Kitaifa
Hospitali ya Muhimbili kujengwa upya
Dodoma. Serikali imesema itaijenga upya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya kupata mkopo nafuu kutoka Benki ya Exim ya nchini India wenye thamani ya zaidi ya Sh600 bilioni.
Hayo yalielezwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa MNH, Profesa Mohamed Janabi, wakati akielezea utekelezaji wa majukumu na mwelekeo wa hospitali hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.
“Sasa hivi tupo katika upembuzi yakinifu, maana yake hospitali itabomolewa na kuanza ujenzi upya, lakini itakwenda kwa awamu, si kwamba itabomolewa yote kwa wakati mmoja,” alisema Profesa Janabi.
Alisema kwa kushirikiana na Serikali, wataacha jengo moja kama lilivyo kwa ajili ya kumbukumbu kwa kizazi kijacho.
Profesa huyo alisema mkopo nafuu wa zaidi ya Sh600 bilioni walizopokea kutoka Benki ya Exim Korea ndizo zitatumika kuijenga upya hospitali hiyo na utalipwa kwa miaka 25.
Akizungumzia huduma ya kupandikiza mimba (IVF), Profesa Janabi alisema itaanza kutolewa mwishoni mwa mwaka huu.
“Tuna wataalamu wameshasoma, lakini tutakapoanza kutoa huduma hii, tutawatumia kwanza wataalamu wenye uzoefu mkubwa kutoka nje kusudi wawape uzoefu wataalamu wetu,” alisema Janabi.
Alisema gharama za huduma hiyo zitajulikana baada ya kukamilika kufungwa kwa mitambo hiyo, huku akisema hazitakuwa sawa na zile za kwenda nje ya nchi.
Washindwa kukaa na puto
Kwa upande wa huduma ya uwekaji maputo kwa watu wenye uzito mkubwa, Profesa Janabi alisema jumla ya watu 128 wamepatiwa huduma hiyo, lakini watatu walishindwa kukaa nayo.
“Siku hizi tunakupandikiza siku hiyo hiyo hatulazi mgonjwa tena na hawa watatu walioshindwa kukaa nayo ni kwa sababu ya miili yao ilishindwa kuhimili kitu kigeni,” alisema.
Wanafunzi wa Sudan
Akizungumzia wanafunzi wa udaktari kutoka nchini Sudan, Profesa Janabi alisema hospitali hiyo hupokea wanafunzi kutoka mabara mbalimbali, ikiwemo Ulaya kwa ajili ya kujifunza kama ilivyo kwa wanafunzi kutoka nchini Sudan.
Alisema wanafunzi hao wapo kwa kipindi cha miezi mitatu na huu ni mwezi wao wa mwisho na kwamba baada ya hapo, utaratibu mwingine utafuata kwa kuzingatia hali ya amani nchini kwao.
“Wanafunzi hawa pia wanamaliza masomo yao, hivyo baada ya hapa vyuo vyao vitajua ni wapi wanakwenda kufanyia mitihani yao ya mwisho,” alisema Profesa Janabi.