Kitaifa

Uamuzi mchungu kwa Taifa

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeamuriwa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) kulipa fidia ya dola 109 milioni (Sh260 bilioni) kwa wawekezaji wa Mradi wa Nikeli wa Ntaka Hill, uamuzi unaoelekea kuwa mchungu kwa Taifa.

Kufuatia hukumu hiyo iliyotokana na hatua zilizochukuliwa na Serikali ya awamu ya tano, Serikali ya Tanzania imesema hatua za kupinga uamuzi na mawasiliano mengine zinaendelea.

Hata hivyo, kwa mujibu wa hukumu hiyo, kiasi hicho cha fidia kitakuwa kinaongezeka kwa asilimia mbili kila siku hadi pale malipo yatakapofanyika.

Hukumu hiyo inatokana na kesi ya madai namba ARB/20/38 iliyowasilishwa na kampuni ya Indiana Resources, dhidi ya Serikali ya Tanzania iliyodumu mahakamani kwa siku 1,012.

“Hatua za kupinga uamuzi na mawasiliano mengine zinaendelea,” alijibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Eliezer Feleshi kwa maandishi alipoulizwa na gazeti hili kuhusu msimamo wa Serikali.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa Julai 14, mwaka huu, Serikali imetakiwa kulipa fidia ya dola 76.7 milioni, sanjari na riba ya asilimia mbili iliyokokotolewa kuanzia Januari 10, 2018 baada ya kuvunjwa kwa mkataba na leseni ya wadai kutwaliwa na Serikali, hivyo kufanya jumla ya fidia kuwa dola 109.5 milioni (Sh260 bilioni).

“Kiasi cha tuzo hii kinaonyesha uwekezaji mkubwa ambao umepotezwa na wanahisa baada ya Serikali ya Tanzania kutwaa leseni ya Ntaka Hill kinyume cha sheria,” alisema Mwenyekiti Mtendaji wa Indiana Resources, Bronwyn Barnes katika taarifa yake kwa umma baada ya hukumu hiyo kutolewa.

Wachambuzi wa masuala ya sheria za kimataifa wanasema hukumu hiyo inaleta hatari ya kukamatwa kwa mali mbalimbali za nchi, zikiwemo ndege za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kama ambavyo imekwishafanyika zaidi ya mara moja, kutokana na urahisi wa hatua hiyo.

Hukumu hiyo imetolewa siku chache baada ya Serikali kuanza kulipa fidia ya dola 165 milioni (Sh380 bilioni) kwa kampuni nyingine iliyoshinda kesi pia kufuatia uamuzi wa kupokonya hatimiliki ya hekta 20,400 za mradi wa sukari huko Bagamoyo mkoani Pwani, kinyume na mkataba wa uwekezaji.

Ili kushinikiza kampuni hiyo kulipwa fedha zake, ilishikilia ndege ya ATCL, Airbus A220-300, kwa takribani mwaka mmoja nchini Uholanzi hadi ilipoachiwa na kurejea nchini Julai 7, mwaka huu.

“Leo niko hapa kuwapa habari njema, siku chache zilizopita niliwajulisha kuna ndege yetu tulikuwa na kesi nchini Uholanzi ikakamatwa, ilikuwa chini ya mikono ya sheria. Bahati nzuri tumefanya mazungumzo na jambo limekwenda vizuri ndege yetu imerudi jana jioni iko Tanzania,” alisema Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa siku moja baada ya ndege hiyo kuachiwa.

Kabla ya hapo, Septemba 2019 ndege nyingine ya ATCL aina ya Bombardier Q400-8 ilikamatwa nchini Canada, kwa shinikizo la mkulima Hermanus Steyn, ambaye anadai fidia baada ya Serikali ya Tanzania kutaifisha mali zake mwaka 1980.

Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Steyn kushikilia ndege za Tanzania, baada ya kufanya hivyo kwa kuzuia ndege ya Tanzania aina ya Airbus A220-300 kuondoka nchini Afrika Kusini Agosti, 2019.

Serikali ya Tanzania kupitia kwa wanasheria wake ilifanikiwa kushinda hoja mahakamani na kufanikiwa kuikomboa ndege hiyo iliyokuwa ikishikiliwa katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo Septemba 3, 2019.

Msingi wa kesi

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, Kampuni ya Indiana ilikuwa inalalamikia kunyang’anywa leseni ya kuhodhi eneo hilo la mradi wa madini.

Mgogoro huo ulichagizwa na marekebisho ya Sheria ya Madini ya 2017 ambayo pamoja na mambo mengine, ilifuta misingi ya kisheria ya umiliki wa leseni ya kuhodhi eneo la madini yaliyofanyika mwaka 2018.

Januari 10, 2018, Serikali ilichapisha Kanuni za Madini (Haki za Madini) za 2018. Chini ya Kanuni ya 21 ya kanuni hizo, Serikali ilifuta leseni zote za kuhodhi ardhi, zilizotolewa kabla ya Januari 10, mwaka 2018.

Leseni hizo zilikoma kuwa na athari yoyote ya kisheria. Haki za maeneo yote yaliyokuwa chini ya leseni hizo ikiwa ni pamoja na leseni iliyokuwa kwa Indiana Resources, zilihamishiwa kwa Serikali.

Kwa mujibu wa Indiana, inayomiliki asilimia 62.4 ya hisa za kampuni hizo mbili; Ntaka Nickel Holdings Ltd na Nachingwea UK Limited zilizokuwa zinamiliki leseni hiyo, zilijaribu kuishawishi Serikali kurejesha leseni hiyo lakini haikufanikiwa hadi mwanzoni mwa mwaka 2020 ilipofungua maombi ya fidia katika Mahakama ya ICSID.

Kampuni hizo zilifungua kesi hiyo ya ukiukwaji wa makubaliano ya Mkataba wa Uwekezaji wa Tanzania (BITs) kati ya Tanzania na Uingereza kuhusu uwekezaji wa kampuni hizo mbili za nchi hiyo.

Mchambuzi huru wa mikataba ya kimataifa ya biashara na uwekezaji, Roselian Jackson alisema kwa kuwa Tanzania ni mwanachama wa ICSID, uamuzi huo unatoa nafasi kwa Indiana kuhitaji malipo yake.

“Kama Serikali ikishindwa kulipa ndiyo utasikia kampuni imepewa kibali cha kushikilia mali za Serikali kama vile ndege ili kushinikiza malipo,” alisema. Alishauri Serikali kuanza kufanya mapitio ya mikataba ya uwekezaji yote nchini ili kuakisi mabadiliko katika mahitaji ya uwekezaji wa kidunia.

“Hizo BiTs (mikataba ya uwekezaji wa nchi na nchi) zimepitwa na wakati, zinaibana nchi kufanya mageuzi yoyote yale ya kisera, mataifa mengi yameshaanza kuboresha mikataba ya aina hiyo.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi