Kitaifa

Mpira wa haki jinai sasa kwa Samia

Moshi/Dar. Yatatekelezwa? Hili ndiyo swali linalogonga vichwa vya wadau wa Haki Jinai nchini baada ya Tume iliyoundwa kuangalia namna ya kuziboresha haki hizo kuwasilisha ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Tume hiyo iliyoongozwa na Jaji mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman ilikabidhi ripoti hiyo juzi, Ikulu jijini Dodoma ikibeba mapendekezo lukuki, ikiwamo haja ya kuboresha utendaji kazi wa Jeshi la Polisi nchini.

Kufuatia mapendekezo hayo, wadau wa haki jinai waliozingumza na Mwananchi wamesema yote yaliyopendekezwa na Tume yanawezekana ikiwa Rais Samia na watendaji wake katika ngazi mbalimbali wataamua ifanyike hivyo.

Miongoni mwa mengi, Tume imependekeza kuanzishwa Mamlaka mpya na Huru ya upelelezi inayojitegemea, itakayojulikana kama Ofisi ya Taifa ya Upelelezi ambayo itakuwa na jukumu la kupeleleza makosa makubwa kama ya ugaidi na mauaji.

Imegusia pia suala la makubaliano ya Kukiri Makosa (Plea Bargaining), utaratibu uliolalamikiwa sana na baadhi ya waliokiri makosa na kutozwa mamilioni ya shilingi, ikipendekeza kuwa malalamiko ya kulazimishwa kukiri makosa, yashughulikiwe kwa njia ya mahakama.

Katika suala hilo, Tume hiyo imependekeza iundwe timu maalumu ya kuchunguza utata katika baadhi ya mali zilizotaifishwa katika utaratibu wa vikosi kazi na mashauri ya kukiri kosa ili kuishauri Serikali ipasavyo namna ya kuyashughulikia.

Mbali na suala hilo, Tume imependekeza kufanyiwa marekebisho kwa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ili kuruhusu makosa yote kuwa na dhamana, isipokuwa makosa makubwa, na kupendekezwa itungwe sheria ya dhamana.

Kama ilivyokuwa kwa Jeshi la Polisi ambalo Tume imependekeza libadilishwe jina na kuwa Huduma za Polisi na kufanyiwa tahmini, pia imependekeza jina la Jeshi la Magereza nalo lifanyiwe marekebisho ya kisheria, kifikra na kimuundo ili liwe ni la kutoa huduma ya urekebishaji wa mienendo.

Pia, tume hiyo imependekeza utaratibu wa kuanzisha taasisi zenye taswira ya kijeshi usitishwe na taasisi ambazo zinatekeleza majukumu ya Haki Jinai au zinazotoa huduma kwa wananchi zenye taswira ya kijeshi zibadilishwe.

Imetaka taasisi hizo — Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Uhamiaji na Jeshi Usu la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu — zirejee katika majukumu yake ya awali ya utoaji wa huduma kwa wananchi.

Katika hilo, Tume imesema Wizara ya Maliasili na Utalii iwarejeshe watumishi wote raia katika vyeo vyao vya ajira ya awali na kuwaondolea mavazi na vyeo vya kijeshi, isipokuwa mavazi hayo yavaliwe na watumishi walioko kwenye idara inayohusika na majukumu ya kupambana na ujangili.

Yote yanawezekana

Baada ya ripoti hiyo kuwasilishwa, gazeti hili limezunguza na wadau kupata mitazamo yao akiwemo, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji mstaafu Amir Manento aliyesema tume imetoa ripoti nzuri na mapendekezo yanapaswa kutekelezwa ili fedha zilizotumika kuiandaa zisiwe zimetumika vibaya.

“Rais akisimamia kila kitu kinaweza kwenda vizuri. Tuyafanyie kazi hayo mapendekezo ili tusiingie hasara kama nchi, twende kuitekeleza ili fedha zetu zisiende bure,” alisema Jaji Manento.

“Kila kitu kinawezekana ikiwa Rais na watu wake wataamua. Yeye ndiye kiongozi mkuu. Hao Ma-RC, Ma-DC wako chini yake, ni yeye wa kuwaeleza tu wasifanye hivi. Wazingatie sheria na yeye anaweza kuwaeleza wasifanye yanayozuiwa kisheria na wanaofanya anawachukulia hatua,” alisisitiza mwenyekiti huyo mstaafu.

Kuhusu Jeshi la Polisi kufanyiwa tathimini kubwa, Jaji Manento alisema hilo linaweza kufanyiwa kazi, ingawa unaweza kubadili hadi jina lakini kama hakuna utashi wa utendaji hakuwezi kuwa na tija.

“Kinachopaswa kufanyika ni wale wanaokiuka sheria na taratibu ni kuchukuliwa hatua,” alisema.

“Tuangalie mfumo wa mafunzo yao, yanatolewa na watu wa aina gani. Lakini tunapaswa kuwa na mtazamo wa kifikra kuanzia kwenye mafunzo na wawe wanafundishwa na watu wenye uwezo,” alisema.

“Polisi wanahitaji chombo cha kusimamiwa. Tuwe na Tume ambayo itakuwa inasimamia utendaji wa polisi. Askari mmoja au wawili wakiambiwa mmetumia madaraka vibaya wanachukuliwa hatua na wanatangazwa, ‘fulani na fulani wamewaweka ndani watu zaidi ya muda, wamefanya hivi na hivi’, mkiwafukuza, wengine hawatafanya hivyo,” alisema

“Bila kufanya hivyo ni kazi bure, ni sawa na mimi mzee, ukinipa suti mpya nikavaa, siwezi kuwa kijana nitabaki hivi hivi. Kwa hiyo hata tukibadili jina la polisi haitasaidia, kikubwa tuwe na chombo cha kulisimamia jeshi na kuchukua hatua kwa wanaokwenda kinyume, bila kuchelewa,” alisisitiza,

Hoja ya utekelezaji wa mapendekezo hayo, inaungwa mkono na Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga ambaye hata hivyo, alisema wanaendelea kuichambua ripoti hiyo kwa kina, lakini ina mambo mazuri mengi.

“Ripoti ina mambo mazuri mengi kama suala la adhabu ya kifo, suala la kukamatakamata watu kama Takukuru, nani anakamata, saa hizi kwa mujibu wa mapendekezo ni polisi pekee. Suala la dhamana nalo, kuna makosa yenye dhama na mengine hayana,” alisema.

“Changamoto sasa tuone utekelezaji wake. Kuna kipindi Jaji Warioba alipewa kazi ya kuchunguza kero ya rushwa (ilikuwa mwaka 1996) na ile ya Katiba lakini hazikutekelezwa. Tusifurahi sana ila tufurahi tukiona utekelezaji wake kwa vitendo.”

Mapendekezo zaidi ya Tume

Ili kuweka usimamizi na mfumo madhubuti wa upelelezi, Tume imependekeza Serikali iunganishe nguvu ya upelelezi na uchunguzi iliyopo sasa katika taasisi mbalimbali za upelelezi wa makosa ya jinai na kuanzisha mamlaka mpya na iliyo huru.

Tume imependekeza chombo hicho kiitwe ama Ofisi ya Taifa ya Upelelezi (OTU) au kwa Kiingereza National Bureau of Investigation ambayo itakuwa na jukumu la kupeleleza makosa yote makubwa ya jinai kama mauaji, ugaidi na mengine.

“Pia inapendekeza mamlaka mpya iwe na bajeti inayojitegemea, uwezo wa kuajiri watumishi, kuwa na chuo bora cha mafunzo na maabara moja ya kisasa ya uchunguzi wa kisayansi na mifumo ya Tehama (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,)” imesema.

Pia imetaka kuimarishwa ubobevu wa wapelelezi huku muundo, majukumu na mipaka ya utendaji ikibainishwa katika sheria ambayo ia itaweka ukomo wa muda wa upelelezi kwa makosa yanayosikilizwa na Mahakama Kuu

‘Plea bargaining’

Katika eneo utekelezaji wa utaratibu wa kukiri kosa, Tume imesema ilipokea maoni kuwa kulikuwepo na uchelewaji wa mashauri kumalizika kwa utaratibu huo kutokana na ridhaa ya DPP kutopatikana kwa wakati.

Halikadhalika, ilidaiwa kuwa washtakiwa kulazimishwa kuingia mikataba ya kukiri makosa bila hiari; na kutokuwepo kwa uwazi kwa kuwa mashauri ya kukiri kosa nchi nzima yalishughulikiwa na DPP na timu maalumu ya maofisa wanne pekee.

Kutokana na hilo, Tume imependekeza malalamiko ya washtakiwa kulazimishwa kuingia katika makubalino ya kukiri kosa yashughulikiwe kwa njia ya mahakama kwa mujibu wa sheria ili haki itendeke kwa pande zote zinazohusika.

Pia imeshauri Ofisi ya DPP itunze kumbukumbu za majadiliano ya makubaliano ya kukiri kosa naundwe timu maalumu ya kuchunguza utata katika baadhi ya mali zilizotaifishwa katika utaratibu wa vikosi kazi na mashauri ya kukiri kosa ili kuishauri Serikali cha kufanya.

Kuachia huru washtakiwa, dhamana

Jaji Chande alisema Tume ilipokea malalamiko ya wadau kuhusu utaratibu wa Nolle Prosequi, ambapo baadhi ya watuhumiwa waliofutiwa mashtaka hukamatwa tena na kushtakiwa kwa makosa sawa na yale yaliyofutwa.

Hata hivyo, Tume imependekeza utaratibu wa Nolle Prosequi uendelee kuwepo kutokana na umuhimu wake katika kulinda masilahi ya umma kwa kumwezesha DPP kufuta mashauri ambayo yamekosa uhalali wa kuwepo mahakamani.

Kuhusu suala la dhamana kwa wanaoshtakiwa kwa utakatishaji wa fedha, Tume imependekeza tafsiri ya kosa hilo irekebishwe ili kupinguza washtakiwa wengi kukosa dhamana kutokana na tafsiri hiyo kuelezwa na Tume kuwa ni pana.

Pia Tume hiyo iliyokuwa na wabobevu, imependekeza Sheria ya Kudhibiti Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa, Sura ya 200, ifanyiwe marekebisho ili uamuzi ya kumnyima dhamana mtuhumiwa utolewe na mahakama.

“CPA Sura ya 20, irekebishwe ili mashauri ya makosa yasiyo na dhamana yaanze kusikilizwa ndani ya muda maalumu utakaowekwa kisheria na ikiwa hayajaanza kusikilizwa ndani ya muda huo, dhamana itolewe isipokuwa kama mahakama itaona kuna sababu za msingi za kumnyima dhamana mshtakiwa huyo.

Mbali na mapendekezo hayo, Tume imependekeza itungwe sheria mahususi ya dhamana (Bail Act) itakayoainisha mfumo, mamlaka na utaratibu wote wa dhamana ili kuliweka suala la dhamana kwenye sheria moja na kupunguza mamlaka zinazoshughulikia jambo hilo.

Kikokotoo mafao ya askari

Katika maeneo ambayo yana dukuduku miongoni mwa askari wa Jeshi la Polisi na Magereza ni kikokotoo cha pensheni kwa askari hao hususani wale wa vyeo vya chini kuhusu mafao yao ya uzeeni.

Msingi wa malalamiko hayo ni utaratibu mpya wa kukokotoa mafao ya mkupuo ya kustaafu ambao umeathiri kiwango cha malipo yao kutokana na malipo yao kutohusisha posho nyingi na umri wao wa kustaafu kuwa mdogo.

Tume inapendekeza mishahara ya askari wa Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza iboreshwe kwa posho za msingi zilizopo kisheria kujumuishwa katika mishahara yao ili kuwawezesha kupata mafao ya mkupuo yanayoridhisha pale wanapostaafu.

Kadhalika, Tume hiyo imependekeza umri wa kustaafu kwa askari wenye vyeo vya chini katika majeshi hayo uongezwe na kuoanishwa na ule wa watumishi wa umma ili muda wa kuchangia kwenye mfuko wa pensheni uongezeke.

Mabadiliko Jeshi la Magereza

Tume ilipokea maoni kutoka kwa wadau na wananchi kuhusu matumizi ya nguvu, ukaguzi unaotweza utu, msongamano wa wafungwa, mahabusu na wazuiliwa pamoja na uchakavu wa miundombinu ya magereza.

Pia, imesema kumekuwa hakuna mabadiliko chanya ya wahalifu wanaomaliza kutumikia vifungo vyao kama ilivyotarajiwa na hali hiyo inasababisha Jeshi la Magereza kulalamikiwa kwa ukiukwaji wa haki za binadamu.

Tume imependekeza kuwa jina la Jeshi la Magereza lifanyiwe marekebisho ya kisheria, kifikra na kimiundo kutoka kuwa sehemu ya kutoa huduma ya kuhifadhi wafungwa na kutoa huduma ya urekebishaji.

Pia imependekeza mitaala ya mafunzo ya askari magereza irekebishwe ili iendane na mabadiliko ya kutimiza majukumu ya urekebishaji ipasavyo.

Ulinzi, usalama wa watoa taarifa

Tume ilisema Sheria ya ulinzi wa watoa taarifa na mashahidi inalenga kutoa ulinzi kwa makundi hayo lakini haijabainisha taasisi mahsusi ya kusimamia na kuratibu ulinzi na usalama wa watoa taarifa na mashahidi.

Mathalan, katika kifungu cha 11 inasema mamlaka yenye jukumu la kumlinda mtoa taarifa na shahidi ikiona upo uwezekano wa maisha au mali za mtu huyo kuwa hatarini, itawasilisha kwa taasisi yenye mamlaka ya kumlinda mtoa taarifa.

Tume imependekeza sheria hiyo ifanyiwe marekebisho na kubainisha taasisi mahsusi ya kuratibu ulinzi wa mashahidi na watoa taarifa nchini ili kuimarisha ulinzi wao na iwe na bajeti ya kutosha.

Kuhusu hilo, mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media, Maxence Melo alisema, “mara nyingi watoa taarifa wanakutana na changamoto ya kujulikana au ‘washughulikiwe’.

“Mara nyingi wanasema Serikali inataka kuwajua, hapana. Ila kuna watu binafsi wakiguswa wanataka kujua ni nani wametoa taarifa,” alisema.

Alisema uwepo wa sheria madhubuti kunamhakikishia usalama mtoaji wa taarifa au ushahidi.

Melo alisema bila kufanya hivyo, anaweza kutokea kiongozi mwandamizi serikalini akazitumia visivyo sheria hizo, ikiwemo ya faragha, hususan kuwalinda watoaji wa taarifa zenye masilahi ya umma, ili ziwe kwenye mikono salama.

Akigusia utekelezaji wa mapendekezo hayo ya tume kwa ujumla, Melo alisema, “Rais wa nchi ndiye mfariji mkuu wa wananchi. Sitarajii apokee ripoti halafu asiyafanyie kazi mapendekezo.”

Aliongeza, “wananchi wanapaswa kufahamu ripoti imeandaliwa kwa kutumia fedha zetu, kwa mantiki hiyo wananchi wanapaswa kuhoji bila kujali chama alichopo, kuwataka watendaji watekeleze mapendekezo hayo ambayo yameandaliwa kwa fedha zao.

Mafunzo JKT, JKU

Pia, Tume imependekeza mifumo ya ajira ndani ya Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza ipitiwe upya ili kuendana na wakati na uwazi katika ajira za Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza uimarishwe.

Jaji Chande alisema suala la kupitia mafunzo ya JKT na JKU kwa kujitolea lisiwe kigezo cha msingi cha kujiunga na Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza hasa katika ajira za utaalamu kama vile udaktari na uhandisi, isipokuwa kigezo hicho kinaweza kuwa cha ziada.

“Utaratibu wa kuajiri askari wa Jeshi la Magereza na Jeshi la Polisi kwa kigezo cha kupitia Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi la Kujenga Uchumi kwa kujitolea umelalamikiwa na wadau unachangia baadhi ya vijana wenye sifa za kujiunga Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza kukosa nafasi,” alisema.

Magereza mguu sawa

Katika hatua nyingine, Jana Kamishna Jenerali wa Magereza, Mzee Ramadhan Nyamka alisema anakusudia kuwaita wakuu wa magereza mikoa yote nchini kufanya kikao cha kutathimini ripoti ya tume.

Hayo aliyabainisha katika hafla ya kuwapandisha vyeo mbalimbali maofisa 73 waliothibishwa na Tume ya Utumishi ya Jeshi, iliyofanyika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji kilichopo Ukonga, Dar es Salaam.

Nyamka alitumia fursa hiyo kuzungumzia ripoti hiyo akisema anachosubiri kwa sasa ni kukabidhiwa kitabu hicho na kuangalia maeneo yanayomuhusu kusimamia na kutoa maelezo kwa watendaji wake kuyatekeleza.Alisema baada ya tathimini hiyo kama kuna mtu ambaye hataelewa watawashirikisha wajumbe walioiandaa ripoti hiyo kutoa ufafanuzi na maelezo ya ziada.

“Ni hatua niliyojipanga nayo kwa sasa katika kutekeleza kwa ukamilifu, na maafisa wangu wawe tayari kwa utekelezaji yale yote yaliyopendekezwa ndani ya ripoti,” alisema Kamishna Jenerali Nyamka

Kuhusu msongamano wa magereza, alisema iwapo mapendekezo ya ripoti ya tume yatafanyiwa kazi kwa kujenga magereza katika wilaya, zitasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa.

“Mapendekezo ya kujenga Magereza katika wilaya ambazo hazina tukifanikiwa kwenye hilo tutakuwa tumetibu tatizo la mrundikano wa wafungwa ndani ya magereza, hasa ya mjini,” alisema

Alisema kiuhalisia msongamano huo unachangiwa na Wilaya mpya 49 ambazo hazina magereza, hivyo wafungwa wanaenda kwenye wilaya za karibu na kusababisha msongamano.

“Uwezo wa Magereza zetu sasa ni kuhifadhi wahalifu 29,000 lakini kuna wakati unakuta wakati mmoja tuna wahalifu 31,000 na ukitazama kiundani msongamano upo katika magereza makuu na yale ya wilaya yanayopokea wafungwa na mahabusu kwa pamoja,” alisema.

Kuacha matumizi ya kuni

Kuhusu agizo la kuacha kutumia kuni, alidai lilitolewa muda mrefu sasa kwa jeshi hilo na kwamba ilikuwa amri kwao, lakini katika bajeti ya mwaka 2023/24 Serikali imewatengea kiasi kidogo cha fedha kuanzia ili kuondokana na matumizi hayo.

“Katika Magereza makubwa ambao ni watumiaji wakubwa wa kuni wanaenda kujenga mifumo ya kutumia gesi, lakini pia watatumia makaa maalumu yanayotengenezwa kwa kutumia makaa ya mawe,” alisema.

Alisema walishafanya majaribio katika gereza la Isanga na matokeo yake yalikuwa mazuri kwamba watatumia makaa hayo mbadala kwa gharama ya chini badala ya kuni. “Badala ya kuwa waharibifu wa mazingira tutakuwa waboreshaji wa mazingira katika nchi yetu,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi