Dar es Salaam. Wakati matumizi ya simu yakirahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha nchini, takribani nusu ya watu wazima walio na umri zaidi ya miaka 16 mkoani Singida hawajaunganishwa na huduma yoyote ya kifedha.
Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Singida ina watu milioni 2.008, huku asilimia 48.5 ni watu wenye umri wa miaka 15 hadi 64 na asilimia 6.5 ikiwa ni wazee wa umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea.
Utafiti wa Finscope Tanzania wa mwaka 2023 uliotolewa mapema mwezi huu, unaeleza asilimia 41 ya watu wazima mkoani humo ndio ambao hawajafikiwa na huduma yoyote ya kifedha, ikiwa ni rasmi au isiyokuwa rasmi.
Hilo linabainika kipindi ambacho ujumuishwaji wa huduma za kifedha kitaifa umetajwa kukua kwa kasi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kutoka asilimia 65 mwaka 2017 hadi asilimia 76 mwaka huu.
Kuimarika kwa utendaji huo kumechangiwa na huduma za fedha kwa njia ya simu, kwa asilimia 72, ikifuatiwa na huduma za benki za biashara kwa asilimia 22.
Ongezeko la jumla la upatikanaji wa huduma za kifedha linatajwa kufufua matumaini ya kupata ushirikishwaji wa asilimia 100 katika siku za usoni, lakini hofu baadhi ya mikoa inaweza kuachwa nyuma ikiwa hali ya sasa itaendelea.
Mbali na Singida, utafiti wa FinScope umeorodhesha mikoa mitano ya chini ambayo imeachwa nyuma katika ujumuishwaji wa huduma hizi za kifedha ambayo ni Kigoma (38), Simiyu (33), Kagera (30) na Rukwa (27). Ili kuhakikisha upatikanaji bora wa huduma za kifedha kwa wakazi katika maeneo haya, itahitajika juhudi mpya za watunga sera.
Hata hivyo, utafiti wa FinScope haukutoa sababu za uwepo wa hali hiyo katika mikoa husika.
Utafiti ulitaja baadhi ya viashiria ambavyo vingeweza kuwa sababu za ukuaji mdogo wa huduma za kifedha katika maeneo hayo, ikiwamo umaskini uliokithiri, elimu duni na ukosefu wa ajira rasmi.
“Watu wazima wengi wa Kitanzania ambao hawatumii huduma rasmi za kifedha wanadai kuwa hawana mapato ya kutosha kutumia huduma hizi. Hii inaonyesha mtazamo wa jumla kwamba huduma rasmi za kifedha zinahitaji mapato makubwa,” utafiti wa FinScope unasema.
Licha ya kwamba mikoa hiyo ina maeneo mengi ya kilimo, kimsingi ni maeneo ya vijijini na pembezoni yenye uanzishwaji mdogo wa biashara binafsi ambazo zingeweza kutoa ajira rasmi kwa watu wengi.
Mikoa minne kati ya hiyo (Singida, Kigoma, Simiyu na Rukwa) pia ni miongoni mwa mikoa 10 yenye watumiaji wachache wa huduma za mawasiliano hadi Juni 2023 kwa mujibu wa Takwimu za Mawasiliano za robo ya Nne ya mwaka wa fedha 2022/23 iliyochapishwa wiki hii na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Usajili duni laini za simu unaweza kuonyesha kwa kiasi fulani matumizi duni ya huduma za kifedha.
“Kwa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi, changamoto kubwa inaweza kuwa ni watu kukosa huduma ya mtandao au haupo kwa kiwango kinachotakiwa.
“Ingawa kuna uhusiano mzuri kati ya umiliki wa simu na matumizi ya huduma za kifedha kupitia simu za mkononi, lakini karibu robo ya watu ambao hawana simu bado wanatumia huduma hizo.”
Hii ikiwa na maana kuwa, baadhi ya watu wasiokuwa na simu wamekuwa wakipata huduma za kifedha kupitia mawakala, ndugu au marafiki.
Wataalamu wanashauri, utafiti wa FinScope 2023 ungetumika kushughulikia vikwazo vya ujumuishwaji mdogo, hasa katika mikoa iliyo nyuma.
“Mfumo wa kwanza uliweka kipaumbele katika mwelekeo wa ufikiaji, wakati wa pili uliweka kipaumbele matumizi ya huduma za kifedha. Uundaji wa Mfumo wa tatu utakuwa wa mashauriano,” alisema Mmari.