Kitaifa
Samia ataka namba monja ya utambuzi
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemwagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na namba moja ya utambulisho inayotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).
Rais Samia ametoa maagizojana jijini Dar es Salaam wakati akizindua huduma ya intaneti ya kasi mpya ya 5G kwa Kampuni ya mawasiliano ya Airtel Tanzania pamoja na mkongo wa mawasiliano wa baharini.
Vilevile, Rais Samia alielekeza taarifa za Mtanzania zianze kuchukuliwa baada ya mtoto kuzaliwa na apewe namba yake ambayo ataitumia katika kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na Taasisi za umma.
Rais Samia alitoa maelekezo hayo jana, ikiwa imepita wiki moja tangu Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliposhauri kuongeza wigo wa utoaji wa vitambulisho vya Taifa kuanzia mtoto anapozaliwa ili Watanzania wajumuishwe kwenye huduma rasmi za kifedha.
Taasisi zisomane
Akifafanua suala hilo, Rais Samia alisema wizara na taasisi zote zinazotoa huduma kama vile Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu, zitumie namba moja ya Mtanzania (utambulisho wa kitaifa).
“Anapoambiwa Samia ni namba 20, basi taarifa zangu zote, taasisi zote zikivuta namba 20, awe ni Samia Suluhu mmoja yuleyule, taarifa zilezile kwa sababu sasa hivi naweza nikawa namba 20 Nida, lakini nikienda benki kuna taarifa nyingine, nikienda afya ninakotibiwa, taarifa nyingine, shule nilikosajiliwa taarifa nyingine.
“Hii inafanya hata usalama ndani ya nchi unakuwa na wasiwasi kidogo, unataka kujuana nani ni nani, mwenyeji wa Tanzania ajulikane, mgeni aliyepo tumjue huyu ni mgeni,” alisema.
Rais Samia alisema hiyo itasaidia hata kupunguza usumbufu kwa wananchi wanapokwenda kupata huduma, wakiambiwa wapeleke taarifa lukuki kutoka kwenye Taasisi tofauti au barua ya Serikali ya mtaa anaoishi.
“Kwa hiyo mkitumia namba moja inayonitambulisha Samia Suluhu, kila taasisi ikifungua ni namba ileile, ni Samia yuleyule. Hii itatupunguzia ninapokwenda kutaka huduma, ninaambiwa lete hiki, lete hiki, lete barua ya mtendaji,” alisisitiza.
Rais Samia alimtaka kila Mtanzania ahakikishe taarifa zote alizozitoa Nida ni sahihi, kama haziko sahihi aende akarekebishe ili atambulike kwa taarifa hizo alizozitoa na hapo wataweza kujua nani ni nani ndani ya nchi.
“Kwa hiyo nitoe wito huo kwa taasisi zote zinazotoa huduma kwa Watanzania kutumia namba moja ya Nida na hii itarahisisha huduma kwa Nida kwamba kuna namba wanazitoa kwa Watanzania.
“Kwamba akizaliwa leo (mtoto), akipewa tu kile cheti na hospitali, kwamba Mtanzania kazaliwa, wa kike au wa kiume, ameingizwa kwenye mtandao, automatically (moja kwa moja) apate namba yake na taarifa zake tuanze kuzikusanya kuanzia siku ile kazaliwa.
“Tunaanza na taarifa zake za hospitali, kazaliwa hospitali gani, saa ngapi, jinsia yake, kilo (uzito) yake alipozaliwa, ana afya au hana, ili taasisi nyingine ziweze kuchukua hizo taarifa na kumfanyia kazi huyu Mtanzania. Niombe sana watu wa wizara, waziri mkuu uko hapa, naomba ulisimamie hilo,” alisema.
Wakati Rais Samia akisema hayo, mtaalamu wa mifumo katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Lazaro Kumbo alisema changamoto iliyopo katika utekelezaji wa suala hilo ni kukosekana kwa sera inayoelekeza taasisi zote kuwa na mfumo mmoja wa kuwasiliana.
“Serikali imeshindwa kutengeneza mfumo huo ambapo kila taasisi inafanya kazi kwa kujitegemea, ndiyo maana ukienda Uhamiaji na Nida wanahitaji namba tofauti sawa na Rita, ni changamoto ambayo Serikali inashindwa kuunganisha taasisi zake,” alisema.
Kumbo alisema kinachopaswa ni kuwepo na sera ya kutambua watu, itakayoweka utakaokuwa unatoa namba kwa kila Mtanzania bila kujali yuko wapi, mathalan mtoto anapozaliwa taarifa zake zinajazwa.
Pia, alishauri ni jukumu hilo ipewe Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) na si Nida kwa sababu watoto watatengwa. Nida ikipewa mamlaka itakuwa inashughulika na watu kuanzia miaka 18 na watoto wadogo watasahaulika.
“Kwa maoni yangu Rita wanapaswa kupewa jukumu hilo kwa sababu wanashughulika na vyeti vya kuzaliwa na vifo au mamlaka hizo mbili ziunganishe nguvu zifanye kazi pamoja,” alisema Kumbo.
Katika hatua nyingine, Rais Samia alimwelekeza pia Waziri Mkuu Majaliwa aliyekuwepo kwenye hafla hiyo, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Wakala wa Serikali Mtandao (eGA) kuhakikisha taasisi za Serikali zinaunganishwa na mawasiliano ya mtandao.
“Serikalini kwetu bado hatujajipanga vizuri, matumizi ya mtandao huu bado hatujayatumia vizuri, naomba tujipange tufanye tathmini, tunahitaji kiasi gani kuziunganisha wizara na taasisi za Serikali kutumia mitandao.
“Kama ni mafunzo kwa watendaji, mafunzo yafanyike, Serikali iende kwenye mtandao. Tukifanya hivyo tutanusuru mambo mengi; kwanza, taarifa kupotea lakini pili, ufanisi ndani ya taasisi za Serikali utaongezeka,” alisema.
Rais Samia aliongeza kuwa: “lazima tuelekee huko, hatuwezi kuimba kwenye majukwaa ‘uchumi wa kidijitali’, maofisini kwetu bado tuna hizo traditional methods (njia za kizamani) za kufanya kazi, haiwezekani.”
Gazeti hili lilizungumza na Mkurugenzi wa Tehama katika Wizara ya Mawasiliano, Mohamed Mashaka kujua uwezekano wa hilo, alisema kwa sasa wanatengeneza mazingira wezeshi ya kuunganisha mifumo na Nida na wataanza kutoa kitambulisho tangu mtu anapozaliwa.
Kwa upande wake, Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Subira Kaswaga alisema mamlaka hiyo ni taasisi ambayo jukumu lake la msingi ni kuratibu, kusimamia uzingatiwaji wa sera, sheria, kanuni, viwango na miongozo katika taasisi za umma.
“Jukumu hili tumepewa kuhakikisha Tehama inatumika kwa usahihi na usalama katika taasisi za umma kwenye utendaji wake wa kazi na utoaji huduma kwa mfumo wa dijitali kwa wananchi popote walipo na kumpunguzia gharama,” alisema.
“Mamlaka imetengeneza mfumo wa kubadilishana taarifa serikalini ambao unaunganisha mifumo mingine ya Tehama katika taasisi za umma iweze kuzungumza pamoja na kubadilishana taarifa, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi kwa utendaji kazi na kuokoa muda,” alisema.
Mapema, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema mkongo wa baharini wa “To Africa” ndio mrefu zaidi duniani, hivyo wamefanya jambo kubwa.
“Mkongo huu una urefu wa kilomita 45,000, unaunganisha zaidi ya nchi 33 duniani, unaunganisha mabara matatu ya Afrika, Asia na Ulaya, unategemewa kuunganisha watu zaidi ya bilioni 3 duniani. Kwa hiyo ni uwekezaji mkubwa sana.
“Mkongo huo umejengwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa zaidi, kwa sasa mikongo mingine ina kasi ya 16 terrabyt per second (kwa sekunde), mkongo wa To Africa una kasi ya 180 terrabyt per second, mara 11.25 zaidi ya kile tulichonacho sasa, hili jambo ni kubwa,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Airtel Tanzania, Dinesh Balsingh aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa msaada wanaowapatia na kuwa kuzinduliwa kwa mkongo huu wa mawasiliano na huduma ya 5G utasaidia kuongeza matumizi ya dijitali nchini.