Kitaifa
CBT, NIMR kuchunguza korosho kuongeza nguvu za kiume
Lindi. Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Brigedia Jenenari Mstaafu, Aloyce Mwanjile amesema kuwa bodi hiyo ipo mbioni kufanya mazungumzo na Taasisi ya Utatifi wa Magonjwa ya Binadamu (Nimri) ili wafanye utafiti wa kisayansi kuhusu ulaji wa korosho kwa wanaume na mchango katika kuongeza nguvu za kiume.
Kauli hiyo ameitoa jana Jumamosi Agosti 5, 2023 katika maadhimisho ya uhamasishaji, ubanguaji na ulaji wa korosho nchini ulioandaliwa na CBT wakishirikiana na kituo cha utafiti cha Tari Naliendele, ambapo amesema kuwa wanaume wengi wanadhana ya kuwa ulaji wa korosho nyeupe unaongeza nguvu za kiume na kuleta heshima ndani ya ndoa.
Amesema kuwa utafiti huo unalengo la kutoa taarifa ya uhakika ambayo itaongeza hamasa ya ubanguaji na ulaji wa korosho nchini.
“Hivi karibuni tunajipanga tufanye mazungumzo na Nimri ili wafanye utafiti na tujue juu ya korosho na waje na majibu ya kisayansi kwa sababu ukiongea na wanadamu wengine wanakwenda mbali zaidi wakituelewesha kwamba ukila korosho inadumisha ndoa, naamini tutaongeza ulaji na kudumisha soko la ndani,” amesema.
“Inawezekana tusizungumze hili kwa kuwa hatuna mamlaka wafanye utafiti ili waje na majibu chanya wanaweza kusababisha korosho zetu kuliwa zote nchini badala ya kupeleka nje na inaweza kuwa sababu ya bei kupanda kwenye korosho,” amesema Mwanjile.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amesema kuwa wanaume wamekuwa wakisema kuwa korosho zinadumisha ndoa na kuongeza heshima nyumbani, hivyo amesisitiza utafiti ufanyike.
“Wanaume wanatuambia kuwa ukila korosho heshima inaongezeka nyumbani kwa leo watakula tuanze kufanya utafiti sisi wenyewe leo tunakula bure na kunywa bure na kesho mtupe majibu tutaulizana asubuhi mmeamkaje kuanzia hapo ndiyo tutaangalia mfano waliokula na wangapi wameamka wamesema wameamka vizuri,” amesema Telack.
“Ulaji wa korosho za ndani utaongeza kiwango cha ubanguaji nchini kutoka asilimia 10 ya sasa hadi asilimia 60 ifikapo 2026 ambapo mnyororo wa thamani katika soko la korosho utasaidia kufufua viwanda nchini,” amesema Telack.
Mratibu wa Uhaurishaji wa Teknolojia na Mahusiano Kituo cha Tari Naliendele, Rashid Kidunda amesema kuwa wameandaa maonyesho hayo kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho Tanzania ili kuongeza hamasa ya ulaji wa korosho.
“Tumekuwa tukiratibu na wadau mbalimbali na wananchi hupata fursa ya kula korosho lengo ni kuhamasisha uwekezaji katika uongezaji thamani wa korosho pamoja na mabibo kwa kuwa teknolojia hizo zipo mkulima anapoongeza thamani anapata faida Zaidi,” amesema Kidunda.
“Unajua kiasi kikubwa cha mabibo huachwa shamba na kuozea huko, zingine hutengenezewa za asili. Hivyo bado fursa zipo yaani asilimia 90 ya korosho ni bibo na asilimia 10 ndio korosho ambapo kilo moja ya mabibo unapata chupa moja ya wine yenye thamani ya Sh8,500,” amesema Kidunda.