Kitaifa
Serikali kutumia Sh1.1 trilioni ujenzi barabara Igawa-Tunduma
Mbeya. Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kwa mara ya kwanza amefunguka na kuwaeleza wananchi jimboni kwake kuwa Serikali itatumia zaidi ya Sh1.1 trilioni mpaka kukamilisha ujenzi wa mradi wa miundombinu ya barabara njia nne.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 218 kutoka Igawa Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya mpaka wa Mji wa Tunduma, Mkoa wa Songwe mpakani mwa Tanzania na nchi jirani ya Zambia.
Dk Tulia ambaye ni Spika wa Bunge, amesema Agosti 6, 2023 kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Mwakibete jijini ambapo Naibu Waziri wa Kilimo, Athony Mavunde alishiriki.
“Ndugu zangu mradi wa barabara njia nne unahitaji zaidi ya Sh1.131 trilioni huku bajeti ya Serikali kwa mwaka huu ni Sh44 trilioni Serikali inahitaji kukusanya mapato ili kutekeleza miradi yote ya elimu, barabara, maji na afya,” amesema.
Amesema katika mipango hiyo mizuri bado kuna watu wanapita huko kuzunguka na kukashfu miradi mikubwa ya kimkakati inayoletwa na Serikali, wapuuzeni ni wapinga maendeleo walikuwa wapi wao kufanya miaka 10 iliyopita.
“Ndugu wana Mwakibete kipindi cha miaka 10 iliyopita wakati jimbo likiongozwa na upande wa pili, wananchi walikuwa wakipata adha ya maji lakini baada ya kupata ridhaa tumepata Sh1 bilioni kufikisha maji katika mitaa miwili ya Kata ya Iganzo ambayo tangu Uhuru hawajawahi kuona maji ya bomba,” amesema.
Amsema miradi yote ya kimkakati ukiwepo wa maji Mto Kiwira na barabara njia nne tayari makandarasi wamewasili kwa kuanza utekelezaji, hiyo ni nguvu ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Mkisikia miradi mikubwa nanyi inawahusu hususan sakata la bandari ambalo kuna watu wamesimamia kucha, kuwa Serikali imeuza jambo ambalo kila wakati nasimama kuzungumza kuwa bandari haijauzwa, hao wanaopita huko wapuuzeni mimi ndio mbunge wa kujiongeza,”amesema.
Aidha amesisitiza wana Mbeya Mjini wako salama katika huduma za afya, maji, elimu ikiwepo Serikali kuelekeza wananchi wa pembezoni mwa jiji kuunganishiwa nishati ya umeme kwa gharama ya Sh27,000 na kwamba CCM wako imara.
Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Kilimo, Athony Mavunde amesema kupitia Mbunge wa Mbeya Mjini, Serikali imeleta miradi mingi ya kimkakati tofauti na miaka 10 iliyopita wakati Jimbo hilo likiongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Amesema Spika amepewa dhamana ya kuwatendea haki wananchi wa Jimbo la Mbeya waliokaa juani kuhakikisha wanampa kura za kishindo na ndiyo wakati wake kutekeleza ilani ya uchaguzi 2020 kujenga hoja kwa Rais Samia Suluhu Hassan na huduma muhimu kwa jamii zinaonekana.
“WanaMbeya siri ya kiongozi mzuri ni kujenga hoja Dk Tulia alipoona adha ya foleni ya magari, alijenga hoja ambayo Serikali imeunga mkono na kuleta mradi mkubwa wa barabara njia nne na siku mkimpoteza mtakuja kunikumbuka hili ninalosema,” amesema.
Ameongeza, “Inawezekana wamemzoea, Dk Tulia ni wa kipekee wanapaswa kutambua wametoka kwenye siasa za uharakati siasa za leo ni kuleta maendeleo ya watu mnapaswa kumtumia ili atimize malengo yake kwa wanambeya,”amesema Mavunde.
Katika hatua nyingine baadhi ya makada waliokuwa Chadema na kuhamia CCM waliwashtua wananchi walipotoa ushuhuda wa kufanya matendo maovu dhidi ya Serikali ya CCM katika kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015-2020 kwa kuteka watu, kuharibu miundombinu ya barabara na matukio mengine mabaya.
Awali aliyekuwa Kada wa Chadema, Lucas Mwampiki amesema amerejea CCM.
“Nimefanya mambo mengi makubwa na mabaya kwa lengo la kuidhoofisha Serikali ya CCM katika chaguzi zilizopita hatimaye mwenyewe kwa hiari yangu nimerejea,”amesema Mwampiki.