Kitaifa
Serikali yaweka kigingi kesi ya mkataba wa bandari
Mbeya. Serikali imewasilisha pingamizi la awali dhidi ya kesi ya kupinga makubaliano ya ushirikiano wa kijamii na kiuchumi baina ya Serikali ya Tanzania na ya Dubai, yanayohusisha uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam, ikiiomba Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya isisikilize.
Kesi hiyo ya kikatiba namba 5 ya mwaka 2023 imefunguliwa na wanasheria wanne Alphonce Lusako, Emmanuel Kalikenya Changula, Raphael Japhet Ngonde na Frank John Nyalusi, wakipinga makubaliano hayo, wakidai kuwa baadhi ya ibara zina masharti mabovu ambayo hayana maslahi kwa taifa.
Wadaiwa katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Katibu wa Bunge la Tanzania.
Sambamba na kesi hiyo ya msingi, pia wanasheria hao wamefungua maombi madogo ya zuio, wakiomba Mahakama hiyo itoe amri ya zuio dhidi ya wadaiwa kuwazuia kuendelea na hatua zozote za utekelezaji wa makubaliano hayo mpaka kesi ya msingi itakapoamuriwa.
Kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa leo Alhamis Julai 20, 2023 na jopo la majaji watatu linoloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji Mustafa Ismail na Abdi Kagomba.
Hata hivyo Serikali katika majibu yake ya maandishi iliyoawasilisha mahakamani hapo yakiungwa na kiapo kinzani kujibu madai ya wadai hao, kabla ya kusikilizwa pande zote kwa mdomo, imeibua pingamizi la awali ikiiomba mahakama hiyo iitupilie mbali kesi hiyo kabla ya kuisikiliza.
Katika pingamizi hilo la awali, Serikali imeibua hoja nne za kisheria inazolenga kuishawishi mahakama hiyo kuwa haipaswi kuisikiliza kesi hiyo na badala yake iitupilie mbali.
Kutokana na kuwepo kwa pingamizi hilo la awali, kiutaratibu mahakama inapaswa kuanza kulisikiliza kwanza pingamizi hilo na kulitolea uamuzi
Hata hivyo Lusako, mmoja wa wadai, amelieleza Mwananchi Digital kuwa licha ya kuwepo kwa pingamizi hilo, wataomba kwanza maombi yao ya zuio la muda yasikilizwe kabla ya kusikiliza pingamizi akidai kuwa tayari hatua za utekelezaji wa makubaliano hayo zimeshaanza.
“Makubaliano hayo yanawaruhusu kufanya amendment (marekebisho) ya sheria za ndani. Na tayari wameshaanza kufanya hivyo. Kwa hiyo tunataka kuiomba mahakama kwanza tusikilizwe maombi yetu ya zuio,” amesema Lusako.
Amesema kuwa kama watasubiri kusikiliza kwanza pingamizi kama taratibu zinavyoelekeza wakati utekelezaji wa makubaliano hayo, basi kesi hiyo haitakuwa na maana.
Makubaliano hayo baina ya Serikali ya Tanzania yalisainiwa Oktoba 25, 2022.
Kwa niaba ya Serikali ya Tanzania yalisainiwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, kwa mamlaka aliyopewa na Rais Samia Suluhu Hassan yakishuhudiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.
Juni 10, 2023, Bunge la Tanzania lilipitisha azimio la kuridhia makubaliano hayo.
Hata hivyo makubaliano hayo yaliibua mjadala mkali unaoendelea mpaka sasa katika mitandao ya kijamii na hata viijiweni, huku wengine wakiyapinga na wengine wakiyaunga mkono
Katikati ya mjadala huo ndipo jopo Mwanasheria Lusako na wenzake walipoamua kufungua kesi Mahakama Kuu Kanda Mbeya, chini ya hati ya dharura kupinga uhalali wa mkataba huo.
Kwa mujibu wa hati ya wadai hao, wanadai kuwa makubaliano hayo ni batili kwa kuwa yanakiuka sheria za nchi za ulinzi wa raslimali na maliasili za nchi na kwamba yaliridhiwa na Bunge kinyume cha utaratibu bila kuwapa nafasi ya kutosha wananchi kutoa maoni yao.
Hivi sasa watu wanaofuatilia kesi hiyo wameshafurika mahakamani wakisubiri kuanza kusikiliza baada ya taratibu kukamilika.
Mawakili wa pande zote wako katika kikao na jopo la majaji wanaoisikiliza kesi hiyo Kwa majadiliano mafupi namna ya kuziendesha kesi hiyo.