Kimataifa
Starlink ya Elon Musk yazinduliwa Kenya
Dar es Salaam. Bilionea, Elon Musk ametangaza katika ukurasa wake wa Twitter kuwa Kampuni yake ya Starlink, imezindua huduma ya internet yenye kasi, inayotumia satellaiti nchini Kenya, na kwamba kwa uzinduzi huo, mteja ataweza kupata huduma za kampuni hiyo bila kujali mipaka ya nchi hiyo.
Kabla ya uzinduzi huo nchini Kenya, wakati Fulani Tanzania ilipokea maombi ya kampuni hiyo kuja kuwekeza nchini, huku wadau wakisema itachochea uchumi wa kidijitali na itakuwa nafuu na yenye kasi.
Taarifa hizo zinasema, huenda hadi kufika Machi 2023 teknolojia hiyo inayomilikiwa na Kampuni ya SpaceX itakuwa imeingia nchini.
Kwenye tovuti yao rasmi, Starlink ilitangaza mpango wao wa kuleta huduma hizo nchini kati ya Januari na Machi 2023, kama wangeruhusiwa na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA).
Hata hivyo, akizungumza na katika mahojiano maalum na Mwananchi Digital Februari mwaka huu, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye; alisema Tanzania ipo tayari kuipokea internet ya Elon Musk ‘Starlink’, na kwamba wanasubiri wawasilishe nyaraka tu.