Connect with us

Kitaifa

Urasimu katika utoaji vibali unavyochochea ujenzi holela

Dar es Salaam. Huenda changamoto ya makazi holela zikaendelea kuongezeka nchini endapo Serikali haitaondoa urasimu wa upatikanaji wa vibali vya ujenzi kwenye halmashauri.

Licha ya mwongozo wa utoaji wa vibali vya ujenzi uliotolewa na Tamisemi mwaka 2018 uliopunguza muda wa maombi ya vibali kutoka wastani wa siku 30 hadi siku saba, baadhi ya waombaji wamedai bado wanatumia zaidi ya siku 30.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini pamoja na ucheleweshwaji, waombaji wengi wamekuwa wakikatishwa tamaa na gharama za vibali vinavyoanzia Sh30,000 hadi Sh1milioni kulingana na aina ya jengo.

Changamoto nyingine ni masharti ya utoaji wa vibali hivyo, ikiwamo mahitaji ya ramani na idadi kubwa ya waombaji kukosa hatimiliki za viwanja vyao,

Kampuni za upimaji wa ardhi nazo zinatajwa kuchochea makazi holela kutokana na biashara ya uuzaji wa vipande vidogo vya ardhi, bila kuzingatia miongozo ya Serikali na hivyo wanunuzi kujenga bila utaratibu maalumu.

Majengo mengi katika maeneo yasiyopangwa hayana vibali na hivyo kuwa uwezekano wa kukosa huduma mbalimbali.

“Kujenga maeneo yasiyotambuliwa kisheria ni tishio la majanga, mfano unajenga kwenye eneo la kupita barabara na baadaye unalazimika kubomoa bila fidia au bondeni ambapo ni hatarishi kijiografia na hujui,” anasema Juma Mwingamno, mwenyekiti wa wenyeviti wa Serikali za mtaa mkoa wa Dar es Salaam.

Mmoja wa watu waliojenga bila vibali ni pamoja na Jamali Athuman, mkazi wa Chanika aliyedai kukatishwa tamaa na mazingira ya urasimu unaoendelea ndani ya halmashauri hizo.

“Mimi nimejenga nyumba ya vyumba vitatu bila kuchukua kibali baada ya kuona napoteza muda na fedha, mara ramani, mara nenda urudi siku fulani, nikaona niendelee na ujenzi tu,” alisema Athuman.

Changamoto za ufahamu

Licha ya umuhimu wa vibali kwa ajili ya kuepuka majanga yanayotokana na makosa ya ujenzi, bado elimu ni ndogo kwa wananchi na wengi wamekuwa wanapuuza.

Husna Anania, mkazi wa Mbagala Mzambarauni, alisema hakumbuki kama waliomba kibali cha ujenzi wakati wa kujenga nyumba yao na hajui kama kuna taratibu za kufuata kabla ya kujenga.

“Taratibu ninazoikumbuka niliponunua kiwanja nilikwenda ofisi za serikali ya mtaa kuandikishiana karatasi za mauziano, hayo mengine siyajui na wewe ndiyo unaniambia kuhusu hayo,”alisema Husna.

Kwa upande wake, Hamis Zamoyoni, mkazi wa Madale, alisema wakati anajenga nyumba yake alitumia miezi minne kufuatilia kibali na kuwa kila alipokuwa anaulizia, aliambiwa bado hadi alipoamua kumtafuta mtu ambaye alimsaidia kukipata kwa haraka.

Taratibu za utoaji wa vibali vya ujenzi kutofahamika kwa wadau wengi wa ujenzi, wakiwemo wananchi wa kawaida na kutofautiana kwa gharama za vibali vya ujenzi baina ya halmashauri moja na nyingine, pia ni tatizo.

Kutoshirikisha wananchi

Mkurugenzi mtendaji wa asasi ya Haki Ardhi, Cathbert Tomitho anasema usumbufu utoaji wa vibali na ujenzi holela unachangiwa na utekelezaji wa mpango wa urasimishaji wa ardhi bila kushirikisha wananchi.

Mpango huo unaotekelezwa na halmashauri kwa kuzitumia kampuni binafsi za upimaji, Tomitho anasema unasababisha migogoro mingi badala ya kuleta mpangilio mzuri wa ardhi.

Ingawa Sheria za Ardhi Namba 4 na 5 ya mwaka 1999 zinahusu ushirikishwaji katika kupanga mipango miji, Tomitho anasema urasimishaji unaendelea katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine, kampuni za upimaji hazishirikishi wanaohitaji huduma.

“Asilimia kubwa ya wamiliki wa viwanja wanauziana kwa maandishi na baadaye wanafuatilia hati huku wengine wakifanya hivyo baada ya kumaliza ujenzi kutokana na sheria kuruhusu,” anasema.

Alisema halmashauri nyingi zinasubiri watu wajenge kisha wanajitokeza na kuwaandikia kuwakataza kuendelea na ujenzi, kitendo kinachokaribisha mianya ya rushwa.

Mwaka jana, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula alipiga marufuku upimaji wa viwanja vya mita 20 kwa 20 lakini baadhi ya watu wameendelea na biashara hiyo kutokana na wingi wa kampuni za upimaji wa viwanja.

Tomitho anasema upo uwezekano wa watendaji kutoka katika ofisi za halmashauri kwenda mitaani wanapoishi wajengaji ili kuepusha usumbufu na kila kitu kinachosababisha urasimu ili kurahisisha mifumo iliyowekwa kisheria kufuatwa.

“Wanaweza kuweka fomu na utaratibu wa kujisajili kwa njia ya kidijitali na awepo mtu kutoka ardhi ambaye anaweza kuwaunganisha kwa urahisi na hal;mashauri na kila muhitaji akatatuliwa shida zake haraka,”anasema Timotho.

Anashauri wanaopewa mamlaka kuacha tabia ya kuwadharau watu wa Serikali za mtaa kwa kuwaona hawana elimu na kuamua kufanya mambo ya upimaji kiholela na kusahau hilo ni kosa kubwa katika usimamizi wa ardhi na hii ikumbukwe hao ni watu wanaoishi na wamiliki wa ardhi katika maeneo husika.

Meneja Biashara kampuni ya upimaji Viwanja Tanzania, Filbert Kato anasema baadhi ya kampuni zilizopewa dhamana ya kuuza viwanja hawana utaratibu wa kutoa ushauri kwa wateja wao na kusababisha migogoro na ujenzi holela.

“Sisi kampuni yetu tumekwenda mbali zaidi hatuishii kuuza tu, pia tunamshauri mteja anunue kiwanja cha aina gani hususani wanaovitumia kwa makazi na tunatumia fursa hiyo kumsaidia kupata hatimiliki na vibali vya ujenzi, akivihitaji,” anasema.

Pia ameshauri kwa kampuni zinaouza viwanja ziwe na taarifa sahihi za sehemu zinazouzwa, zisiishie tu kuuza bali zimsaidie mteja na kumtoa kwenye mateso ya migogoro ya ardhi baadaye.

Kauli ya Serikali

Kamishna Msaidizi wa Ardhi Tanzania, Idrisa Kayera anasema vibali vya ujenzi kisheria hutolewa kuwa maeneo yote wakati wa ujenzi, hususani yaliyopangwa na kupimwa.

Ili kudhibiti ujenzi holela wameamua kuunda kamati za urasimishaji ardhi kwa kuitisha mikutano kwenye mitaa inayokutanisha wananchi wa eneo husika na watu wa kurasimisha kwa kuteua watu wenye elimu kidogo kuhusu masuala ardhi na fedha ili kusimamia shughuli hiyo.

Anasema Serikali inatafuta kampuni ili kuandaa mpangomji katika eneo husika baada ya maeneo hayo kuanza kujengwa bila kupimwa.

Anasema kampuni hiyo itaboresha ili kuwa na maeneo ya miundombinu ikiwemo barabara, maeneo ya wazi na huduma nyingine.

“Miundombinu yote inapatikana kwa njia ya kushirikishana kwa kila mmoja kutoa baadhi ya kipande cha ardhi, japokuwa wananchi bado ni wagumu kuelewa. Pia ni haki yao wanaotakiwa kupata fidia ili kuwezesha kupata hayo maeneo,” anasema Kayera.

Pia, Kayera anasema Serikali inaendelea kukutana na changamoto ya makazi yasiyopimwa kutokana na ukosefu wa fedha kwa muda mrefu ili kuweka mipango miji na kupima maeneo yanayomilikiwa na watu binafsi.

“Kuna fedha zilitolewa mwaka jana, Sh50milioni, kwa mkopo kwenye halmashauri kwa ajili ya kuhakikisha wanatoa maeneo yaliyopimwa kwa ajili ya kuuza au kugawa kwa wale wahusika waliokubaliwa kwenye maombi ya umiliki wa ardhi,”anasema.

Kayera anasema maeneo mengi yameandaliwa michoro ya mipango miji huku makamishna ardhi wakipewa maelekezo kwenda kwenye mitaa kutoa elimu.

Mkakati mwingine ni pamoja na kuendelea na uhamasishaji wamiliki wa mashamba kuhusu michoro hiyo ili waweze kuacha barabara na maeneo mengine kwa matumizi ya kijamii.

Hata hivyo Kayera anasema changamoto ni kukosekana fedha za kulipa fidia kwa watakaotoa maeneo yao kwa ajili ya miundombinu.

“Kwa sheria ya Tanzania mtu hawezi kuachia eneo lake hadi alipwe fidia, hivyo mambo mengine ni kushawishiana na kubembelezana ili waweze kukubali kuachia sehemu ya maeneo yao,” anasema.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi