Kitaifa
Idadi wanaosaka matibabu nguvu za kiume BMH yapaa
Dodoma. Wagonjwa wa kisukari, presha na tezi dume wamejitokeza katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kuhitaji huduma ya kuwekewa kipandikizi kwenye uume kukabiliana na tatizo la nguvu za kiume.
Takwimu zilizopatikana katika hospitali hiyo zinaonyesha kuwa kati ya wagonjwa 10 wanaofika kwenye kliniki za wagonjwa hayo, sita au saba wanaeleza kukabiliwa na tatizo la nguvu za kiume.
Kliniki za maradhi ya kisukari, presha na tezi dume katika hospitali hiyo hufanyika mara mbili kwa wiki, Jumanne na Alhamisi.
Kuongezeka idadi ya watu wanaohitaji huduma hiyo kunatokana na hospitali hiyo kutangaza kutoa huduma hiyo Juni mwaka huu, baada ya wanaume wawili kupatiwa huduma.
Akizungumza na Mwananchi, Remidius Rugakingira, daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo, figo na wanaume hospitalini hapo alisema kabla ya kutangazwa huduma hiyo walikuwa wakijitokeza wanaume watatu au wanne kati ya wagonjwa 10.
Alisema awali changamoto ya kukosa nguvu za kiume ilikuwa jambo la siri, lakini tangu kutangazwa kuwapo kwa huduma hiyo, wanaume wamekuwa wakizungumza kukabiliwa na tatizo hilo wanapokwenda kliniki.
“Kwa siku za karibuni kumekuwa na mwamko mkubwa wa wanaume kuelezea wanakabiliwa na upungufu wa nguvu za kiume, tofauti na ilivyokuwa huko nyuma. Walikuwa wanaona aibu kusema,” alisema.
Dk Rugakingira alisema wengi waliojitokeza bado wanaendelea na tiba kwenye kliniki zao ambao baada ya kupona au hali kurejea kawaida ndipo wataweza kupandikizwa uume.
Akizungumza na vyombo vya habari hivi karibuni, Mkurugenzi wa BMH, Dk Alphonce Chandika alisema gharama za upandikizaji ni kati ya Sh6 milioni hadi Sh10 milioni, tofauti na nje ya nchi ambako inapatikana hadi kwa Sh50 milioni.
Nguvu za kiume kupotea
Dk Rugakingira alitaja sababu nyingine zinazosababisha wanaume kukosa nguvu hizo ni matumizi holela ya dawa za kuongeza nguvu za kiume, msongo wa mawazo na kukosa usingizi.
“Utakuta mtu anakwenda dukani kununua kidonge kimoja cha kuongeza nguvu za kiume na wenyewe wanaita ‘kushtua’ baada ya hapo haendelei kunywa dawa hiyo, matokeo yake anashindwa kufanya tendo la ndoa,” alisema.
Alisema dawa hizo zinashauriwa kutumiwa kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu na mtu hulazimika kunywa dozi aliyoandikiwa.
Dk Rugakingira alisema upungufu wa nguvu za kiume unachangiwa na ulaji wa watu, hivyo wanapaswa kuangalia vyakula wanavyokula.
Alisema mtu anatakiwa kula vyakula vyenye virutubisho vyote vya protini, wanga, mafuta na sukari, badala ya kula visivyo na uwiano huo.
Kwa wagonjwa, aliwataka kuzingatia ubora wa chakula wanachokula badala ya ladha ili kuepuka madhara zaidi.
Pia, alishauri watu kufanya mazoezi hata ya kukimbia kwa dakika 30 mara tatu kwa wiki, kupunguza msongo wa mawazo, kulala vizuri, kupima presha na kisukari ili kuanza matibabu mapema.
Dk Rugakingira aliwataka watu kuiga maisha ya jamii ya Wamasai ambao hutembea kwa miguu mwendo mrefu, hivyo wengi hawapati maradhi kama presha na kisukari.
Kwa upande wake, Dk George Mkira, daktari wa magonjwa ya kisukari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma alisema wagonjwa wa kisukari na presha hupata upungufu wa nguvu za kiume kutokana na maradhi hayo kuathiri mishipa ya fahamu na usafirishaji damu kwenye viungo muhimu, hivyo kusababisha kushindwa kufanya kazi vizuri.
Alisema maradhi hayo huathiri kuta za mishipa ya damu na kusababisha inayokwenda sehemu za siri kutanuka na kushindwa kufanya kazi vizuri.
“Kuna namna kuta za mishipa ya damu zinaathirika kutokana na magonjwa hayo kwa kupunguza presha ya damu kwenye sehemu hizo ambazo zina hisia na mwisho wa siku wanashindwa kufanya tendo la ndoa,” alisema Dk Mkira.
Miaka mitatu bila tendo la ndoa
Dk Rugakingira alisema watu wawili waliofanyiwa upasuaji wa kupandikiza vichocheo vya nguvu za kiume Juni mwaka huu, walikuwa hawawezi kusimamisha uume kwa muda wa miaka mitatu.
Alisema baada ya kuwafuatilia wamebaini wanaendelea vizuri na wanashiriki tendo la ndoa bila shida na wanaweza kupata watoto.
Mmoja kati ya wanaume hao, alisema alipata ajali iliyomsabisha kupoteza uwezo wa kufanya tendo la ndoa kwa miaka mitatu; mwingine akichelewa matibabu baada ya kupata maambukizi kwenye njia ya mkojo.
Mmoja afunguka
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, mmoja wa wagonjwa wenye mawe kwenye figo aliyepoteza nguvu za kiume, alisema alipata changamoto hiyo mwaka 2018.
Alisema alifanyiwa upasuaji mwanzoni mwa mwaka huu, lakini akabainika kukabiliwa na ugonjwa wa tezi dume uliosababisha ashindwe kabisa kufanya tendo la ndoa.
“Siku daktari akinihakikishia kuwa nimeshapona tatizo la tezi dume ndiyo nitaanza kushughulikia la ukosefu wa nguvu za kiume ili nirudi kwenye hali yangu ya kawaida,” alisema.
Alisema yeye na mkewe hawana tatizo katika uhusiano kwa sababu anaelewa alipitia misukosuko ya kiafya iliyosababisha kupungua kwa nguvu za kiume.
Doreen Fumbi, mkazi wa Makulu jijini Dodoma, alisema wanaume wenye tatizo la nguvu za kiume hawana furaha kwenye ndoa kwa kuwa hawajiamini.
“Inafika hatua hata akikuona umesimama na mwanaume mwingine mnaongea anafikiri unamweleza matatizo yake ya nguvu za kiume. Kikubwa nawashauri waende hospitalini ili watibiwe na si kujihisi kila wakati wanyonge kana kwamba tatizo halina tiba,” alisema.