Kitaifa
CCM yapiga marufuku ‘chawa wa mama’
Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepiga marufuku kundi la ‘chama wa mama’ kikieleza dhamira yao ni kusaka madaraka tu.
Chama hicho pia kimetoa maelekezo ya kubadilishwa jina kutoka ‘chawa wa mama’ na kuwa ‘watetezi wa mama’ ambao watakuwa wamejitambulisha kutoka nje ya chama na siyo waliopo ndani ya jumuiya tatu za CCM zinazotumia majukwaa yake kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan.
Katibu wa chama hicho Wilaya ya Ilala, Frata Katumwa akizungumza na wajumbe wa baraza la wilaya hiyo la Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) wiki mbili zilizopita, alisema uamuzi huo ni maelekezo ya Halmashauri Kuu ya chama hicho iliyokutana Julai 9, mwaka huu.
“Kuna maagizo maalumu ambayo sitakosa kuyaeleza katika hili baraza na nina uhakika mtendaji wa UWT utakuwa umeshapokea maelekezo hayo kutoka Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama, kikao kilichofanyika juzi (Julai 9, 2023), kuna kikundi kimeibuka kinajiita chawa wa mama,” alisema Frata katika video inayosambaa mtandaoni.
“Huwezi kuanzisha chama ndani ya chama, wanajivisha kivuli cha chawa wa mama, lakini malengo yao ni kutafuta uongozi, kuunda makundi ndani ya chama ili kutafuta nafasi, hili haliwezekani. Kama wanataka chawa wanashauri jina libadilike kuwa mtetezi wa mama. Lakini wafuate taratibu, sasa kinachoshangaza UWT, UVCCM, JWT wana msemo wa chawa wa mama. Sasa ukiwa chawa wa mama ndiyo utamsemea vizuri? Tunachojichanganya ni nini?” alihoji Frata.
Juhudi za kupata uongozi wa juu wa CCM kuzungumzia suala hilo ziligonga mwamba, baada ya simu ya msemaji wa chama hicho, Sophia Mjema kutopatikana, huku Katibu Mkuu, Daniel Chongolo akiwa kwenye kikao kwa mujibu wa taarifa za msaidizi wake aliyepokea simu.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Frata alisema anaamini maelekezo hayo yalikuwa ya nchi nzima, licha ya kupokea barua inayohusisha wilaya yake.
“Ninaamini maagizo yalikuwa ya nchi nzima, sasa siwezi kusemea hilo ila mimi nilipewa barua na tayari grupu lao (WhatsApp) wamefuta jina la chawa,” alisema.
Katika ufafanuzi wake, Frata alisema chama hicho hakikatai uanzishaji wa kundi linalomuunga mkono Rais Samia, lakini lisihusishe mwanachama anayetoka ndani ya jumuiya tatu za chama hicho.
“Katiba yetu ya chama iko wazi, huwezi kuanzisha chama ndani ya chama, wanajivalisha kivuli cha ‘chawa wa mama’ kumbe wana malengo ya kutafuta uongozi, hili haliwezekani..’’ alisema.
Alichosema Rais Samia
Msingi wa kuibuka kundi hilo hadharani ulitokana na kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan ya Januari, mwaka huu kuhusu chawa wake watakaomsaidia kwenye siasa dhidi ya vyama vya upinzani.
Akizungumza na viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa Ikulu, Dar es Salaam, Rais Samia alitangaza kuruhusu mikutano ya hadhara ya kisiasa, huku akiwasihi wanasiasa kufanya siasa za kistaarabu na siyo kutukanana majukwaani. Alisema yeye anaweza kuvumilia lakini ‘chawa wake’ wanaweza wasistahimili.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chawa wa Mama Tanzania(Chamata), Maimartha Moshi alisema agizo hilo halihusishi mabadiliko katika chama hicho, ambacho tayari kimeshasajiliwa na kufikisha wanachama milioni 1.8 waliojisajili
“Chama hiki kitaendelea na majukumu yake bila kubadili jina, ndio jina tulilosajili na tumekuwa tukitekeleza majukumu mbalimbali ya kusaidia wananchi watambue kazi zinazofanywa na mama (Rais Samia Suluhu Hassan),”alisema Maimartha.
Walichosema wachambuzi
Uamuzi huo umepokewa kwa mtazamo chanya na wachambuzi wa siasa, walioshauri CCM kuwekeza kwa vijana wanaojenga hoja, badala ya kuendelea kutumia jina hilo linalodhoofisha heshima ya chama na Rais Samia aliyekuwa na dhamira njema juu ya msamiati huo.
Wachambuzi waliozungumza na gazeti hili walisema tafsiri ya ‘chawa’ katika jamii ni mtu, kundi linalojipendekeza ‘kulamba miguu’ ya watu wenye kipato au mamlaka kwa lengo la kujipatia manufaa fulani bila kujali uwezo wao au ushawishi wa hoja zao kwenye jamii.
Mchambuzi wa siasa na wakili wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke alisema uamuzi wa kuzuia kundi hilo, utasaidia kurejesha utulivu, huku akishauri uwekezaji kwa vijana wanaojenga hoja. “Hilo kundi halina msaada wowote kwenye siasa zake, chawa ni blinded follower (mfuasi asiyejitambua)” alisema Kyauke.
Dk Richard Mbunda, mhadhiri mwandamizi idara ya sayansi ya siasa na utawala bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema kundi hilo lingeendelea kudhoofisha heshima ya chama hicho.
“Jina linabeba heshima ya chama na viongozi wake, kwa kuwa na wanachama wanaojipendekeza,” alisema na kuongeza:
‘‘Athari zake ni kwamba Rais ni mwanasiasa ambaye ni binadamu anayeweza kukosea na tunatakiwa kusimamia masilahi ya Taifa.’’