Connect with us

Kitaifa

Nyongeza ya mishahara kuanza mwezi ujao

Dodoma. Serikali imetangaza kuwa nyongeza ya mshahara ya kila mwaka itaanza kulipwa mwezi ujao.

Waziri katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Simbachawene aliyasema hayo jana, baada ya kuulizwa na Mwananchi kuhusu nyongeza ya mishahara iliyotakiwa kuanza kulipwa mwaka wa fedha Julai, mwaka huu.

Nyongeza hiyo ilitangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika sherehe za wafanyakazi uwanja wa Jamhuri, mkoani Morogoro, Mei Mosi mwaka huu.

 Ahadi hiyo ilikuja ikiwa ni miaka saba tangu kuondolewa kwa mfumo huo na Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli mwaka 2016.

“Wafanyakazi mambo ni moto… Mambo ni fire,” alisikika Rais Samia wakati akitangaza kurejeshwa nyongeza ya mishahara ya kila mwaka kwa wafanyakazi wa umma.

Samia pia aliwasihi wafanyabiashara kutoongeza bei za bidhaa, huku akiwaahidi wafanyakazi kuwa mambo mazuri yanakuja pasipo kutangaza hadharani nyongeza hiyo.

Jana, Waziri Simbachawe alisema kuchelewa kulipwa kwa nyongeza hiyo kunatokana kuchelewa kwa mchakato wa kubadilisha mifumo ya mishahara.

Alisema kutokana na mishahara kuanza kulipwa kuanzia tarehe 24, walichelewa kufanya hivyo Julai mwaka huu, hivyo wataanza kulipa mwezi ujao.

“Tutaanza kulipa Agosti mwaka huu na tutalipa pamoja na nyongeza ambayo haikulipwa mwezi huu,” alisema Simbachawene.

Kuchelewa kwa nyongeza hiyo, kumezua malalamiko kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi wa umma nchini juu ya utekelezaji wa ahadi hiyo.

Akilizungumzia hilo, Rais wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya alisema wafanyakazi walitarajia ahadi hiyo itaanza kutekelezwa Julai 2023, lakini haikutekelezwa.

Alisema Tucta lilichukua hatua za haraka kuwasiliana na waziri mwenye dhamana, George Simbachawene na kufanya kikao na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Juma Mkomi ili kupata ufafanuzi wa jambo hilo.

Alisema ni kweli Serikali ilitarajia kutekeleza ahadi hiyo Julai mwaka huu, lakini kutokana na sababu za kitaalamu zilisababisha kuchelewa kutekelezwa kwa suala hilo kwa wakati uliokusudiwa.

Alisema hata hivyo, Serikali imewaahidi kukamilisha suala hilo kupitia mishahara itakayotolewa kwa wafanyakazi Agosti 2023.

“Niiombe Serikali kutekeleza suala hili muhimu kama ambavyo imeahidi ili kuendelea kuongeza morali kwa wafanyakazi katika kufanya kazi ya kutoa huduma kwa wananchi,” alisema.

Nyamhokya aliwataka watumishi wa umma kuendelea kuwa na subira na kuendelea kufanya kazi kwa molari na viwango vya juu.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu Tanzania (THTU), Dk Paul Loisulie alisema wamepokea malalamiko kutoka kwa wanachama wao juu ya kutoanza kulipwa kwa nyongeza hiyo.

“Mei Mosi Rais aliahidi nyongeza ya mishahara, sasa ilipofika Julai ambao ndio mwaka wa fedha, wafanyakazi hawakuona wakaanza kulalamika, ndiyo maana tukaenda utumishi kutafuta majibu,” alisema.

Alisema baada ya kupokea malalamiko hayo waliwasiliana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambao waliwathibitishia ahadi hiyo ipo palepale na itaanza kutekelezwa Agosti mwaka huu.

Aliwataka wanachama wa THTU kutulia wakati Serikali inafanyia kazi utekelezaji wa ahadi yake.

Naye Rais wa Chama cha Walimu Nchini (CWT), Leah Ulaya alisema nyongeza haijatolewa kwa watumishi wote na ndiyo maana wanaendelea kuamini kwa kuwa Serikali ni sikivu na iliahidiwa na Rais Samia mwenyewe itatolewa.

“Mimi ni pia ni mwalimu na kimsingi na walimu wenzangu wengi tu wamekuwa wakituuliza sisi viongozi wao kwamba mbona tumeona kimya tulichoahidiwa hatujapata,” alisema.

Leah aliiomba Serikali kutekeleza ahadi hiyo haraka ili kuinua molari ya watu kuendelea kufanya kazi.

“Najua litatekelezwa, ninachosisitiza hilo lifanyike mapema ili lisiwavunje moyo watumishi,”alisema Ulaya.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi