Kitaifa

Maumivu viwango vipya kodi ya majengo yaanza

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza ongezeko la kodi ya majengo itakayotozwa na kupitia ununuzi wa umeme kuanzia Julai, 2023.

Mabadiliko ya kodi hiyo yametokana na mabadiliko ya Sheria ya Serikali za Mitaa ya Utozaji wa Kodi ya Majengo, Sura 289 kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2023 ambayo pia yanapanua wigo wa ukusanyaji wa kodi hiyo, kwa kujumuisha nyumba zilizopo maeneo yote ya wilaya.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TRA jana, nyumba ya kawaida iliyokuwa inatozwa Sh12,000 kwa mwaka, sasa itatozwa Sh18,000 sawa na Sh1,500 kwa mwezi.

Nyumba za ghorofa katika maeneo ya majiji, manispaa za halmashauri za miji zilizokuwa zinatozwa Sh60,000 kwa kila sakafu kwa mwaka, sasa zitatozwa Sh90,000 kwa kila sakafu, sawa na Sh7,500 kwa mwezi.

Tangazo hilo lililotolewa kwa ushirikiano wa TRA na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), pia linaeleza kuwa nyumba za ghorofa katika maeneo ya halmashauri za wilaya zilizokuwa zinatozwa Sh60,000 kwa kila nyumba kwa mwaka, sasa zitatozwa Sh90,000.

“Utekelezaji wa kutoza kodi hii ya majengo kwa kufuata mabadiliko tajwa hapo juu, umeanza Julai, 2023. Viwango hivyo vya utozaji kodi ya majengo vilivyobadilika na vitaendelea kutozwa kupitia ununuzi wa umeme,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Tangazo hilo limekuja ikiwa ni siku chache tangu Serikali ilipopendekeza kufanyika marekebisho hayo kupitia hotuba ya bajeti iliyosomwa bungeni Juni, mwaka huu .

Katika mapendekezo, Bunge liliombwa na kufanya marekebisho ya kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Serikali za Mitaa ya Utozaji wa Kodi ya Majengo, Sura 289 kwa kuongeza maeneo yote ya wilaya, isipokuwa majengo yaliyosamehewa.

Pendekezo lingine ni kutaka kazi ya uthaminishaji wa majengo ianze mwaka wa fedha 2023/24, ili kodi itozwe kwa kuzingatia thamani halisi ya jengo ifikapo mwaka 2026.

Kufanya hivyo kunaipa Tamisemi mamlaka ya kuthaminisha na kukusanya kodi ya majengo kupitia namba ya malipo ya Serikali kuanzia Januari, 2024.

“Katika kipindi cha mpito, utaratibu wa kutumia Luku kukusanya kodi husika utaendelea kutumika. Lengo la hatua hii ni kutoa nafasi kwa Serikali kuanza maandalizi ya uthaminishaji na kuondoa jukumu hilo kwa Tanesco ambayo jukumu lake la msingi ni kuzalisha na kusambaza nishati ya umeme nchini,” alisema Dk Mwigulu Nchemba, waziri wa fedha na mipango akiwasilisha bajeti.

Mabadiliko hayo hayatawaacha wamiliki wa majengo wasiotumia umeme wa Tanesco kwa kuwa nao wametakiwa kufika katika ofisi ya TRA iliyo karibu nao kwa ajili ya kupatiwa ankara ya malipo.

“Wamiliki wote wanaostahili kupata msamaha wa kodi ya majengo, wataendelea kupata msamaha huo kwa kufuata utaratibu uliokuwepo tangu awali. Baadhi ya wanaostahili kupata msamaha huo ni pamoja na wamiliki wa majengo ya ibada (makanisa na misikiti), majengo ya Serikali, wazee wa miaka 60 kwa nyumba moja ya kuishi isiyotumika kibiashara pamoja na wenye ulemavu wasio na shughuli za kujipatia kipato,” imeelezwa.

Serikali ilianza kutekeleza ukusanyaji wa kodi ya majengo kwa kutumia mfumo wa ununuzi wa umeme Julai mosi, 2021 chini ya usimamizi wa TRA kwa kushirikiana na Tanesco ukihusisha mita za aina zote za umeme.

Akizungumzia mabadiliko hayo, Dk Balozi Morwa ambaye ni mshauri wa uchumi alisema mfumo wa kodi wa majengo utaumiza watu wa kipato cha chini kwa sababu ya kutokuwapo mchanganuo mzuri wa ulipaji kodi hizo.

Alisema si sahihi kumlipisha mtu ambaye anatumia nyumba kwa ajili ya makazi fedha sawa na yule ambaye anaitumia kujiingizia kipato.

“Kwa nini wote wawe sawa kwa kulipa Sh15,000 (mfano), nyumba ya makazi isiwe sawa na mimi mwenye nyumba kama hiyo lakini naitumia kujiingizia kipato. Uwepo mchanganuo, hata haya maghorofa tunayozungumzia kuwa yalipe Sh60,000 kwa sakafu, zipo baadhi ya nyumba ambazo ni bora kuliko sakafu ya hizo ghorofa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi