Kitaifa
Kesi za mikataba kimataifa zashtua wadau, watoa njia
Dar es Salaam. Siku mbili baada ya Serikali kutoa msimamo wa kukata rufaa dhidi ya hukumu ya kulipa fidia ya Dola 109 milioni za Marekani (Sh260 bilioni) katika uwekezaji wa Mradi wa Nikeli wa Ntaka Hill, wadau wameshauri kuendesha majadiliano na wawekezaji walioathiriwa na mageuzi ya kisheria nchini.
Wadau hao wameshauri Serikali kuendesha majadiliano nao ili kutafuta maridhiano na wawekezaji wenye uhalali wa kunufaika na fidia inayotokana na dosari za mageuzi ya sheria za utajiri wa rasilimali za mwaka 2017, zilizoanza kuathiri Taifa kutokana na madai yaliyopo au ushindi wa kesi zilizoamuliwa.
Kuhusu mikataba kwa jumla, wameshauri Serikali kufanya mapitio upya ya mikataba hiyo inayoathiri uhuru wa mageuzi ya kisera katika mataifa mbalimbali pamoja na kuandaa nyaraka itakayokuwa msingi wa makubaliano ya nchi na nchi au ukanda wowote ule utakaolazimu Tanzania kushiriki.
Julai 14, mwaka huu Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya uwekezaji (ICSID) iliamuru Serikali kuilipa fidia Kampuni ya Indiana Resources na wanahisa wenza Dola 109 milioni za Marekani (Sh260 bilioni) baada ya kujiridhisha ukiukwaji wa mkataba katika Mradi wa Nikeli wa Ntaka Hill mwaka 2018.
Hukumu hiyo inaielekeza Serikali kulipa fidia ya Dola 76.7 milioni za Marekani, sanjari na riba ya asilimia mbili iliyoanzia Januari 10, 2018 baada ya kuvunja mkataba huo, hivyo kufanya jumla ya fidia kuwa Dola 109.5 milioni za Marekani (Sh260 bilioni). Pia inahusisha gharama ya uendeshaji wa kesi hadi Julai 14, mwaka huu.
Hata hivyo kwa mujibu wa ICSID, Serikali bado inakabiliwa na kesi 11 za madai ya fidia zilizosajiliwa katika Mahakama hiyo, ikiwamo iliyofunguliwa Julai 27, 2020 na Kampuni ya Winshear Gold Corporation pamoja na Montero Mining & Exploration Limited iliyofunguliwa Oktoba 5, mwaka 2020.
Kabla ya uamuzi huo, tayari Serikali imeshakiri kuanza kulipa fidia ya Dola 165 milioni (Sh380 bilioni) kwa Kampuni ya Eco Energy Group iliyoshinda kesi pia dhidi ya uamuzi wa kupokonya hatimiliki ya hekta 20,400 za mradi wa sukari Bagamoyo, ikiwa ni ukiukwaji wa mkataba wa uwekezaji.
Maoni ya wadau
Leo ni siku ya 10 tangu kurejea kwa ndege ya Serikali aina ya Airbus A220 iliyokuwa inashikiliwa Uholanzi tangu Januari mwaka jana na kampuni hiyo kwa madai ya kuchelewa kulipa fidia, ikiwa ni mwendelezo wa matukio ya ndege za Tanzania kushikiliwa kwa shinikizo la kulipa fidia haraka.
Wakitoa maoni yao, Mwanasheria wa Chama cha Wanasheria Watetezi wa Mazingira Tanzania (Leat), Clay Mwaifani alishauri Serikali kuanzisha mchakato wa maridhiano na waathirika wote wa leseni hodhi ikiwa ni utekelezaji wa 4R za Rais Samia Suluhu Hassan ili kuepuka kulipa fidia kubwa zaidi ya hiyo.
“Walitumia fedha kwa utafiti na leseni ziliwaruhusu, hivyo na Serikali ilisema itafidia gharama zilizokuwa zimeingiwa na wawekezaji na huo ndio msingi wa madai yao. Tuombe waondoe shauri lao (Indiana Resources), na wengine wote waitwe na tuzungumze nao kabla nao hawajaamua kutushtaki,” alisema Mwaifani.
Rais Samia alionyesha dhamira ya mageuzi katika Taifa kupitia mtazamo wa 4R, ambazo ni maridhiano (Reconciliation), mabadiliko (Reforms), ustahimilivu (Resilience) na kujenga upya (Rebuilding).
Hoja hiyo iliungwa mkono na Katibu Mtendaji wa Chemba ya Madini na Nishati Tanzania (TCME), Benjamini Mchwampaka aliyeshauri Serikali kuongeza umakini wakati wa mabadiliko inayofanya katika sheria zake, akiamini katika majadiliano.
“Serikali inapotaka kufanya mabadiliko ya kisheria inatakiwa kuendesha majadiliano na wadau ili kuepuka athari za namna hiyo, ninaamini kama kungekuwa na majadiliano tusingefikia kwenye athari hizi, mashauriano yangetengeneza win to win situation (manufaa pande zote),” alisema Mchwampaka.
Alishauri hilo ikiwa ni miezi minne imepita tangu chemba hiyo kushauri mbele ya tume ya maboresho ya mfumo wa haki jinai kufanya marekebisho katika sheria tatu za utajiri wa rasilimali za mwaka 2017 kupitia mageuzi ya Serikali ya awamu ya tano kwa lengo la kurejesha ustawi wa sekta hiyo.
Sheria hizo ni ile ya mamlaka ya nchi kuhusu umiliki wa maliasili ya mwaka 2017 pamoja na sheria ya mapitio na majadiliano kuhusu masharti hasi katika mikataba inayohusu maliasili za nchi ya mwaka 2017 na sheria ya madini sura 123; sheria ya madini ya mwaka 2010, iliyorekebishwa 2017, 2018 na 2019.