Kitaifa

Maumivu ongezeko la bei za mafuta Tanzania

Dodoma. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei ya ukomo kwa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa huku kukiwa na ongezeko katika mafuta ya petroli na dizeli.

 Bei ya mafuta petroli katika jiji la Dar es Salaam imepanda kutoka Sh2, 736 hadi kufikia Sh3,199 ikiwa ni ongezeko la Sh463 kwa lita.

Bei ya dizeli pia imepanda kutoka Sh2, 544 hadi kufikia Sh 2,935 (ongezeko la 391) huku mafuta ya taa yakipungua kutoka Sh2, 829 hadi Sh2, 668 kwa jiji la Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na EWURA, bei hizo zinaanza kutumika leo Jumatano Agosti 2, 2023 katika mikoa mbalimbali nchini.

Kupanda kwa bei hizo kumekuja wakati baadhi ya maeneo nchini yakikabiliwa na upungugu wa mafuta ya petroli na dizeli, hali iliyosababisha msongamano wa watu kwenye vituo vya mafuta.

Katika taarifa hiyo bei ya mafuta ya petroli katika mkoani Tanga imeongezeka kutoka Sh2,724 hadi kufikia 3,245, dizeli kutoka Sh2,760 hadi Sh2,981 wakati mafuta taa yakipungua kutoka Sh2,968 hadi Sh2,740.

Mkoa wa Mtwara petroli imepanda kutoka Sh2,809 hadi Sh3,271, dizeli ikiongezeka kutoka Sh3000 hadi 3008 huku mafuta ya taa yakipungua kutoka Sh2901 hadi Sh2714.

Kwa mujibu wa Ewura imesema mabadiliko ya bei za mafuta yanatokana na changamoto za upatikanaji wa Dola za Marekani, mabadiliko ya sera za kikodi na kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola.

“Mabadiliko ya bei za mafuta kwa Agosti yanatokana na changamoto za upatikanaji wa Dola za Marekani, mabadiliko ya sera za kikodi, kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola hiyo, ongezeko la gharama za mafuta katika soko la dunia na gharama za uagizaji wa mafuta,”imeeleza taarifa hiyo ya Ewura.

Bei hizo za rejareja kwa mkoa wa Arusha zitauzwa (Sh3283), Kibaha (Sh3204), Dodoma (Sh3258), Geita (Sh3364), Iringa (Sh3263), Kagera (Sh3415), Katavi (Sh3357) na Kilimanjaro (Sh3273).

Ramadhani Juma, dereva wa huduma za usafiri wa mtandaoni kwa njia ya Bajaji anasema mafuta yanapopanda ni changamoto kwenye mzunguko wa biashara hiyo huku kilio kikubwa kikionekana zaidi kwa madereva wa usafiri wa abiria kwa njia ya mitandao kwa magari yanayotumia mafuta.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi