Kitaifa
Bodi yaongeza mikopo vyuoni
Unguja/Dar. Wakati Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) likitangaza matokeo ya kidato cha sita mwaka 2023 huku asilimia 99.23 ya watahiniwa wakifaulu, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imefungua dirisha la kuomba mikopo, huku ikiongeza Sh77 bilioni.
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Mohamed alitangaza matokeo hayo visiwani Zanzibar juzi, huku Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga akizindua dirisha la kuomba mikopo litakalodumu kwa siku 90 kuanzia leo hadi Oktoba 15.
Wanafunzi wa elimu ya juu 205,000 katika mwaka wa masomo 2023/24 wametengewa Sh731 bilioni ambazo ni ongezeko la Sh77 bilioni ikilinganishwa na fedha zilizotolewa mwaka uliopita wa masomo Sh654 bilioni kwa wanafunzi 194,438.
Akitangaza matokeo hayo, Dk Mohamed alisema ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 0.26 ikilinganishwa na mwaka jana, huku wavulana wakiongoza kwa ufaulu.
Alisema watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani ni 106,883, kati ya hao wasichana ni 47,340 na wavulana 59, 543.
“Jumla ya watahiniwa 104,549 sawa na asilimia 99.23 ya watahiniwa waliofanya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2023 wamefaulu. Wasichana waliofaulu ni 46,707, sawa na asilimia 99.51 na wavulana ni 57,843 sawa na asilimia 99.00,” alisema Dk Mohamed.
Kati ya wote, watahiniwa wa shule waliofanya mtihani walikuwa 96,319 sawa na asilimia 99.44, wasichana 43,366 na wavulana 52,953 huku 539 sawa na asilimia 0.56 hawakufanya mtihani.
Dk Mohamed alisema, kati ya watahiniwa 10,025 wa kujitegemea waliosajiliwa, watahiniwa 9,258 sawa na asilimia 92.35 walifanya mtihani na 767 sawa na asilimia 7.65 hawakufanya mtihani.
Mwaka 2022 waliofaulu walikuwa 93,136 sawa na asilimia 98.97, hivyo ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 0.26 ikilinganishwa na mwaka 2023.
Dk Mohamed alisema ufaulu ni mzuri zaidi kwa wavulana ambao ni 52,463, sawa na asilimia 99.36 ikilinganishwa na wasichana 42,979 sawa na asilimia 99.24.
Pia, katika ufaulu wa daraja la kwanza wavulana wamefaulu vizuri kwa asilimia 40.57 kuliko wasichana kwa asilimia 34.88.
Alisema, katika matokeo hayo watahiniwa 95,442 wamepata ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu lakini ufaulu mkubwa ukiwa katika daraja la kwanza na la pili.
Daraja la kwanza ni watahiniwa 36,527 sawa na asilimia 38.01, wenye wastani wa ufaulu kati ya gredi A na C sawa na wastani wa alama 60 hadi 100.
Daraja la pili ni watahiniwa 44,312, sawa na asilimia 46.11 wenye wastani wa ufaulu wa gredi D sawa na alama 50 hadi 59.
Dk Mohamed alisema ufaulu wa daraja la tatu ni watahiniwa 14,603 sawa na asilimia 15.19 wenye wastani wa ufaulu wa gredi E (wastani wa alama 40 hadi 49).
Mwaka 2022 watahiniwa waliopata ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu walikuwa 83,877, sawa na asilimia 99.24.
“Hivyo ubora wa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 0.06 ikilinganishwa na mwaka jana,” alisema Dk Mohamed.
Kutokana na ufaulu huo, wadau wa elimu waliozungumza na gazeti hili walisema hatua hiyo inachochea hata upande wa ngazi za elimu ya juu kuhakikisha wanaandaa mazingira mazuri.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza), Professa Moh’med Makame Haji alisema jambo hilo linatia moyo kuona elimu inazidi kupanuka, huku akisema umefika wakati sasa taasisi za elimu ya juu kuandaa mazingira wezeshi kwa kuwa na programu zenye uwezo wa kuwapokea wanafunzi hao.
“Ufaulu huu unaonyesha hatua za elimu tunayofikia, hata sisi tulio huku tunapata faraja kwa sababu kada zetu zinapata wanafunzi wa kutosha, lakini bado taasisi nyingi za elimu ya juu hazina uwezo wa kuchukua wanafunzi wengi katika mazingira bora na wezeshi,” alisema
Profesa Haji alisema katika programu za sayansi na afya bado zinakabiliwa na changamoto kubwa, hivyo maeneo hayo yanahitaji kuongezewa nguvu wakati wakupokea wanafunzi hao,
Alisema idadi hiyo inaongeza hata wanaopata mikopo inakuwa kubwa na kuwafanya wengine wasipate mkopo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St John, Shadidu Ndossa alisema kiwango hicho cha ufaulu ni matunda ya uwekezaji mkubwa uliofanyika katika shule za sekondari, ikiwamo kujenga maabara zinazotoa fursa kwa wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza kufanya majaribio ya kisayansi.
“Tofauti na ilivyokuwa zamani wakati tunasoma sisi, siku hizi shule nyingi zina maabara, watoto wanamaliza kidato cha nne wanajua kufanya majaribio ndio maana hata wakienda kidato cha tano na sita ufaulu unakuwa mkubwa kama tunavyoona sasa kwenye tahasusi za sayansi,” alisema Ndossa.
Kufutwa, kuzuiwa
Katika matokeo hayo, Dk Mohamed alisema watahiniwa 11 matokeo yao yamefutwa, kati ya hao wanane wa shule na watatu kujitegemea waliobainika kufanya udanganyifu.
Alisema wamezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 169, wakiwamo 153 wa mtihani wa kidato cha sita, wanane mtihani wa ualimu daraja A (GATCE) na wanane wa mtihani wa stashahada ya ualimu wa sekondari (DSEE) waliopata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani msomo yote au idadi kubwa.
“Watahiniwa wamepewa fursa kufanya mtihani (mwaka 2024)kwa masomo ambayo hawakuyafanya kwa sababu ya ugonjwa kwa mujibu wa kifungu cha 32(1) cha kanuni za mitihani.”
Katika hatua nyingine Nacte, imesitisha mtihani wa maarifa (QT) badala yake imeruhusu watahiniwa wa kujitegemea kufanya upimaji wa kitaifa kidato cha pili.
Kwa kawaida baraza limekuwa likiendesha mtihani wa maarifa QT.
Lengo la mtihani huo lilikuwa kuwezesha watahiniwa wanaosoma kwa njia mbadala kupata sifa ya kufanya mtihani wa kidato cha nne baada ya kufaulu mtihani huo.
“Kwa kuwa maudhui ya mtihani wa maarifa (QT) na upimaji wa kitaifa wa kidato cha pili (FTNA), yanafanana baraza limefanya maboresho ya usajili na utahini wa watahiniwa wa kujitegema kwa ngazi ya kidato cha pili kwa lengo la kupata sifa ya kufanya mtihani wa kidato cha nne,” alisema.
Ufaulu katika umahiri, masomo
Dk Mohamed alisema idadi ya shule katika makundi ya umahiri inaonyesha kati ya shule zote 876 zenye matokeo ya ACSEE 2023, shule 643, sawa na asilimia 73.40 zimepata wastani wa daraja la C.
Pia alisema shule zilizopata wastani wa daraja la A-C zimeongezeka kwa asilimia 6.62 kutoka 622 sawa na silimia 74.31 mwaka 2022 hadi kufikia shule 709 (asilimia 80.33) na hakuna shule yenye wastani wa daraja la S au F.
Alisema takwimu zinaonyesha watahiniwa wamefaulu vizuri katika masomo mengi kwa kuwa na ufaulu kati ya asilimia 97.74 na 100 isipokuwa somo la Basic Applied Mathematics ambalo lina ufaulu wa asilimia 68.53.
Hata hivyo, alisema ufaulu katika somo hilo umeimarika kutoka asilimia 58.66 kwa mwaka 2022 hadi 68.56 mwaka huu.
Mikopo yaongezeka
Jana, akizindua dirisha la mikopo, Naibu Waziri, Kipanga alisema HELSB imeshazindua mwongozo wa uombaji wa mikopo kwa mwaka mpya wa masomo na kuwataka waombaji kusoma maelekezo yaliyopo kwenye mwongozo kabla ya kutuma maombi ili kuepusha uwezekano wa kufanya makosa yatakayowagharimu kukosa mikopo.
“Dhamira ya Serikali kuwawezesha vijana wa Kitanzania kupata elimu ya juu inaonekana kwa vitendo na ndiyo maana jitihada hizi zinachukuliwa. Haitapendeza kuona waombaji wanakosa mkopo kwa sababu ya kutozingatia maelekezo yaliyotolewa kwenye mwongozo huo,” alisema Kipanga.
“Kutolewa kwa mwongozo huu kunatoa fursa kwa wanafunzi na wazazi kusoma kabla ya kuanza kuomba mikopo, hatutarajii makosa kwa sababu maelekezo yote yametolewa kwenye mwongozo.”
Naibu waziri huyo alifafanua kuwa ufunguzi wa dirisha hilo la maombi ya mikopo hauwahusu wanafunzi wa ngazi ya diploma na kuwataka kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiandaa utaratibu wa kundi hilo kupata mikopo kama ilivyoahidiwa kwenye bajeti kuu iliyowasilishwa bungeni Juni mwaka huu.
Kuhusu wanafunzi wanaoendelea na mafunzo katika kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema mwongozo huo utasambazwa kwenye kambi zote na watatuma maombi ya mikopo baada ya kumaliza muda wao wa mafunzo.
Kwa upande wake, Kabidhi Wasii Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (Rita), Frank Kanyusi alisema taasisi hiyo imejiandaa kufanikisha uhakiki wa nyaraka zinazopaswa kutolewa na taasisi hiyo.
“Tumetengeneza mfumo kwa kushirikiana na bodi ya mikopo ambao utawezesha waombaji kuhakiki vyeti vyao kwa njia ya mtandao na kurejeshewa majibu kwa njia ya mtandao, wakati huo bodi watapata taarifa kwa kuwa mifumo imeunganishwa,” alisema Kanyusi.