Kitaifa
Waziri Ulega ‘amkuna’ Rais Samia mradi wa BBT
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amesema mradi wa kuwezesha vijana kujitegemea maarufu ‘BBT’ (Bulding Better Tomorrow) umeichangamsha Wizara ya Mifugo na Uvuvi, akisema hiyo ndio maana ya uchumi wa buluu.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumanne Agosti 8, 2023 katika maonyesho ya Wakulima maarufu Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya. Rais Samia ameeleza hayo akiwa katika banda la mifugo.
“Nakumbuka mwaka jana (wakati wa uapisho), nilisema kuwa sitosema tena (kuhusu wizara ya mifugo), lakini mmechangamsha vizuri vijana wameingia katika ufugaji,” amesema.
Machi mwaka 2022 akiwaapisha baadhi ya mawaziri akiwemo Ulega, Rais Samia alimtaka waziri huyo kuhakikisha anafanya kazi kwa bidii akisema anataka kuona wizara ya mifugo na uvuvi ikinyanyuka.
“Nakuamini na nadhani utaweza, kama wakati ule ulikuwa hufanyi kwa sababu ulikuwa chini ya mtu, sasa utaonekana unafanya kwa sababu hauko chini ya mtu au na wewe utakuwa kama wale. Safari bado ni ndefu tuna miaka miwili mbele yetu, nikuombe sana ukafanye kazi,” amesema Rais Samia na kuongeza;
“Nashukuru BBT imeichangamsha wizara kilichonifurahisha huyu (mnufaika wa BBT-uvuvi kutoka Geita) kuzungumzia unenepeshaji wa kaa na majongoo bahari, ameeleza kama amezaliwa yaliko. Hii ndio faida ya Tanzania.”
Pia Rais Samia amewaambia vijana kuwa anazunguka ulimwenguni kutafuta fedha nje ya bajeti ya Serikali, kwa ajili yao akitambua kupitia kilimo cha mazao na ufugaji wa samaki, nyuki na misitu, ndiko kundi hilo litakapopata ajira.
“Niwatie moyo, mama nipo naendelea kutafuta fedha, fanyeni kazi,” amesisitiza Rais Samia wakati akizungumza na vijana wa BBT wa uvuvi walionufaika na mpango huo.
Michael Tadeo ni miongoni mwa wanafuaika BBT- uvuvi, amemweleza Rais Samia kupitia mpango huo, wamefundishwa kunenepesha majongoo bahari na kaa.
“Tukiwa katika vituo tumejengewa uwezo kuhusu viumbe vya maji chumvi na baridi, mheshimiwa Rais (Samia) tumefundishwa kuhusu unenepeshaji wa kaa ambao wapo hatarini kupotea kutokana na uhitaji wake na thamani,” amesema Tadeo.
Awali Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema wamenunua boti 160 za kisasa, ‘cage’ maalumu za kufugia sato, na akamuomba Rais Samia kwenda kuzikabidhi kwa vijana na kina mama mkoani Mwanza.