Kitaifa
Hujuma, upigaji vyabainika NHIF
Dar es Salaam. Kuyumba kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) huenda kumechangiwa na mambo matano, zikiwemo hujuma na upigaji kupitia matumizi yasiyo sahihi ya kadi za wanachama.
Miongoni mwa mambo hayo ni wasio wanachama kutumia kadi za wanachama kupata huduma, baadhi ya wanachama kuacha kadi hospitali na kutumika isivyo, watoa huduma kutozingatia taratibu za uhakiki, kadi kuwa na taarifa zenye shaka na nyingine kudurufiwa kwa nia ovu.
Katika uhakiki wake, NHIF imebaini kadi 1,346 zinatumika kwa wasio wanachama wala wanufaika wa mfuko huo, ikidaiwa kuwa ama wameziazima kwa wanachama au taarifa zake zimeghushiwa.
Hayo yamebainika kupitia uhakiki wa wanachama uliofanywa na NHIF kuanzia Juni 1, mwaka huu katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Arusha, Kilimanjaro na Dodoma.
Uhakiki huo unafanyika ikiwa ni mwaka mmoja, tangu wadau kuibua wasiwasi kuwa huenda mfuko huo ukafilisika, kutokana na mwenendo mbaya wa uendeshaji wake.
Hofu ya kufilisika kwa mfuko huo, ilitokana na kile kilichowahi kuelezwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/22.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, NHIF ilivilipa vituo vya afya madai yasiyo ya kweli kiasi cha Sh14.46 bilioni kwa kipindi cha mwaka 2019/20 hadi 2021/22.
Wakati CAG akiyasema hayo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano NHIF, Angela Mziray alifafanua madai hayo akisema watumishi wa vituo vya matibabu ambao ripoti inasema tayari wameripotiwa kwenye mabaraza ya kitaaluma.
Pia alisema watumishi wa NHIF waliokuwa 17 tayari walisharipotiwa kwenye kamati za nidhamu za mfuko.
Akitoa taarifa ya uhakiki wa wanachama jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Benard Konga alisema uchambuzi unafanyika kujua gharama za matibabu zilizotumiwa na watu hao.
Alisema iwapo zitajulikana, wanachama watapaswa kuzilipa pamoja na hatua nyingine za kisheria watakazochukuliwa.
“Kila tulipobaini hilo, tulimnyang’anya mtu huyo kadi na kubaki nayo kisha kutoa taarifa kwa mwanachama tukimtaka aje kuifuata kadi yake ofisini,” alisema.
Uhakiki huo, alisema umebaini uwepo wa wanachama 2,490 walioacha kadi zao kwenye vituo vya kutolea huduma.
Kutokana na hilo, Konga alisema uchunguzi unaendelea kubaini iwapo ni watoa huduma waliotaka wanachama waache kadi ili watengeneze madai baadaye au wanachama wenyewe walizisahau.
“Nitoe rai kwa wanachama kuhakikisha unaposaini baada ya kupata huduma, chukua kadi yako na kwa watoa huduma iwapo mwanachama amesahau ni jukumu lao kutupatia taarifa sisi ili tuzifuate na kumrejeshea mwanachama,” alisema.
Jambo lingine lililobainika kutokana na uhakiki huo ni kudurufiwa kwa kadi za wanachama, akisema baadhi hutoa nakala na kwenda nazo katika vituo vya kutolea huduma.
“Hilo limebainishwa wazi kuwa ni kinyume na mikataba yetu, kwamba mwanachama atibiwe kwa kadi halisi atakayokuja nayo,” alisema.
Katika kudhibiti ujanjaujanja, alisema matumizi ya alama za kibaiolojia kama vidole na sura yanatarajiwa kuanza karibuni.
Alisema uhakiki huo, umebaini baadhi ya watoa huduma hawazingatii taratibu za uhakiki wa wanachama kabla ya kuwapa huduma, jambo linalosababisha wasiostahili kuhudumiwa.
Jingine lililobainika ni ule mtindo wa mtu kumtuma ndugu, jamaa au rafiki kwenda kumchukulia dawa.
“Kwamba mimi naumwa, nampa ndugu yangu kadi yangu aende kunichukulia dawa, miongozo ya tiba inataka daktari amuone mgonjwa ndipo atoe tiba,” alisema.
Kulingana na Konga, kadi 3,589 zimebainika kuwa na taarifa zenye mashaka na hivyo wanachama wanaozimiliki wanapaswa kwenda katika ofisi za NHIF kuzihuisha.
Mkurugenzi huyo alisema uhakiki huo umesababisha NHIF kusitisha kutoa huduma kwa taasisi 88 ambazo waajiriwa wake wengi wamehusika katika makosa yaliyobainishwa.
“Kwa hiyo, taasisi kama 88 tumesitisha kuwapa huduma na tumeshawataarifu nia ya kukaa nao mezani na kama wanataka kuendelea tutawapa masharti kwa kuwa wanapaswa kuwa walinzi wa mfuko,” alisema.
Pia katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, mfuko huo ulisitisha mikataba 48 ya watoa huduma waliofanya biashara katika hali ya ujanjaujanja.
Pamoja na mikataba hiyo, alisema wataalamu 139 wa huduma za afya walichukuliwa hatua mbalimbali kulingana na sheria na miongozo ya nchi.
Kadhalika, wanachama 1,197 walichukuliwa hatua mbalimbali ikiwemo kusitishiwa matumizi ya kadi zao, kulipia gharama na kuripoti katika vyombo mbalimbali vya uchunguzi.
Akizungumzia hilo, Rais wa Tanzania Health Summit, Dk Omary Chillo alisema ulaghai wa wanachama inaweza kuwa moja ya sababu za hasara katika mfuko huo, ingawa zipo nyingine zinazochagiza hilo.
“Hii inaweza kuwa moja ya sababu, lakini zipo na nyingine. Kweli kumekuwepo na wanachama wasio waadilifu, hawaaminiki wanawapa wenzao kadi wanazitumia kinyume na utaratibu,” alisema.
NHIF iboreshe teknolojia
Ili kuondokana na kadhia hiyo, maboresho katika mifumo ya teknolojia, yametajwa kuwa mwarobaini wa changamoto hizo, kwa mujibu wa wadau wa bima nchini.
“Watumie alama za vidole na wahakikishe wanaweka mitambo hiyo katika kila hospitali kwa sababu gharama yake si kubwa, ni jambo linalowezekana,” alisema Mkurugenzi wa Utafiti na Huduma za Ushauri kutoka Chuo cha Bima Afrika, Anselmi Anselmi.
Alieleza kuwa utaratibu huo ndio unaotumika na kampuni mbalimbali binafsi za bima, ndiyo maana ni nadra kusikia aina yoyote ya udanganyifu ikifanyika kwa kampuni hizo.
“Kampuni binafsi zote zinaweka ‘biometric’ alama za vidole au uso, hasa katika hospitali ambazo wanaona zina wateja wengi, kwa hiyo NHIF inapaswa kufanya hivyo,” alisema.
Kilichoelezwa na Anselmi kinaungwa mkono na Mkuu wa zamani wa mawasiliano katika taasisi isiyo ya Kiserikali ya Sikika, Lilian Kallaghe aliyesema matumizi ya teknolojia ndiyo suluhu ya udanganyifu huo.
Alitolea mfano kampuni tatu tofauti alizowahi kuwa mwanachama, akisema zinatumia alama za vidole kuhakiki taarifa za mteja.
“Kuna siku kwa bahati mbaya nilienda na kadi ya mume wangu, nilipoweka kidole tu waliniambia hii kadi si yako, nilipotoa nikaona ya mume wangu, kwa hiyo ukitumia alama za vidole itasaidia,” alisema.
Kulingana na Lilian, umefika wakati kwa NHIF kuiga kile kinachofanywa na kampuni nyingine, ili kudhibiti baadhi ya changamoto.