Kitaifa

Faida, hasara mtoto kulelewa na mzazi mmoja

Watu wengi wameendelea kuzungumzia suala la maadili, hasa kwa vijana.

Kwa mfano hili wimbi la panyarodi linaloendelea kutajwa kwa vitendo viovu, hii ni miongoni mwa sababu kubwa ya mmomonyoko wa maadili.
Inaonekana dhahiri baadhi ya wazazi wameshindwa kutimiza jukumu la malezi ya watoto wao.

Nasema hivi kwa sababu wengi wao wanaotekeleza uhalifu huo ni watoto wa miaka kuanzia 14 na kuendelea ambao kama mzazi akiwa makini kwenye malezi, hawezi fikia hatua hiyo ya kupoteza maadili.

Lakini kabla hatujafika mbali, hebu tujiulize, maadili ni nini?
Furaha Mwankenja ni mmoja wa wataalamu wa saikolojia, aliwahi kuniambia, maadili ni mafundisho yanayotolewa hasa katika malezi yanayomjenga mtu katika kutenda mema katika nyanja tofauti.

Amesema tunapozungumzia maadili kwa vijana, moja kwa moja tunamtazama mzazi ambaye ndiye kinara namba moja wa kumfanya mtoto ama kijana wake kukua katika maadili.

Wajuzi wa sayansi ya jamii kwa upande wao pia wanasema malezi kabla na baada ya kuzaliwa mtoto, yanaweza kubashiri makuzi yake katika siku za usoni.
Lakini kwa upande mwingine, viongozi wetu wa dini nao wanatuambia ili mtoto au kijana aonekane yupo mwenye maadili, ni pale tu wazazi wake wanapochagua mtindo wa maisha unaojikita katika hofu ya Mungu.

Wanasema hofu ya Mungu inamsaidia mzazi pia kumsaidia mwanaye kujitenga na uovu na kujikuta akiilea familia yake katika misingi bora ya maadili kulingana na dini aiabuduyo.

Sasa tunapozungumzia maadili kwa vijana, suala hili linajikita kwenye misingi ya malezi na makuzi tangu utotoni, kwa sababu malezi kwa watoto ndani ya familia yanawategemea sana wazazi na jamii inayowazunguka.

Hivyo, kuanzia hapo, tunaweza kujiuliza swali je, hii kasi ya mmomonyoko wa maadili kwa vijana hivi sasa inatengenezwa na nani? Au ni nani tumlaumu katika hili.
Kwa upande wangu jibu lake ni wazazi na jamii inayomzunguka huyu kijana.

Lakini wengine watasema ni kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia inayowafanya vijana wengi kujikita kwenye matumizi ya mitandao ya kijamii, je, lina ukweli kwa asilimia 100? Mimi mzazi nasema hapana, bali linachangia kwa asilimia fulani lakini si kwa 100.

Hapo juu nimeandika malezi bora ya mtoto huanzia kwenye familia iliyo na hofu ya Mungu. Na hofu ya Mungu si kwamba ndiyo kila siku wazazi na watoto wao wakakeshe kanisani na msikitini kuitafuta hiyo hofu ya Mungu, la hasha!

Bali nazungumzia maisha yale ambayo familia hizi zinaweza kuishi kwa kuhakikisha yanakuwa na usafi wa moyo kwa kiwango kinachotakiwa.
Kwa sababu tabia ya mzazi inapaswa kuwa kioo kwa mtoto wake hata atakapofikia umri wa ujana.

Hivyo, mmomonyoko wa maadili kwa vijana ni matokeo ya malezi katika hatua za mwanzo kabisa utotoni.

Tabia ya mzazi au mlezi wake, inaweza kupimwa katika akili za kijana mwenye maadili au aliyekumbwa na mmomonyoko wa maadili.

Kwa maana hiyo, mzazi au mlezi kamwe hawezi kujitenga na lawama ya aina yoyote pale yanapotokea matatizo kwa vijana.

Uwajibikaji wa makundi yanayotajwa katika jamii kinaweza kuwa kigezo cha pili cha mmomonyoko wa maadili.

Na hapa ndipo unapokuta kuna kundi la vijana ambao wamelelewa kwenye familia zenye hofu kuu ya Mungu, maadili yametamalaki, lakini ghafla tu akaibuka na tabia ya aina yake.

Na hapa napo ndipo lile swali langu la awali, mmomonyoko wa maadili kwa vijana, nani alaumiwe? Swali linalogusa hisia na kariba za watu makundi mengi.

Ila wazazi tukumbuke mtoto anapozaliwa, kichwa chake kinakuwa wazi kwa ajili ya kupokea na kujifunza na kuiga mambo mapya yote kutoka kwa wazazi wake. Kile anachokipokea, ndicho kinachokwenda kuujaza moyo na ubongo wake hata baada ya kuufikia ujana na utu uzima kabisa. Na akifikia umri wa ujana, ndipo unaweza kuitambua msimamo wa tabia yake.

Ila tunaponyoosha kidole kwa mzazi, kijana naye anayo nafasi yake ya kuepuka mmomonyoko huu wa maadili.

Kama walivyo na haki ya kulelewa wakiwa watoto, bado wanawajibika kulinda maadili yao, mzazi sema na mwanao pale unapoona anapotoka, haenendi kadiri ya ulivyomkuza kimaadili.

Huenda ukaja kubaini matumizi ya sayansi na teknolojia na kuiga kutoka kwa wageni na matumizi ya mtandao ndiyo iliyomsababishia abadilike kitabia.
Kwa sababu wataalamu wanatuambia suala la mmomonyoko wa maadili kwa vijana ni tatizo pia linalosababishwa na vyanzo vingine vingi ambavyo wazazi huenda hawavifahamu.

Hivyo ili kukabiliana nalo, linahitaji nguvu ya pamoja kwa lengo la kuwarudisha wale waliokengeuka katika mfumo bora wa malezi.

Wamesema mara nyingi tabia huchangia kuathiri yale yote ambayo mzazi wakati mwingine humfundisha mtoto wake.

Wamesema mtoto anapojifunza mara zote anahitaji kuombewa, kupendwa na kuambiwa maneno ya kutia moyo na wazazi wake.
Kwa sababu vinywa vya wazazi hutoa maneno yenye baraka, hasa wanaponuwia jambo jema au baya kwa mtoto wao.

Kama wazazi watazungumza maneno mabaya kwa mtoto katika makuzi, basi shetani naye hutumia nafasi hiyo kuendelea kumchanganya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi