Makala

Ufahamu uhaini, moja ya tishio kubwa zaidi la amani kwa nchi yoyote duniani

Agosti 10 mwaka huu Wakili Boniface Anyisile Mwabukusi alisimama nje ya Mahakama Jijini Mbeya na kusema kwamba anapinga uamuzi wa mahakama kutupilia mbali kesi aliyofungua dhidi ya serikali kuhoji na kutaka kuvunja makubaliano ya Tanzania na Dubai kuendeleza Bandari.

Pembeni yake alikuwepo kada wa CHADEMA, Mpaluka Saidi Mdude Nyagali. Mwabukusi alivua joho lake lake la uwakili na kusema kuwa ataongoza umma kuingia barabarani kuandamana bila ukomo. Akaongeza anaipa serikali siku 14 kuvunja makubaliano yake na Dubai.

Usiku wa siku hiyo hiyo Dkt Wilibrod Slaa akatanfaza kupitia mitandao kwamba maneno ya Mwabukusi na Mdude kutaka kuitoa serikali madarakani kwa nguvu kama haitavunja mkataba huo ni sawa.

Haikuchukua masaa 48 wote wakawa wametiwa nguvuni na Polisi wa Tanzania na kuhojiwa kwa tuhuma za uhaini.

Je uhaini ni nini?

Uhaini ni kitendo cha watu au kikundi cha watu kutaka kuitoa serikali iliyo madarakani kikatiba bila kufuata sanduku la kura (njia za kikatiba). Nchi zote duniani zimeweka kosa la uhaini kama kosa namba moja la tishio la usalama wa nchi na adhabu yake iwapo itadhitika ni kifo. Adhabu hii iko karibu kila nchi duniani kwa kosa la uhaini. Nchi nyingine huenda mbali na huchukulia hatua kali hata wale walioshiriki kwa namna ndogo tu mfano vyombo vya habari vinavyorusha matangazo yenye maudhui ya kutetea wenye tuhuma za uhaini, na kadhalika.

Uhaini au vitendo vya uhaini vina athari gani?

Historia ya nchi nyingi linapokuja suala la uhaini na kufanikiwa ni kama kula nyama ya mtu, unatamani kuendelea. Mfano pale DRC zamani Zaire, Mobutu wa Zabanga aliondoa utawala halali wa Lumumba kihaini akishirikiana na majasusi wa Marekani na Ubelgiji ili kuchota rasilimali za Zaire. Mara nyingi mafanikio ya uhaini hufarakanisha nchi. Mfano nchi zote tunazoziona leo zenye machafuko Afrika zimewahi kupitia uhaini.

Uhaini unaweza kufadhiliwa na mataifa ya nje?

Katika vita ya kiuchumi kwenye dunia ya leo, hili linafanyika mara nyingi. Mfano Pale Misri wakati mataifa ya Kiarabu yakimuondoa Rais Muhammad Morsi yalianza kwanza kwa kutoa fedha za vikundi vya kisiasa, vyombo vya habari na maafisa wa jeshi. Vikundi hivi kwa kuwa vilishirikiana na vyombo ndani ya serikali vilipata nafasi ya kukua, vikamtukana Morsi kwa zaidi ya miaka miwili, vikaita chama chake cha Muslim Brotherhood kuwa cha kigaidi, vikamuita Morsi haipendi Misri na mwisho vikaondoa uhalali wa yeye kuwa Rais. Uhaini wa kimamboleo huu.

Tanzania kumewahi kuwa na wahaini?

Yes. Januari 1964 kuna walioasi Jeshi wakitaka kumpindua Nyerere. Wakadhibitiwa. Oscar Kambona aliwahi kushtakiwa kwa uhaini kutaka kumpindua Mwalimu Nyerere. Akakimbilia Uingereza kupitia Nairobi. Wenzake kama kina Bibi Titi, wakafungwa maisha gerezani Kisiwani Mafia. Mwaka 1982 wengine wakateka ndege kutaka Mwalimu ajiuzulu, nao wakaishia kwenye dhahma kubwa. Matishio ya uhaini yaliisha enzi za Mwalimu kutokana na sheria kali na mfano wa waliojaribu walivyoshughulikiwa na sheria. Moja ya hatari kubwa kabisa ya mfumo wa Kikatiba, amani na umoja wa nchi ni kuacha mbegu yoyote ya kiashiria cha kuondoa serikali madarakani kihaini.

Nchi nyingi wenye tuhuma za uhaini hupotezwa bila hata kufuata utaratibu wa sheria jambo ambalo linapigiwa sana kelele. Wenye kutaka kufanya hivi wanajua ndio maana utawala wa JPM hakukuwa na watu wa aina hiyo kutoka na kuogopa hatma yao. Baada ya miaka mingi ya Tanzania kuwa katika utulivu usio na viashiria vya uhaini, mwaka huu vimeibuka hayumkini baada ya Rais Samia kuruhusu uhuru mkubwa kufanya siasa, na sasa Dkt Slaa na wenzake wako chini ya Polisi. Nini kitaendelea? Muda utasema.

*George Rugambwa*
*Safarini Mbeya*

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi