Connect with us

Kitaifa

Ulaghai kwa simu bado, Serikali na watoa huduma wakuna kichwa

Wakati tangazo la kutaka kila laini ya simu isajiliwe kwa alama za vidole linatolewa, watu walijua ulaghai na udanganyifu kwa njia ya simu utabaki historia, lakini sasa ni takribani miaka mitano na wengi bado wanapoteza fedha kwa njia hizo.

Ripoti ya hivi karibuni ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaonyesha kuna ongezeko la matukio ya ulaghai kwa karibu mara mbili hadi kufika matukio 23,234 yaliyoripotiwa katika kipindi cha miezi mitatu iliyoishia Juni, 2023, ukilinganisha na matukio 12,044 yaliyoripotiwa katika robo iliyoishia Machi 2023.

Mkoa wa Rukwa, wenye laini za simu milioni 1.05, Morogoro (milioni 3.2) na Dar es Salaam yenye milioni 11.9 imeendelea kuongoza katika orodha hiyo katika kipindi cha miezi sita iliyopita.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mikoa miwili (Rukwa na Morogoro) ilichangia zaidi ya theluthi mbili ya matukio ya udanganyifu yaliyofanyika kwa njia ya simu.

Rukwa iliongoza kwa kuchangia matukio 8,991, sawa na asilimia 38.7, Morogoro ikifuatia kwa matukio 6,535 (28.13%), Dar es Salaam licha ya kuwa na mkoa unaoongoza kwa watumiaji wengi wa simu ulikuwa na matukio 2,999, sawa na asilimia 12.91, huku Mbeya ikiwa na matukio 1,684 sawa na asilimia 7.25 ya matukio yote.

Simiyu ndio mkoa wa Tanzania bara uliorekodi matukio machache zaidi ambapo yalikuwa 14 (asilimia 0.06) ukifuatiwa na Njombe ambao ulirekodi matukio 19 tu sawa na asilimia 0.08. Visiwa vya Zanzibar kwa ujumla wake vilirekodi matukio 14 pekee.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabiri Bakari anasema kiuhalisia idadi ya matukio ya udanganyifu kwa njia ya simu yanapungua, lakini udhibiti zaidi unapaswa kuendelea ili kuyamaliza kabisa.

Anasema TCRA inaweka wazi taarifa hizi ili kuonyesha umma kuwa matukio haya bado yanaendelea na wanapaswa kuchukua tahadhali, kila mtu katika eneo lake kadiri inavyowezekana ili kumaliza kabisa visa hivyo.

“Tunategemea viongozi wa maeneo yanayotajwa kushiriki kukomesha huu uhalifu, maana idadi inayotajwa katika mkoa si kwamba visa vimesambaa mkoa mzima, bali unakuta kuna eneo limekithiri, mfano Morogoro wilaya ya Kilosa ndiyo kuna hali mbaya zaidi,” anasema Dk Bakari.

Anasema mbali na mamlaka za utawala katika maeneo husika, pia watoa huduma za mawasiliano wanaonyeshwa taarifa hizo ili kuongeza udhibiti katika usimamizi wa laini za simu na usajili wake.

“Hiki si kitu kizuri kuonekana katika ripoti za kampuni ya simu,” anasema.

Dk Jabiri anasema hata waliotapeliwa hawakutakiwa kutapeliwa, kwani umma umekuwa ukielezwa siku zote usifuate maelekezo yanayotolewa kupitia namba za kawaida kwa kuwa namba ya mawasiliano ya mtandao wa simu ni 100 tu.

“Tunaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali, ni bahati mbaya tu wakati mwingine mtu anatapeliwa katika mazingira ambayo anachelewa kutafakari kwa kina.

“Namba zinazohusika na utapeli, vifaa vinavyotumika na kitambulisho kilichotumika kusajili vinafungiwa na kwa kushirikiana na mamlaka nyingine tunatumai kuwa tutamaliza changamoto hii,” anasema Dk Bakari.

Mtandao wa Airtel ambao unaongoza kwa kuwa na visa vingi vya matukio ya udanganyifu katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita hadi Juni, 2023 ulisema uelewa mdogo ndiyo sababu ya watu kuendelea kutapeliwa kwa njia ya simu.

Laini za mtandao wa Airtel zilihusika na asilimia 44 ya matukio yote ya udanganyifu, ukifuatiwa na Tigo kwa asilimia 33, Vodacom asilimia 18, TTCL asilimia 3 na Halotel kwa asilimia 2.

“Tunadhibiti vitendo hivi kwa kutoa elimu kwa wateja wetu mara kwa mara kupitia ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) na mitandao ya kijamii tukiwasihi kutotoa namba zao za siri, taarifa za kiwango cha fedha walichonacho na taarifa za kitambulisho chao cha Taifa,” anasema Jackson Mbando, meneja uhusiano na mawasiliano wa Airtel.

Mbando anasema mtandao huo pia unabaini SMS za ulaghai na kuwafungia kupata huduma tena na kudhibiti mifumo ya usajili wa laini za simu.

“Tunatoa taarifa za walaghai kwa watoa huduma wenzetu ili nao wazuie namba za utambulisho na IMEI za vifaa vilivyotumika kupata huduma kwenye mfumo.”

Vodacom ndiyo mtandao wenye watumiaji wengi zaidi wa huduma za simu, ukiwa na laini zilizo hai milioni 19.11, sawa na asilimia 30 ya soko na watumiaji wa huduma za miamala wapatao milioni 17.19. Licha ya ukubwa wake, mtandao huu unashikilia namba tatu kwa matukio ya udanganyifu mtandaoni.

Katika ripoti ya robo ya pili ya mwaka iliyoishia Machi, 2023 Vodacom ilichangia asilimia 28 ya matukio yote ya udanganyifu, lakini katika robo ya nne kiwango hicho kimepungua kwa asilimia 10 hadi asilimia 18 kutokana na mkakati wake wa ndani wa kudhibiti ulaghai wa simu.

“Tunatumia njia tatu kudhibiti ulaghai kwa wateja wetu na hizi zimetusaidia kupunguza kiwango, kwanza tunazuia, tunatambua na kudhibiti,” yalieleza majibu ya Vodacom walipoulizwa wamewezaje kupunguza kiwango hicho.

Majibu hayo yaliyotolewa na Meneja uhusiano wa umma wa kampuni hiyo, Alex Bitekeye yanaeleza kampuni hiyo hushirikiana na wadau wengine, ikiwemo mitandao mingine ya simu katika udhibiti huo huku ikiweka nguvu zaidi katika kutoa elimu kwa wateja wake.

“Tunajitahidi kila mara kuwaelimisha wateja wetu kuhusu mitindo mipya ya ulaghai na taratibu sahihi zilizo salama kwa huduma wanazozipata kutoka kwetu,” inaeleza taarifa hiyo.

Alisema elimu imekuwa ikitolewa katika majukwaa mbalimbali, yakiwemo yale yanayokutanisha watu, mitandao ya kijamii, SMS, matangazo ya redio na runinga kwa lengo la kuhakikisha kila mtu anaelewa.

“Tumeanzisha jukwaa maalumu la kimtandao kwa ajili ya udhibiti wa usalama ‘Bug Bounty’ ili wananchi waweze kuripoti ulaghai moja kwa moja. Juhudi zetu hizi ndizo zimetupa matokeo chanya kama yalivyo katika ripoti ya TCRA,” alisema.

Pamoja na majibu ya watoa huduma, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Usimamizi na Maendeleo ya Ujasiriamali, Dk Donath Olomi anasema tatizo ni jamii ya Watanzania inayopenda kupata fedha kirahisi na kwa kuwa haina uelewa wa kutosha wanaishia kuumizwa.

“Watu wanatumia fursa mkato, wakiambiwa ukifanya hivi na hivi unapata pesa basi wanakimbilia haraka na utapeli huu upo wa aina nyingi, kila siku unabadilika na kila siku watu wanalaghaiwa,” alisema Dk Olomi.

Alisema ni muhimu zaidi kuweka nguvu katika uelimishaji wa umma ili kuikinga jamii na ulaghai.

“Miongoni mwa majukumu makuu ya Serikali ni kuwalinda wananchi wake si tu dhidi ya uvamizi, bali hata kwa matukio kama haya ambayo yanawarudisha nyuma. Usajili wa laini kwa kutumia vitambulisho vya Taifa tulijua ungemaliza hili, lakini mambo bado,” anasema Dk Olomi, akihoji ulipo mkwamo.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi