Connect with us

Kitaifa

Mabalozi kikaangoni

Dar es Salaam. Mabalozi wanaowakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali wamewekwa kikaangoni kwa kushindwa kutekeleza vema majukumu yao, huku msomi wa diplomasia akibainisha mambo mitatu yanayochangia wawe hivyo.

Rais Samia Suluhu Hassan ndiye alibainisha jinsi Serikali inavyobeba mzigo wa kuwatunza mabalozi ambao hawaleti tija yoyote huku wengine wakiwa “hawajui wanachokifanya.”

Amesema mabalozi hao wana dhima kubwa ya kuiwakilisha Tanzania katika mataifa waliyopangiwa, hivyo waende kufanya kazi kwa kuzingatia matokeo, badala ya kusubiri matukio ili waonekane wapo.

Wakati Rais Samia akisema hayo, msomi wa diplomasia ya uchumi katika Chuo cha Diplomasia, Profesa Wetengere Kitojo akihojiwa na Mwananchi kuhusu sababu za hali hiyo, alisema mabalozi wamekuwa hawafanyi vizuri kwenye balozi zao kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kutohusishwa kwenye mikakati ya Serikali.

Profesa Kitojo alihoji pia ni kwa kiasi gani Serikali inatoa rasilimali kwa ajili ya kuwasaidia mabalozi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Baadhi ya rasilimali hizo ni rasilimali watu na fedha.

“Mimi niko ubalozini, naambiwa nitekeleze diplomasia ya uchumi, nina rasilimali za kutosha? (Hizi ni) pamoja na rasilimali za kuitisha mikutano, rasilimali za watu wangu kutembelea kampuni kubwa kuwaeleza fursa zilizopo Tanzania, nina uwezo wa kuandaa maonyesho,” alihoji.

Alisema mabalozi wanaoteuliwa wengi hawana ujuzi wa diplomasia ya uchumi na pia balozi nyingi hazina wataalamu wanaoweza kumsaidia katika kuweka mipango na kuitekeleza kikamilifu.

Profesa Kitojo alisema ni vigumu kupima ufanisi wa balozi kwa sababu unaweza usione matokeo ndani ya muda mfupi, lakini balozi akawa amepanda mbegu ambayo matunda yake yatapatikana baadaye.

“Mara nyingi nafasi za ubalozi zimekuwa za kisiasa, uteuzi unatolewa kama kulipa fadhila, huwezi kupata matokeo. Kwanza angalia tu wanaoteuliwa ni watu wa namna gani, hapo utapata picha kubwa,” alisema.

Alisema mafunzo kwa mabalozi ni muhimu kwa sababu yatainua uelewa wao na kuwafanya waone fursa na kuitangaza Tanzania duniani na hatimaye nchi itanufaika.

Akitolea mfano, Profesa Kitojo alisema nchi zilizoendelea zinakuwa na ajenda zake wanazopewa mabalozi wake wakazitekeleze.

Alichosema Rais Samia

Rais Samia alibainisha hayo jana, katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma kwenye hafla ya kuwaapisha mabalozi wapya aliowateua Agosti 11, mwaka huu na kuwapangia vituo katika mataifa mbalimbali.

Walioapishwa ni pamoja na Balozi Gelasius Byakanwa (Burundi), Balozi Habib Awesi Mohamed (Qatar), Balozi Imani Njalikai (Algeria), Ramson Mwaisaka (Rwanda), Hassan Mwamweta (Ujerumani) na Mohamed Juma Abdallah (Saudi Arabia).

Baada ya kuwaapisha, huku akitoa mifano, Rais Samia alisema mabalozi wengi hawajui wanachokifanya kwenye nchi walizopelekwa, hivyo wanashindwa kufanya mambo yenye tija kwa Taifa kupitia uhusiano wa kidiplomasia uliopo.

“Nilishakutana na Rais mwenzangu ndani ya nchi za Kiafrika, ndani ya Sadc (Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika), akaniambia ‘nibadilishie balozi, uliyeniletea hata kazini haendi, mikutano hashiriki, yupoyupo tu, hatuelewi. Tanzania hatujawazoea hivyo, sasa labda ubadilishe’, nikamwambia nimekusikia,” alisema Rais Samia bila kusema kama amefanyia kazi suala hilo.

Ingawa Rais Samia hakubainisha ni nani na nchi gani alikokuwa balozi hiyo, mataifa ambayo yanaunda Sadc ni Angola, Botswana, Comoro, DR Congo, Uswatini, Lesotho, Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Seychelles, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe na Tanzania.

Katika hatua nyingine, Rais Samia alisema tume aliyounda kwa ajili ya kuipitia Wizara ya Mambo ya Nje imempelekea mapendekezo ya kuboresha utendaji wake na mabalozi, ikiwa ni pamoja na kuzifunga zile ambazo hazina tija au kuziongezea nguvu zile zenye tija.

“Ile Tume niliyoiunda niliitaka ituambie balozi ambazo zina maana mpaka leo na balozi ambazo kwa ushirikiano wetu, hatuna haja ya kupoteza pesa kupeleka watu, au (balozi) za kupandisha hadhi au za kushusha hadhi yake.

“Nimepokea draft ya kwanza, nimewarudishia, hiki na hiki hakimo, wanaendelea kufanyia kazi na nadhani hiyo ripoti itakapokuja tunaweza kuirekebisha wizara yetu mambo yaweze kwenda mbele,” alisema.

Kiongozi huyo aliwataka mabalozi wakafanye kazi kwa kuzingatia matokeo badala ya kusubiri matukio.

“Nenda katengeneze mpango kazi, nenda kafanye kazi na tuone matokeo ya kazi unayofanya kule, vinginevyo, hatuna rasilimali za kumpa mtu akakae tu huko na familia yake, ana-enjoy (anakula raha) tu huko, hatujui anafanya nini, hakuna mrejesho, wapo tu huko nje. Tunataka tuone mrejesho unakuja,” alisisitiza Rais Samia.

Akitoa mfano mwingine, Rais Samia alisema Novemba mwaka jana alikutana na mabalozi huko Zanzibar na kujadiliana masuala mengi, lakini hadi sasa hajapata ripoti ya utekelezaji.

Alisema Tanzania inaingia mikataba na mataifa mengi, lakini mabalozi hawaijui na inaishia kwenye makabati.

“Kuna MoU tunasaini na mataifa mbalimbali, nyingi tu, ukipitia orodha ya MoU na mikataba tuliyosaini na nchi nyingi tu, lakini nyingi baada ya kusainiwa iko kwenye makabati, hatujui utekelezaji unaendaje, ziko tu.

“Lakini atakapokuja mtu kutoka hiyo nchi, mwaka fulani tulisaini MoU ilifika hapa, bado hatujafanya hapa…miaka imepita MoU haijafanyiwa kazi. Kwa hiyo mnapokwenda huko angalieni tumesaini nao vitu gani, vimefikia hatua gani ili mkienda muwe na kitu cha kusema,” alisema.

Hawajafanya chochote

Rais Salia aliongeza kuwa kuna mabalozi ambao wanaiwakilisha Tanzania katika nchi zaidi ya moja lakini hawajafanya chochote kwenye nchi wanazokaa, lakini wanatumia muda mwingine kupeleka taarifa zao za utambulisho kwenye maeneo mengine ya uwakilishi.

“Tunataka tuone matokeo, siyo tu kutambulika kwamba uko hapa, matokeo ya kule uliko ni kitu gani,” alihoji.

Aliwataka mabalozi hao kujua fursa zinazopatikana Tanzania ili wanapokwenda huko wawe na uwezo wa kuzitangaza na kuhamasisha wawekezaji kuja Tanzania.

“Mahitaji yetu na siasa za kikanda ulimwenguni ndiyo zinazoamua diplomasia yetu, bila kuzingatia haya ni sawa na kuwa na chama cha siasa kisichokuwa na dira wala ajenda zake, bali kinaendeshwa na matukio, kuna tukio limetokea linadakwa hilohilo, ndiyo siasa yao.

“Sisi kama mabalozi hatuendi hivyo, tunakwenda tukiwa tunajua mwelekeo wetu kama Tanzania ni kitu gani,” alisema Rais Samia na kuitaka Wizara ya Mambo ya Nje iweke utaratibu maalumu wa kuwajengea uwezo.

Mkuu huyo wa nchi alisema miaka ya hivi karibuni, kumetokea mahitaji mapya ya dunia, yakiwemo mabadiliko ya tabianchi, mapinduzi ya nne ya viwanda, matumizi ya akili bandia, uchumi wa buluu, umuhimu wa madini ya kimkakati, utalii endelevu, mahitaji ya diaspora na masuala ya haki za binadamu.

“Mahitaji yote haya yanaibua fursa na changamoto kwa nchi yoyote ile, kwa hiyo mwende mkiwa mnayajua hayo. Kwa hiyo ni vema wizara ikaainisha majukumu, wajibu na stahili za kila balozi ili kulinda masilahi yetu kwenye maeneo hayo,” alisema.

Mapema, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipohutubia kwenye hafla hiyo, alisema watakutana na mabalozi kwa ajili ya kuwapa maelekezo na msisitizo wa majukumu ya kwenda kufanya katika maeneo waliyopangiwa.

“Watanzania tuna matumaini makubwa kwenu kwamba mtakwenda kuimarisha uhusiano na mataifa ambayo Mheshimiwa Rais anawapeleka…diplomasia yetu ya kisiasa, kiuchumi, tunahitaji iimarike,” alisema.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax alimshukuru Rais Samia kwa kuiongezea nguvu kazi wizara hiyo na kwamba wanatarajia mabalozi hao wataleta tija kwa Taifa.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi