Connect with us

Kitaifa

Hizi hapa hoja nne za Serikali kupinga kesi ya bandari isisikilizwe

Mbeya. Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya leo Jumanne, Julai 25, 2023 imeanza kusikiliza kesi ya kupinga mkataba wa makubaliano ya uboreshaji na usimamizi wa bandari baina ya Serikali ya Tanzania na Dubai (IGA), pamoja na pingamizi la Serikali dhidi ya kesi hiyo.

Kesi hiyo ya kikatiba namba 5 ya mwaka 2023, imefunguliwa na wanasheria vijana wanne kutoka mikoa tofauti, wakipinga makubaliano hayo kwa madai kuwa ni batili kwa kuwa yana ibara zenye masharti yanayokiuka sheria za nchi na Katiba.

Hata hivyo, Serikali imewasilisha pingamizi la awali ikitaka Mahakama hiyo isiisikilize kesi hiyo, huku ikibainisha hoja nne za kutaka Mahakama hiyo iitupilie mbali kesi hiyo bila kuwasikiliza wadai hao.

Miongoni mwa sababu hizo, Serikali inadai mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa mujibu wa Ibara ya 7 (2) ya Katiba ya Nchi.

Ibara hiyo inasomeka: “Masharti ya sehemu hii (sehemu ya Pili) ya Sura hii (Sura ya Kwanza) hayatatiliwa nguvu ya kisheria na mahakama yoyote.”

Mahakama yoyote nchini haitakuwa na uwezo wa kuamua juu ya suala kama kutenda au kukosa kutenda kwa mtu au mahakama yoyote, au kama sheria au hukumu yoyote inaambatana na masharti ya sehemu hii ya sura hii.

Katika hoja ya pili, Serikali inadai shauri hilo kwa kufunguliwa chini ya ibara ya 108 (2) na chini ya kifungu cha 2 (3) cha Sheria ya Usimamiaji Haki na Matumizi ya Sheria (JALA), halina nguvu ya kuhoji ukiukwaji (sheria/Katika) kwa mambo yanayoangukia katika ibara ya 12 mpaka 29 za Katiba ya nchi (kuhusu wajibu na haki za msingi).

Badala yake Serikali inadai utaratibu sahihi wadai walipaswa kutumia Sheria ya Utekelezaji Wajibu na Haki za Msingi (BRADEA).

Hoja ya tatu, Serikali inadai kuwa shauri hilo limefunguliwa wakati usio muafaka, ni batili na halina nguvu kwa kuwa wadai bado walikuwa na njia mbadala ya kupata haki wanazoziomba chini ya sheria za ununuzi.

Na hoja ya nne, Serikali inadai kwamba kiapo kinachounga mkono shauri la msingi kina kasoro zisizorekebishika kwa kuwa hoja za kisheria (badala ya hoja za kiushahidi), maoni binafsi na hitimisho (kuhusu madai yao kwenye kesi), jambo ambalo inasema ni kinyume cha maelekezo ya kisheria.

Hivyo wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo Serikali (wadaiwa) kupitia jopo la mawakili wa Serikali watatoa ufafanuzi wa kina wa hoja hizo moja baada ya nyingine.

Kisha mawakili wa wadai nao kujibu hoja hizo moja ya nyingine Kwa kuzingatia maelezo ya ufafanuzi wa Serikali, kama wanakubaliana nayo au la na kutoa sababu za kutokubaliana nazo.

Wanasheria hao vijana wanapinga makubaliano hayo yanayohusu uwekezaji katika bandari katika bahari na katika maziwa kuwa ni batili kwa kuwa masharti ya baadhi ya Ibara zake yanakiuka Sheria za Nchi za Ulinzi wa Raslimali na Maliasili za Nchi na Katiba ya Nchi.

Vile vile wanadai kwamba yanahatarisha mamlaka ya Nchi na usalama wa Taifa na kwamba yaliridhiwa na Bunge kinyume cha utaratibu bila kuwapa nafasi ya kutosha wananchi kutoa maoni yao.

Wadai hao (waliofungua kesi hiyo ni Alphonce Lusako, Emmanuel Chengula, Raphael Ngonde na Frank Nyalus, ambao wanawakilishwa na mawakili Boniface Mwabukusi (Kiongozi wa jopo) Philipo Mwakilima na Levino Nagalimitumba.

Wadaiwa katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambaye ni mshahri wa Serikali kwa mauslanya kisheria, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Katibu wa Bunge la Tanzania, ambaye ni mtendaji mkuu na mratibu wa shughuli za Bunge.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ndiye aliyesaini makubaliano hayo Oktoba 25, 2023 Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, baada ya kupewa nguvu ya kisheria na Rais Samia Suluhu Hassan, huku Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, akishuhudia.

Hivyo wadai wanadai kuwa kitendo cha Waziri na Katibu Mkuu kusaini na kisha kuyawasilisha makubaliano hayo bungeni kwa ajili ya kupitishwa bila kushirikisha umma na kutoa nafasi ya kutosha kwa wananchi kutoa maoni yao, walikiuka matakwa ya Sheria za Nchi.

Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watu lianoloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji Mustafa Ismail na Abd Kagomba.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi