Kitaifa

Kukwama upanuzi Mloganzila maumivu upande wa huduma

Kukwama kwa ujenzi wa upanuzi wa Hospitali ya Taaluma na Tiba Mloganzila umetajwa kuwa miongoni mwa sababu za kusuasua na upungufu wa watalaamu.

Wakati hospitali hiyo inaanzishwa mwaka 2016, matarajio yalikuwa ni kuwepo kwa jengo la hospitali kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu na majengo mengine kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa madaktari na wataalamu wengine wa afya wapatao 15,000 kila mwaka, jambo ambalo halijafanyika.

Miaka saba baadaye kilichokamilika katika hospitali hiyo iliyopo katika eneo lenye ukubwa wa ekari 3,800 ni majengo mawili tu — lile la Hospitali na la Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu, huku yale ya chuo cha afya yakikosekana.

Mradi huo ambao ungehusisha mabweni ya wanafunzi, jengo la kufundishia, maktaba, bwalo na maabara, ambao ungegharimu Sh13.3 bilioni, ulianza mwaka 2016 baada ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutiliana saini ya makubaliano na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kabla ya kuusitisha kimyakimya mwaka 2018.

Hadi Juni 17, 2023 kazi iliyofanyika katika eneo la mradi ni uchimbaji wa msingi na baadhi ya kuta za majengo saba, ambayo hata hivyo yamefunikwa na nyasi ndefu na miti iliyoota.

Hali ikiwa hivyo, bado wataalamu wanaamini kuwepo kwa chuo cha afya na tiba Kampasi ya Mloganzila, kungeleta tija katika utoaji huduma kwa wagonjwa na maendeleo ya hospitali kwa ujumla, badala yake kumekuwa na simulizi zinazoacha maswali lukuki.

Kusuasua kwa huduma

Kutokamilika kwa mradi huo kumechangia malalamiko na kusuasua katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa hospitalini hapo, uchunguzi wa Mwananchi kwa takribani miezi saba umebaini.

Kulingana na uchunguzi huo, mkwamo huo umechangia wataalamu wengi kuhama na kwenda katika hospitali zingine kubwa zenye vyuo jirani kwa ajili ya kujiendeleza kitaaluma au kufundisha, zikiwemo Benjamin Mkapa (Dodoma), Bungando (Mwanza), KCMC (Kilimanjaro), Mbeya, Muhimbili, Iringa na vyuo vingine.

Hospitali hizo kubwa, zimekuwa zikipata wataalamu wengi kutoka vituo mbalimbali vya afya kote nchini, wakiwemo madaktari wa kawaida na mabingwa ambao wanajiendeleza kielimu na kufundisha katika vyuo hivyo huku wakiendelea kufanya kazi, fursa ambayo inakosekana Mloganzila.

Mkwamo huo unaondoa thamani ya uwekezaji wa mabilioni ya fedha uliyofanywa na Serikali katika kuifanya Mloganzila kuwa hospitali ya taaluma na tiba, ambao uligharimu Dola za Marekani 61 milioni (Dola 18 milioni 18 za Serikali na mkopo wa Dola 43 milioni kutoka Korea.)

Maswali kibao

Kwanini mradi huo haukujengwa na kukamilika kwa wakati? Ni nani anawajibika katika hili? Fedha ambazo TBA ilipewa kama malipo ya awali zimefanya kazi ipi? Nini hatima ya mradi huo kwa sasa? Hayo ni baadhi ya maswali yanayogonga vichwa kuhusu mradi huo.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Sylvia Lupembe alisema mkataba na TBA ulivunjwa baada ya taasisi hiyo kulipwa Sh3.9 bilioni lakini ikasuasua kutekeleza mradi huo.

Uongozi wa TBA ulipoulizwa juu ya suala hilo, awali ulisema unaandaa majibu lakini siku ulipomwita mwandishi kuyatoa Aprili 11 mwaka huu, ulisita kufanya hivyo.

Badala yake TBA iliomba muda zaidi na hata Mei 8, siku ambayo Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Daud Kandoro alikutana na kufanya mazungumzo na mwandishi, aliomba muda zaidi. Subira iliendelea na hata ilipofika Juni 17 bado hakukuwa na majibu yaliyotolewa.

Hata hivyo, taarifa za ndani ambazo Kandoro hakuwa tayari kuzithibitisha, zilieleza kuwa katika mradi huo ambao TBA ilipewa ukandarasi, pia kulikuwa na kandarasi nyingine kutoka serikalini.

Ujenzi wa kampasi hiyo, kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika, ulitakiwa kwenda sambamba na ujenzi wa hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) maarufu kama Hosteli za Magufuli.

Mkwamo wa mradi

Vuta nikuvute kati ya Wizara ya Elimu na TBA ilianza kipindi cha awali cha ujenzi wa mradi huo mwishoni mwa mwaka 2017.

Januari 20, 2018 Waziri wa Elimu wakati huo, Profesa Joyce Ndalichako alieleza kuchukizwa na maendeleo duni ya ujenzi huo uliokuwa umesimama kukiwa na msingi wa majengo manne pekee.

“Hamko makini na kazi yenu, niwahakikishie ikifika Jumamosi sijaona kinachoendelea nawachukulia hatua. Haiwezekani nimewapa fedha tangu Agosti mwaka jana (2017) mpaka leo mmechimba msingi pekee, nahangaika ujenzi ukamilike madaktari wakae hapa watoe huduma kwa wagonjwa, ninyi mnaleta mchezo, nipo kazini lazima mtii ninachokiagiza,” aling’aka Profesa Ndalichako.

Meneja wa TBA Kanda ya Dar es Salaam, Manasseh Shekalaghe alimweleza Profesa Ndalichako kuwa kilichokwamisha ujenzi huo zilikuwa ni mvua zilizonyesha na msingi ukafukiwa na udongo.

Hata Makamu wa Rais (wakati huo) Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara eneo hilo Juni 9, 2018 alieleza kushangazwa na kusuasua ujenzi wa mradi huo.

Alisema kuharakishwa kwa ujenzi huo kungeiwezesha hospitali hiyo kufanya udahili wa wanafunzi wengi zaidi na nchi kufaidika kwa kupata wataalam, jambo ambalo halijafanyika hadi sasa.

Hata hivyo, Juni 21, mwaka huu Mwananchi alipotaka kujua hatima ya mradi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo alisema Serikali inaangalia namna ya kuukamilisha.

“Tunajua ni mradi uliosimama na lazima ukamilike. Tunahitaji kuukamilisha, Watanzania wengi wanauhitaji na vijana wanahitaji elimu, fedha ikipatikana ujenzi utaendelea,” alisema.

Profesa Nombo alipoulizwa hatima ya fedha hizo zilizokwishatumika na mikataba ya ujenzi, alisema “mambo mengine ni ya kiutawala kwa sasa tunaangalia imalizwe watoto waweze kusoma, kama kuna taarifa sisi Wizara ya Elimu tutaitoa.”

Madaktari wanavyohama

Tangu kuzinduliwa kwa hospitali hiyo yenye vitanda 608 mwaka 2017, wataalamu wa afya wamekuwa wakifika kutoa huduma na kuondoka hasa wale ambao wanajiendeleza kielimu kutokana na kukosekana chuo na makazi karibu na eneo la kazi.

“Ninajiendeleza kielimu nilitamani kuendelea kutoa huduma Mloganzila lakini kutokana na kukosekana kwa kampasi pale, imenilazimu kutafuta chuo kingine nje Dar es Salaam,” alisema mmoja wa madaktari aliyewahi kuhudumu hospitali hiyo huku akitaka kutotajwa jina.

Daktari mwingine alisema; “kuna kitu kimoja Serikali inapaswa kugundua, ili kuondoa changamoto za ile hospitali wanatakiwa kujenga kampasi haraka ili sisi na madaktari wengine tusome palepale na kuendelea kutoa tiba. Hospitali itakuwa na wataalamu wengi kama Upanga (Muhimbili).”

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Profesa Mohamed Janabi alisema pamoja na ukweli kwamba kwenye kada ya afya lazima wataalamu wajiendeleze, lakini hawawezi kuondoka wataalamu wote.

“Kuna kozi fupi na wapo wanaoenda kozi ndefu. Mimi ndiye mtia saini wa mwisho kabisa, haiwezekani kitengo kina wataalamu 10 tukawaruhusu wanane wakasome, haiwezekani. Tunapotoa ruhusa tunahakikisha haziathiri huduma,” alisema.

“Ni kweli wanaenda kusoma kwa kuwa vitu vinabadilika, huwezi kutumia teknolojia ya mwaka 2000 ukamtibu mgonjwa leo, ndiyo maana wataalamu wetu wanasoma siku baada ya siku.”

Alipoulizwa mkwamo wa kampasi ya Mloganzila umeathiri kwa kiasi gani utoaji wa huduma katika hospitali hiyo, alisema “hili swali aulizwe Makamu Mkuu wa Chuo cha Muhas.”

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano kwa umma Muhas, Hellen Mtui alisema kwa sasa hawawezi kuzungumzia hospitali hiyo kwa sasa.

“Sisi kama chuo tuko sawa, ila ujenzi ungekamilika tungeweza kudahili wanafunzi wengi zaidi,” alisema.

Uongozi wafafanua

Upungufu wa madaktari na watalaamu wengine Mloganzila umekuwa ukisababisha hofu na wasiwasi miongoni mwa jamii na baadhi ya ndugu ambao wagonjwa wao huamishiwa hapo.

Haya yanatokea Mloganzila ikiwa ni hospitali kubwa, yenye vifaa tiba na mitambo ya kisasa kuwahi kuwepo katika hospitali nyingi nchini, huku ikiwa na wodi nzuri zenye hadhi, vitanda vya kutosha na mazingira yanayofaa ikilinganishwa na hospitali zingine.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini mambo kadhaa yanayochangia malalamiko ya wagonjwa na ndugu ni kuondoka kwa wataalamu wengi.

Asilimia kubwa ya wagonjwa wanaofikishwa hospitalini hapo hutokea katika Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Upanga kutokana na wingi wa wagonjwa huku wengine wakielekezwa huko kwa ajili ya vipimo vikubwa.

Upanga yenye vitanda 1,500 haiwezi kupokea wagonjwa wote kwa kuwa idadi ya wanaopewa rufaa kwenda Muhimbili ni kubwa kwa sasa, hivyo wengi huhamishiwa Mloganzila.

Awali, hospitali hiyo ilikuwa chini ya uangalizi na uendeshaji wa Muhas, ikitambulika kama Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MAMC) mpaka Oktoba 3, 2018 ilipokabidhiwa kwa Muhimbili.

Kabla ya kuchukuliwa na Muhimbili, wataalamu waliokuwa wakitoa tiba ni pamoja na wakufunzi na baadhi ya wataalamu kutoka hospitali ya Upanga, hivyo ilikuwa ni vigumu katika kutoa huduma kwa kuwa walikuwa na majukumu mengi huku wakipambana na changamoto ya umbali wa kilomita 43 kati ya chuo na hospitalini.

Huduma zalalamikiwa

Eneo la hospitali nalo limekuwa na changamoto, ndugu wa wagonjwa huonekana wamekaa muda mrefu wakisubiri muda wa kuona wagonjwa wao wakilazimika kushinda hapo kutokana na umbali wa maeneo wanayotoka.

Wanaotoka mikoani hulazimika kukodi vyumba karibu na hospitali huku wengine wakilala katika jengo la mghahawa usiku.

Licha ya hayo, malalamiko makubwa ni uhaba wa rasilimali watu (madaktari), hali ambayo huwafanya wengi wabaki kuwa na hofu ya kuwapoteza ndugu zao.

Akitoa ufafanuzi wa changamoto hizo, Profesa Janabi licha ya kukiri kuwepo kwa malalamiko, alisema nyingine ni imani potofu kuhusu hospitali ya Mloganzila.

“Nilipoingia Muhimbili Oktoba 2022 malalamiko ya wananchi yalikuwa kuhusu hii hospitali, nikiri pia niliwahi kuyasikia kabla sijaja, nilijiuliza kwanini kuna hii changamoto ambayo kwanza wananchi wamepoteza imani na hospitali na tumeambiwa kuna upungufu wa wataalamu.

“Tulichokifanya Novemba menejimenti ilihamisha idara tatu kutoka upanga kuja huku, magonjwa ya moyo, kisukari na kiharusi, hizi kliniki tatu kila moja inabeba wagonjwa 40 mpaka 60 kwa siku,” alisema.

Sababu za kuhamisha

Profesa Janabi alisema hospitali imekuwa ikiwahamisha baadhi ya wagonjwa kwenda Mloganzila kutokana na kuwa na nafasi pamoja na vitanda vya kutosha.

“Muhimbili ina vitanda 1,500, Mloganzila 656, Muhimbili ilifikia hatua (wagonjwa) walilala wawiliwawili wakati Mloganzila ilikuwa na wagonjwa 200 na vitanda 456 vilibaki tupu.”

Alisema hatua ya kwanza ilikuwa ni kuhamisha vitengo vikubwa vitatu, Novemba 2022 walihamisha kitengo cha moyo, wagonjwa wa kisukari na wagonjwa wa kupooza ‘stroke’ na walikuwa wakihamisha idara nzima — wagonjwa na wafanyakazi wote.

“Hatukutafuta wafanyakazi wapya. Vitengo hivi vyote tulivipeleka kule ndiyo maana ukienda sasa hivi Mloganzila ina wagonjwa mpaka 450 waliolazwa.”

Profesa Janabi alisema kwa bahati mbaya hapo katikati uelewa wa wananchi ilikuwa kwamba wakipelekwa Mloganzila wanafariki.

“Sina hakina huu uelewa ulianzia wapi kwa kuwa wagonjwa wanafariki Amana, Palestina, Upanga, Muhimbili kila hospitali lakini ilikuwa bahati mbaya mgonjwa anayefariki Mloganzila ni kama kitu cha ajabu.”

Profesa Janabi alisema huenda moja ya sababu ilikuwa ni madaktari kufanya kazi Mloganzila na kisha baadaye wanarudi Muhimbili, jambo ambalo kwa sasa wamelirekebisha na sasa hospitali hiyo inatoa tiba zote vizuri, hasa upasuaji.

Vilevile, alisema ubora wa huduma unaendelea kuimarishwa na hivi sasa Mloganzila inahudumia takriban wagonjwa 800 kila siku huku akisisitiza kuwa baadhi yao hupelekwa hospitalini hapo kutokana na huduma wanazozihitaji kupatikana Mloganzila pekee.

Kuhusu suala la uchache wa wataalamu, Profesa Janabi alisema kwa sasa hospitali hiyo ina jumla ya watumishi 741 wa kada mbalimbali na kati yao madaktari ni 151 wakiwemo madaktari bingwa 88 na wa kawaida 63. Pia kuna wauguzi 315 na wahudumu wa afya 76.

“Siwezi kusema tuna wataalamu wa kutosha, tunafanya tathmini, hili ni swali gumu sana kwangu. Tumekuwa tukilizungumzia na tunatafuta wataalamu wa nje waweze kutufanyia tathmni kujua tuna upungufu wa watu wangapi, ufanisi wa kazi pamoja na uwajibikaji kwa waliopo,” alifafanua.

“Upungufu upo, lakini ni kwa asilimia ngapi, mpaka tathmini ndiyo tutajua. Tumefanya maamuzi mengi ambayo yameongeza wataalamu lakini pia kila Jumatano mimi nakuja huku natibu wagonjwa na kufanya kazi za utawala.”

Ujenzi wa kota

Kuhusu changamoto ya umbali kwa watumishi wa afya, Profesa Janabi alisema wanakusudia kujenga kota na hosteli kwa ajili ya watoa huduma.

“Mikakati ya kujenga hosteli ipo na hili halikwepeki. Dhumuni la Mloganzila wakati wa awamu ya nne ilikuwa kuongeza idadi ya wanafunzi kufikia 15,000 kwa sasa tunachukua wanafunzi 200 Mloganzila.

“Tumelizungumzia juzi, mkakati upo hatuna jinsi lazima tuongeze madarasa, hospitali iongeze majengo na chuo kiongeze madarasa na maabara za tafiti. Kuna mpango wa Muhimbili kujenga kitengo cha upandikizaji.

“Kwa sasa tupo kwenye mchakato wa mazungumzo na NSSF, PSSF kuhusu kujenga ‘appatment’ za vyumba viwili kwa ajili ya wafanyakazi, kimoja wawe wanaishi karibu, huo ndiyo mtazamo wa bodi na Wizara ya Afya. Watumishi hawa wanatakiwa kuwa na huduma zote za msingi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi