Kitaifa
Utafiti waonesha wanawake ‘wanakumbatia’ ukatili wa kijinsia
Shinyanga. Mila na desturi kandamizi katika jamii zimetajwa kuwa chanzo cha kuendelea vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto huku, baadhi ya wanawake wakidaiwa kuwa walinzi wa mila hizo kutokana na kuona umuhimu wa watoto wa kiume kuliko wa kike.
Akizungumza Agost 16, 2023 wakati wa kuwasilisha matokeo ya utafiti uliofanyika kwa miaka miwili katika Kata 18 za Halmashauri ya Shinyanga, Mtafiti kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru mkoani Arusha, Mathias Mkude amesema wamebaini wanawake ni waendelezaji wa mifumo kandamizi inayochangia ukatili huo.
Amesema pamoja na kuwa na mfumo rasmi wa kutoa taarifa za matukio ya ukatili lakini jamii bado inaamini katika mifumo isiyo rasmi kutoa taarifa ambapo kupitia utafiti huo watu 54 wametajwa na jamii kwenye maeneo utafiti ulipofanyika ambao ndiyo hupewa taarifa kati yao 50 ni wanajamii na wanne viongozi.
“Tumegundua pia pamoja na uwepo wa matukio ya ukatili wanawake ndiyo waendelezaji wa mifumo inayopelekea ukatili kutokana na kuendeleza ngazi ya familia hata mama mwenyewe anaona umuhimu wa mtoto wa kiume kuliko wa kike,”amesema Mkude
Amesema kupitia utafiti huo wamewafikia watu 1, 264 kwenye Kata 18 za Halmashauri hiyo na kuzungumza na wawakilishi wa Serikali 128 ikiwa ni pamoja na kufanya mkutano wa zaidi ya watu 900 kutoka makundi mbalimbali ya kijamii.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Shinyanga, Ngasa Mboje amesema utafiti huo utasaidia kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Amesema uwepo wa mashirika yanayotoa elimu kwa jamii ikiwemo Taasisi ya Citizens 4 change na Mfuko wa Ruzuku kwa wanawake Tanzania (WFT-Trust) ambao wamefanya utafiti huo utachangia kuleta mabadiliko kwa jamii.
Ofisa Programu Mwandamizi kutoka WFT –Trust, Neema Msangi amesema utafiti huo umefanyika eneo ambalo walikuwa wakitekeleza miradi ya ukatili kwa kuhusisha taasisi mbalimbali ambazo zimechangia kuleta mabadiliko.
Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Shinyanga, Rehema Edson ametumia fursa hiyo kuyataka mashirika kutumia utafiti huo kama chachu ya kupambana zaidi na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kuangalia wanawake na watoto ambao ndiyo waathirika zaidi.