Connect with us

Kimataifa

Sababu za kushuka kwa thamani ya sarafu za EAC

Arusha. Uzalishaji mdogo na utegemezi mkubwa wa bidhaa kutoka nje ndio unaosababisha kushuka kwa thamani ya sarafu za nchi za Afrika Mashariki.

“Usafirishaji wetu nje ya nchi ni mdogo kuliko uagizaji. Hili limeweka shinikizo kubwa kwa thamani ya sarafu zetu,” haya yanasemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC), John Kalisa.

Amesema ili kukabiliana na kuporomoka kwa sarafu, nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hazina budi kuongeza tija na thamani ya mauzo ya nje.

Akizungumza na gazeti dada la The Citizen jana jijini hapa, Kalisa alisema sababu nyingine za kushuka kwa sarafu za EAC dhidi ya sarafu za kigeni ni kuongezeka kwa deni la mataifa hayo kutokana na miradi mikubwa inayotekelezwa.

Ripoti ya hivi karibuni ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ilionyesha nchi ya Kenya ambayo ndiyo kubwa kwa uchumi (EAC), ilishuhudia kushuka kwa sarafu yake kwa kiwango kikubwa kuliko nchi nyingine ndani ya jumuiya hiyo.

“Ni rahisi kujua sababu za kwa nini Shilingi ya Kenya ilianguka, ni kutokana na athari za Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo wa mwaka jana na ukame uliolikumbwa Taifa hilo,” alisema Kalisa.
Alisema wakati huohuo; Kenya ilirekodi kiwango cha juu zaidi cha deni la nje dhidi ya Pato la Taifa (GDP) ikilinganishwa na mataifa mengine ya EAC.

“Unatarajia nini kwa nchi kutumia asilimia 60 ya pato lake la kiuchumi (GDP) kulipa madeni?” alihoji Kalisa.

Kabla ya anguko lake, Shilingi ya Kenya imekuwa yenye nguvu katika mipaka ya mataifa ya EAC ikilinganishwa na nyingine, lakini sasa hali ni tofauti.

Mpaka jana dola moja ya Marekani iliuzwa kwa Ksh142.6 (Sh2,455), Shilingi ya Uganda 3,630, Faranga za Rwanda 1,178, Faranga za Burundi 2,833 na Faranga za DR Congo 2,415).

Ripoti hiyo ya AfDB inaitaja Pauni ya Sudan Kusini kuwa ni miongoni zilizoporomoka zaidi katika kipindi cha mwaka 2022. Mpaka jana, Dola moja ya Kimarekani ilikuwa ikibadilishwa kwa paundi 130 za Sudan Kusini.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Rwanda ndiyo nchi iliyoshuhudia ukuaji mkubwa wa uchumi ndani ya EAC, uchumi wake ukipanda kwa asilimia 7.8.

Tanzania ilitajwa namba tatu, ikibebwa na kuimarika kwa sekta ya utalii huku uchumi wa Uganda ukichangamshwa na uendelezaji wa miradi ya mafuta na gesi.

Kama mtendaji wa chombo kikuu cha uangalizi wa sekta binafsi, Kalisa alisema EAC inapaswa kuacha utegemezi wa kulisha watu wake kwa chakula kutoka nje, lakini pia kukuza uzalishaji wa bidhaa muhimu ndani Jumuiya.

Hata hivyo, alipendekeza kuharakishwa kwa Mfumo wa Malipo wa Pan African (PAPS) ambao anaamini utapunguza upotevu wa viwango vya kubadilisha fedha.

Mwenyekiti wa baraza la wafanyabiashara Mkoa wa Arusha, Walter Maeda alisema kushuka kwa thamani ya shilingi kunatokana utendaji mbovu katika biashara ya nje.

“Labda hatuuzi mauzo ya kutosha. Ndiyo maana sarafu yetu inapoteza thamani dhidi ya dola,” alisema.
Aliwataka Watanzania kuimarisha uzalishaji wa mazao ya kilimo, hususani uzalishaji wa chakula ili kudhibiti kuporomoka kwa shilingi kutokana na kuagiza chakula kutoka nje ya nchi.

Reuben Mcharo ambaye ni mtaalamu wa kilimo, alisisitiza kuwa Tanzania na nchi nyingine za EAC zinapaswa kuacha kusafirisha malighafi na badala yake ziongeze thamani ya mazao ya shambani ili kukuza uchumi wake.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi