Connect with us

Kitaifa

Rais Samia ataka unafuu mbolea ya ruzuku

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemwagiza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kukaa na Wizara ya Fedha ili kuangalia gharama za usambazaji wa mbolea ya ruzuku kwa lengo la kuleta unafuu kwa wakulima.

Rais Samia ametoa agizo hilo, leo Jumatano Agosti 8, 2023 katika kilele cha maonyesho ya Wakulima, Nanenane yanayofanyika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Maonyesho ya mwaka huu, yamebeba kauli mbiu ya ‘vijana na wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula’. Ambapo Rais Samia amesema kauli mbiu hiyo inalenga kutambua mchango wa vijana na wanawake katika kilimo, mifugo na uvuvi.

Rais Samia amesema moja ya changamoto iliyojitokeza msimu uliopita ni kuifikisha mbolea ngazi ya kata, akisema bei ya mfumo ilikuwa Sh 70,000 kwa mfuko mmoja.

“Sasa mara hii ni Sh 85,000 pamoja na gharama ya kufikisha mbolea kwa wakulima, nikuagize waziri (Bashe) angalieni namna ya kupata gharama za usambazaji angalau kwa mawakala wakubwa ili kuleta ahueni kwa wananchi angalau Sh5, 000 itolewe.

“Serikali ichangie na wakulima achangie ili mbolea ifike tumsipe mzigo mkubwa sana mkulima, naomba mkazitazame bei za mbolea,”amesema.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea ili kuongeza uzalishaji wa mazao, huku akiwaomba wakulima kuendelea kujisajili na kuhakiki taarifa zao za usajili ili kuwezesha kununua mbolea hiyo.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema ajenda ya Serikali ni kuongeza mchango wa sekta ya kilimo hadi asilimia 10, kufikia mwaka 2030 akisema uwezekano huo upo.

Amesema ndio maana Serikali inaelekeza nguvu katika sekta ya kilimo, ambapo pia kuna masuala ya uvuvi na ufugaji yamepewa umuhimu mkubwa.

Katika kufanikisha hilo, Rais Samia amesema Serikali imechukua hatua kadhaa katika kuelekeza nguvu ikiwemo kuongeza bajeti za sekta husika ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“Lengo la Serikali ni kutumia hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, ambapo kwa sasa zaidi ya hekta 700,000 ndizo zinazotumika katika umwagiliaji na milioni 28 zimebaki,”amesema.

Mbali na hilo, aliwataka maofisa ugani kukaa katika maeneo waliopangiwwa ili kuwasaidia wakulima na wafugaji kwa kuwapatia utalaamu na mbinu za kisasa za uzalishaji.

Pia alikubaliana na ombi la mbunge wa Mbeya Mjini aliyeomba muda wa maonyesho hayo kuongezwa kwa siku saba ili kutoa fursa kwa wananchi kufanya biashara zao hadi pale mamlaka zitakapoanza mchakato wa kuuboresha viwanja hivyo.

“Naungana na Spika (Dk Tulia) kutoa wiki moja zaidi kwa wawekezaji hasa wale waliotoka nyanda za juu kusini ili kuendelea kuonyesha na kuchukua vifaa. Nimwagize Bashe aongeze siku nyingine saba,” amesema.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi