Kitaifa
JESHI LA POLISI LAWAONYA WACHOCHEZI WANAOPANGA MAANDAMANO
Kamanda wa Polisi Tanzania, IGP Camilius Wambura amewataka wanaoandaa maandamano Nchi nzima ili kuiangusha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wasitishe uchochezi huo mara moja na kusisitiza kuwa huo ni uhaini na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Amesema hayo leo Jijini Dar es salaam baada ya taarifa zilizoanza kusambaa siku ya jana katika mitandao ya kijamii zinazohusisha kundi la Watu wanaoandaa maandamano nchi nzima ya kuiangusha Serikali baada ya kushindwa kesi waliofungua dhidi ya Serikali kuhusu uwekezaji bandarini.
“Huu ni uhaini. Jambo la kwanza, wakome kabisa na wasitishe matamshi yao ya kichochezi. Lakini jambo la pili, niwape taarifa tu kwamba watachukuliwa hatua za kisheria kwa uchochezi wanaoufanya, uhaini wanao-plan wote ni makosa ya jinai, niwaataarifu Jeshi letu la Polisi ni Jeshi imara sana wasitikise kiberiti,” alisema na kuendelea.
“Tutakuwa tayari kuwashughulikia wale wote wanaojaribu kufanya uchochezi na vitendo vya uhaini kwa hali yoyote, maana kumekuwa na upotoshaji mwingi na Jeshi la Polisi haliwezi kuwavumilia watu hawa,” alisema IGP Wambura, huku akiwashauri Watanzania kutowaamini wale wanaojaribu kufanya ushawishi na uchochezi katika Taifa letu.