Kitaifa
Utelekezwaji wa miradi mikubwa, ufanisi mdogo Chato
Baada ya mazishi ya Dk Magufuli, Machi 26, 2020, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Wilaya ya Chato, Samuel Bigambo, alimsihi mrithi wa kiti cha urais, Samia Suluhu Hassan kumuenzi mtangulizi wake kwa kuendeleza miradi na mipango yote ya maendeleo ya Chato.
“Tunaomba miradi ya maendeleo, ikiwamo ujenzi wa hospitali ya kanda, uwanja wa ndege wa Chato na mengine katika sekta za elimu, afya na barabara iendelezwe kama njia ya kumuenzi hayati Rais Magufuli,” alisema Bigambo.
Ukiachana na uwanja wa ndege wa Chato ambao ni miongoni mwa alama alizoziacha Magufuli, katika eneo hilo alilozaliwa kulikuwa kuna miradi mingine mikubwa iliyoanzishwa kuanzia mwaka 2016, ukiwamo ujenzi wa stendi ya mabasi ya kisasa wilayani Chato, Hospitali ya Rufaa na chuo cha ufundi.
Pia, katika kipindi hicho ilianzishwa mbuga ya wanyama ya Burigi-Chato, ujenzi wa hoteli ya kitalii ya nyota tatu, Chuo Kikuu cha Chato na taasisi nyingine, hasa za Serikali zilizoanzisha ofisi huko kwa kujenga majengo ya kisasa.
Miongoni mwa mawaziri wa Serikali iliyoongozwa na Rais Magufuli ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini aliiambia Mwananchi kuwa: “Magufuli alikuwa anakusudia kuikuza Chato kimkakati kwa kuweka taasisi na miundombinu muhimu ili ikue ichangamke na kuifanya kuwa mkoa, ndilo lingekamilika hilo.”
Stendi ya mabasi
Ukifika eneo inapojengwa stendi mpya ya kisasa yenye uwezo wa kuhudumia mabasi 130, huoni ile kasi ya ujenzi kama ilivyokuwa awali, baadhi ya maeneo yameota nyasi na kwa kuona tu unaweza kusema mkandarasi hajafika eneo la mradi muda mrefu.
Katika eneo hilo inakojengwa stendi ya Chato yenye ukubwa wa mita za mraba 30,000 mkabala imejengwa stendi ya mabasi madogo yenye ukubwa wa mita za mraba 7,500 ambayo hivi sasa ndiyo inayohudumia mabasi madogo na makubwa.
Licha ya stendi hiyo kutoa huduma iliyopaswa kutolewa na stendi mbili, hakuna msongamano, hivyo unaweza kuhisi eneo hilo ni kubwa kuliko mahitaji yake Chato.
Mzunguko wa watu katika stendi hiyo muda wa mabasi kuwasili kwa makadirio hawazidi 200.
Katika kitabu cha ‘I am the state’ (2023) kulichoandikwa na wahariri wanne wa habari wa Tanzania (Ansbert Ngurumo, Absalom Kibanda, Jesse Kwayu na Neville Meena) kinaelezea stendi hiyo kuwa ina uwezo wa kuegesha mabasi madogo 108 kwa wakati mmoja, lakini wastani wa mabasi yanayoegeshwa hapo ni 20.
“Mpaka kufikia Novemba, 2022 kati ya maduka 50 yaliyopo katika stendi hiyo ndogo, yaliyopata wapangaji ni 19,” kinaeleza kitabu hicho kinachozungumzia maisha ya Rais Magufuli na namna alivyofanya upendeleo wa kuendeleza mji aliozaliwa.
Mradi mwingine uliotelekezwa ni ujenzi wa hoteli ya kitalii ya nyota tatu eneo la Rubambangwe-Chato ambayo hivi sasa imebakia kichakani kukiwa hakuna uendelezaji unaofanyika.
Jiwe la msingi la hoteli hiyo iliyokuwa imepagwa kutumia Sh12.9 bilioni liliwekwa Julai 10, 2019 na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na utalii wa wakati huo, Dk Hamis Kigwangalla.
Mbuga ya wanyama
Kitabu hicho pia kinaeleza hali ilivyo katika Mbuga ya Burigi ambayo wanyama wake walikusanywa kutoka mbuga nyingine.
Baadhi ya picha za kitabu hicho zinaonyesha mafuvu ya wanyama wanaokufa katika mbuga hiyo kwa sababu mbalimbali, ikiwamo kupigana wenyewe.
Watafiti waliohusika kuandaa kitabu hicho ndiyo watalii pekee waliotumia Geti la Nyungwe katika mwezi wa Novemba, 2022 na pindi walipotaka kutumia Geti la Mganza kutoka mbugani waliambiwa limefungwa kutokana na uchache wa watalii.
Hospitali ya rufaa
Mbali na mbuga, mradi wa Hospitali ya Rufaa ya Chato nao ni miongoni mwa miradi mikubwa iliyoanzishwa katika wilaya hiyo wakati wa utawala wa Rais Magufuli (Novemba 5, 2015 hadi Machi 17, 2020), licha ya kuwa haijakamilika kwa asilimia 100, lakini tayari inatoa huduma.
“Hapa huduma zinatolewa kama kawaida, ni vile tu bado haijakamilika kama ilivyokusuduiwa, bado kufungwa kwa mashine za CT Scan, MRI na X-Ray kama alivyoahidi Rais (Samia Suluhu) alipotembelea hapa,” alisema daktari mmoja aliyekuwa akila chakula cha mchana kwa mama ntilie mkabala na hospitali hiyo.
Hata hivyo, hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya ya mwaka 2022/23 ilieleza kuwa tangu hospitali hiyo ianze kutoa huduma Julai, 2021 hadi Machi 2022 ilikuwa imehudumia wagonjwa 5,607.
Kati ya hao wagonjwa wa nje (OPD) walikuwa 4,810 na wa ndani (IPD) walikuwa 797.
Pia, maeneo yaliyokuwa yametengwa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Chato na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Tawi la Geita yamebakia mapori yenye vifusi vya mchanga na changarawe yaliyozungushiwa uzio kwa nje, kuna vibao vinavyoelezea mradi vilivyopauka.
Kuhusu ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Chato na tija yake hivi sasa, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe anasema ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Chato na mengine yaliyofanyika wakati wa uongozi wa Rais Magufuli yanaacha funzo kwa viongozi wengine juu ya upendeleo.
“Kwetu wanasiasa jambo kubwa tunalojifunza ni kuwa tusitumie mamlaka na madaraka yetu kupendelea tunapotoka maana gharama kwa nchi zinakuwa kubwa sana,” anasema kiongozi huyo akihusisha kauli yake na madai ya Rais wa Awamu ya Tano, hayati John Magufuli kuipendelea Chato.