia hatua (maaskofu) yeye peke yake, bali kwa kutumia chombo cha kikatiba kitakachoangalia maadili na mwenendo wa viongozi,” kilidokeza chanzo chetu kimoja.
Chanzo hicho kilidokeza viongozi hao ni pamoja na wachungaji na maaskofu na kuwa maamuzi ya pendekezo la kuwa na katiba moja, yatafanywa pia na mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika Agosti 23 na 24 katika Chuo Kikuu cha Makumira.
Mkutano huo mkuu utatanguliwa na maadhimisho ya miaka 60 ya Kanisa hilo yatakayofanyika Agosti 21, mwaka huu katika chuo hicho kinachomilikiwa na kanisa hilo, mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Mbali na mabadiliko ya katiba na ajenda nyingine, mkutano huo mkuu utamchagua Mkuu wa Kanisa, nafasi inayoshikiliwa kwa sasa na Askofu Fredrick Shoo (pichani), ambaye pia ni mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa hilo.
Katibu Mkuu KKKT afunguka
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Katibu Mkuu wa KKKT, Mhandisi Robert Kitundu alisema kabla ya mkutano mkuu na halmashauri kuu, kutatanguliwa na maadhimisho ya miaka 60 ya kuanzishwa kwa kanisa hilo.
Kuhusu mabadiliko ya katiba, alisema hayo ni masuala ya ndani ya kanisa na kwa sasa hawezi kulizungumzia kwa sababu linatakiwa kutolewa na mkutano mkuu.
“Hayo ni mambo ya ndani ya kanisa. Mambo ya ndani siwezi kuzungumzia kwa sasa kwa sababu linatakiwa litolewe na mkutano mkuu kama makubaliano. Lipo ni ajenda na hiyo ajenda itaingia kwenye mkutano mkuu,” alisema na kuongeza:
“Hivyo ni vikao vya ndani vya kanisa ambavyo vinapaswa kuheshimiwa kwa namna hiyo, wao watakubaliana liingie au lisiingie. Kuna vikao vya ndani ambavyo vinapitisha hili kwa hiyo siwezi kulisema kwa uwazi,” alisisitiza.
Kitundu alifafanua kuwa baada ya maadhimisho ya miaka 60, halmashauri kuu ya kanisa itakutana Agosti 22 ambacho ni kikao kimojawapo kinachoandaa mkutano mkuu utakaofanyika Agosti 23 na 24.
Mkutano mkuu utaambatana na uchaguzi wa mkuu wa Kanisa hilo. Katibu mkuu huyo alisema Agosti 21 watafanya ibada maalumu kuadhimisha miaka 60. Pia Rais Samia atazindua maaabara za chuo hicho na kuangalia kazi zilizofanywa na kanisa.
“Tutakuwa na ibada maalumu, tutaangalia kazi zilizofanywa na kanisa ikiwemo kuhudumia watu kupitia hospitali, shule na vyuo vyetu,” alisema.
Aidha, Kitundu alisema, makanisa saba yaliyoungana na kuanzisha KKKT yatatambuliwa siku hiyo na wazee wawili ambao Juni 19, 1963 walishuhudia utiaji saini wa kuanzishwa kwa kanisa hilo.