Connect with us

Kitaifa

Ripoti Maalumu: Maduka ya mangi yaliyogeuka ‘baa bubu’, chanzo cha upotevu mapato serikalini

Dar/mikoani. Ni jambo la kawaida kuwapo kwa maduka yauzayo bidhaa mbalimbali mitaani maarufu kama ‘Kwa Mangi’ katika maeneo mbalimbali nchini, uchunguzi wa Mwananchi Digital umebaini mengi ya maduka haya yamegeuka kuwa ‘baa bubu,’ kwa kutoa huduma ya vileo bila kuwa na leseni kutoka mamlaka husika, huku mabilioni ya fedha ya mapato ya Serikali yakipotea kutokana na hali hiyo.

Kauli hii inathibitishwa na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za mwaka wa fedha 2020/21 pamoja na ile ya 2021/22 zinazoonyesha kuwapo kwa upotevu wa Sh961.8 milioni na Sh1.71 bilioni mtawalia kutokana na halmashauri kushindwa kukusanya fedha kutokana na kusimamia leseni za vileo.

“Halmashauri 59 pekee kati ya 149 zilikusanya mapato yote kutokana na kudhibiti leseni za vileo kwa mwaka wa fedha 2021/22,”imesema ripoti hiyo, ambayo inamaanisha ni asilimia 39.5 ya halshauri zote nchini zinazuia upotevu huu.

Hili ni sawa na ongezeko la asilimia 78 la upotevu wa fedha katika leseni za vileo kwa mwaka 2021/22 ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2020/21.

Uchunguzi uliofanywa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Kilimanjaro umegundua kuwa maduka hayo yaliyogeuka baa, bila kuwa na leseni; hasa zinazohusika na kuuza vileo vya aina mbalimbali.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, amekiri kwamba, kutokuwa na leseni ya biashara husika kunaweza kusababisha mwanya wa kukwepa kodi na kufifisha mapato huku akiahidi kulifuatilia jambo hilo.

“Kwa kawaida biashara zote lazima ziwe na leseni, kama wanauza kwa watu lazima watoe risiti, ndio maana tunasema maduka yote lazima yawe na leseni na hayo ya vinywaji yana leseni maalumu pia,” amesema.

“Tutalifanyia kazi kuona hilo, kama ni maduka yote au sio yote (yanayohusika)… baada ya kufuatilia tutajua kama ni rejareja au jumla ili kuona namna ya kukabiliana na hali hiyo,” ameongeza.

Mbali na kutia hofu ya upotezaji wa mapato kwa njia ya kodi kwa Serikali lakini biashara hii ni kicheko kwa wateja na wauzaji ambao wote hufaidika kwa namna tofauti.

Ripoti Maalumu: Maduka ya mangi yaliyogeuka ‘baa bubu’, chanzo cha upotevu mapato serikalini

Kwa upande wa wateja wa vileo katika maduka hayo, wanasema ukaribu uliopo na makazi yao ndio sababu kubwa inayosababisha kustawi kwa biashara hiyo katika maduka ya mangi huku wakiwa na uwezo wa kukopa bila kuwa na wasiwasi tofauti na baa za kawaida.

 “Hapa ni karibu na nyumbani nina uwezo wa kunywa bia na kurudi kwa urahisi bila kuwaza usafiri. Pia nikimaliza kunywa ninachukua na mahitaji mengine kama mafuta na mchele kwa ajili ya familia,”amesema Raphael Mushi Mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro.

Candy Buguni, mkazi wa Mabibo jijini Dar es Salaam anasema ni rahisi kwenda kukopa bila wasiwasi kwani muuzaji anafahamiana naye na ni mteja wake wa muda mrefu.

“Kwa mangi naweza kuchukua bia bila kuwa na fedha lakini ananiamini kwasababu ni jirani yake na pia mteja wa muda mrefu, tofauti na baa ambayo lazima niwe na fedha za kutosha ili ninywe,”amesema.

Jerome Macha, mmiliki wa duka katikaMtaa wa Mwananyamala Kwa Mama Zakaria jijini Dar es Salaam anasema mara nyingi huuza pombe wakati wa usiku watu wakirudi kazini lakini mchana anauza pombe kali za kupima huku wateja wake wakubwa wakiwa waokota chupa za plastiki.

“Hapa mchana tunauza pombe kali za kupima na wateja wengi wanakuwa wale wanaookota makopo na vyuma. Wakati wa usiku watu mbalimbali wakirudi kazini wanapitia kinywaji (pombe) kwaajili ya kuburudika,”amesema.

Macha amesema dukani kwakwe ana kipimo cha pombe kali kuanzia Sh200 hadi Sh1,000 inategemea na fedha ya mteja, jambo linalotajwa kuwavutia zaidi wanywaji.

Ukizungumzia uuzaji wa pombe katika maduka ya Mangi pia huwezi acha kulitaja Jiji la Mwanza ambapo, Yusuph Kinema (si jina halisi) Mkazi wa Kijiweni Kata ya Nyegezi anasema wanauza vileo bila leseni kutokana na kuhofia gharama katika leseni huku wakitaka kupata faida zaidi.

“Ukisema uuze kwa uwazi TRA (Mamlaka ya Mapato) na watu wa jiji wanakutaka uwe na leseni tofauti za bidhaa na vinywaji kitu ambacho kinatufanya tuuze kwa  kwa kificho ili tuweze kupata faida,” amesema.

Henry John (si jina halisi), muuza duka wa Moshi Mjini anaungana na hoja ya Kinema wa Mwanza kuhusiana na kuhofia gharama kubwa katika ukataji wa leseni za vileo.

 “Kuhusu kibali cha kuuza pombe inakuwa ngumu kwetu kufanya hivyo kutokana na mtaji wetu wa biashara kuwa mdogo hivyo tunahofia kodi inaweza kuwa kubwa,”

Kuhusu hoja inayoibuliwa na wafanyabiashara kuogopa kukata leseni ya vileo katika maduka yao kwa hofu ya gharama, Mwananchi Digital imefanya uchunguzi na kugundua pengine ni kukosekana kwa elimu sahihi kwa wafanyabiashara hao kwani bei ya leseni hiyo ni Sh30,000 hadi Sh40,000 kwa miezi sita.

Kwa upande wake, Afisa Biashara wa Manispaa ya Moshi Mjini, Prosper Msele  anasema katika eneo lake wafanyabiashara wengi wanauza vileo bila kuwa na leseni huku akisisitiza ni kosa kisheria.

“Changamoto iliyopo wengi wanakiuka wanauza bidhaa za kawaida na wanauza vileo bila kuwa na leseni. Hii ni kinyume na sheria ya vileo ya mwaka 1998 inayowataka wauzaji wote wa vileo kupata leseni ya biashara hiyo,”amesema.

Msele amesema leseni ambazo muuza vileo anapaswa kuwa nayo ni ile ya ithibati au ya groceries (duka lenye bidhaa na vileo) ambalo linamtaka mtu kunywea nyumbani baada ya kununua na visitumiwe hapo.

Hata hivyo suala la kunywea pombe mbali na duka ni jambo lingine ambalo linakiukwa na wengi huku katika Jiji la Dar es Salaam, maduka mengi ya Mangi wakati wa usiku hugeuka kuwa baa ambapo wanywaji hukusanyika na kunywa katika eneo hilo.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa mlipa kodi TRA, Richard Kayombo amesema kwa upande wao wanahakikisha wanatoa namba ya mlipa kodi kwa mfanyabiashara (TIN) huku upande wa kufuatilia ni biashara gani inauzwa na eneo linakuwa chini ya Halmshauri husika.

“Sisi kama TRA tunatoa namba ya mlipa kodi (TIN) kwa ajili ya biashara ila kuhusu aina ya biashara na anaenda kuuza wapi na kitu gani, ni manispaa inahusika na hilo,”amesema alipoulizwa kuhusu kuyatambua maduka hayo ya mtaani yanayouza vileo bila leseni.

Wachumi washauri

Mchumi Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora anasema maduka haya kutokuwa na leseni ina athari katika mapato ya Serikali lakini pia inaleta ukakasi katika upimaji wa uchumi wa Taifa.

“Biashara hizi ni zinaitwa dead asset (mali mfu) zinashindwa kuingizia Serikali mapato lakini pia zinakwamisha upimaji sahihi wa ukuaji wa uchumi kutokana na kutokuwepo uhalisia katika urari wa mapato ya Taifa,” amesema.

Profesa Kamuzora, ameshauri Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara hasa wadogo ili warasimishe biashara zao na kuwe na rekodi sahihi.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi