Connect with us

Kitaifa

Vyeo vya mchongo vyashtua, waziri awashukia maofisa utumishi

Dodoma. Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais) Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Simbachawene amefichua jinsi baadhi ya watumishi wanavyoukwaa ukuu wa idara na vitengo kwenye halmashauri kwa michongo ya rushwa.

Simbachawene alisema hayo wakati akifungua mafunzo kwa watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) na maofisa utumishi wa halmashauri za Tanzania Bara jijini hapa jana.

Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na TSC kufundisha jinsi ya kutumia mfumo mpya wa Taarifa Shirikishi za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS), Simbachawene alisema baadhi ya maofisa utumishi wanapokea rushwa kati ya Sh5 milioni hadi Sh10 milioni ili watoe ukuu wa vitengo na idara.

“Kwa maofisa utumishi huko kuna changamoto, rushwa ni nyingi,” alisema Simbachawene.

Alisema ujio wa mfumo huo utakuwa na taarifa zote na rahisi kuwabaini maofisa wanaowateua watendaji baada ya kupokea rushwa.

“Wako watumishi huko wilayani, wanatuambia kabisa, pale kwetu siwezi kuteuliwa hata kama nina sifa, labda mniteue ninyi moja kwa moja. Sasa sisi Wizara ya Utumishi hatuteui tu watu, kuna mamlaka za ajira, lazima zifanye michakato, lakini haifanyiki kwa sababu ya rushwa,” alisema Simbachawene.

Pia, alisema kuna changamoto ya watumishi kukaimishwa madaraka kwa muda mrefu, hali inayosababishwa na baadhi ya maofisa utumishi wanaotaka kupatiwa rushwa ndipo wapendekeze watumishi wengine.

“Hamuanzishi mchakato kwa sababu rushwa imewajaa. Nayasema haya mimi ni mbunge miaka 20, ni Waziri niliyepita wizara nyingi, wengine mko nao huko, ni jamaa zetu, ni ndugu zetu,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuanzia sasa, wakibaini kuna mtumishi mwenye sifa lakini hajaanzishiwa mchakato au kupandishwa cheo, ofisa utumishi wa halmashauri husika ataliwa kichwa.

Alisema kwa wanaofanya kazi halmashauri mchakato mara zote huanzia huko na kwenda Tamisemi.

Simbachawene alisema maofisa hao hawafuati utaratibu huo, badala yake wanaficha taarifa za watumishi wenye sifa kwa makusudi ili wawapandishe waliowapa rushwa.

“Jamani hii nchi tunaiua wenyewe, huko kwenye mitandao mnatupiga kweli wakati ninyi ndio waharibifu,” alisema Simbachawene na kuwataka wabadilike na wafanye kazi kwa weledi.

Hata hivyo, alisema maofisa utumishi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo ya ukosefu usafiri, wakati mwingine huchangisha fedha kutoka kwa watumishi kwa madai ya kwenda kuzishughulikia.

Katibu Mkuu (Ofisi ya Rais) Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi alisema kama itafanyika tathimini ya watumishi wanaopeleka malalamiko kwenye ofisi yake, wengi ni walimu.

“Ni imani yetu ujio wa mfumo huu utatusaidia kutatua changamoto za walimu. Si kwa mfumo tu, bali utashi pia,” alisema Mkomi.

Wadau wafunguka

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Hendry Mkunda alisema kwa sababu suala hilo limesemwa na mamlaka, inaonyesha mifumo ya taarifa za utumishi haiko sawa, jambo linalotoa mwanya wa upendeleo kufanyika.

Alisema kama mifumo iko sawa, hakuna uwezekano wa kuwapo rushwa, kwani iko wazi na ina taarifa za watumishi na uwezo wao kiutendaji.

“Upandishaji wa vyeo na mengine haufanyiki kwa sababu ya utashi tu wa mtu, kama kuna mwanya ndiyo kabisa. Lakini ninachokiona mimi kwa hili huenda mifumo sio rafiki inatoa mwanya,” alisema Mkunda.

Hata hivyo, alishauri kama hali iko hivyo, kuna haja ya kufanya maboresho makubwa ya usimamizi wa wafanyakazi kwa kuhakikisha mifumo iliyopo inasomana kusudi kuepusha hiki kinachoendelea.

Mmoja wa wakurugenzi wa zamani aliyeomba hifadhi ya jina lake, alisema hadhani kama kuna ofisa utumishi anaweza kutoa madaraka kwa upendeleo kwa sababu tayari kuna mfumo wa upandishaji watumishi madaraka.

“Kwanza mtumishi anajaza fomu za upimaji wa utendaji kazi wake kila mwaka, zinazoonyesha taarifa zake zote za utendaji, ambazo zinapelekwa pia katika Kamati ya Fedha na Mipango za halmashauri zinazoweza kukataa kuhusu mapendekezo ya kupandisha vyeo,” alisema.

Pia, alisema zipo bodi za ajira zinazoangalia mchakato wa upandishaji vyeo na katika mchakato huo, kuna nafasi ya wajumbe kusema hapana kwa mtu asiyestahili.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda alisema anatamani uchunguzi wa kina ufanyike kuwatambua watumishi hao na kisha kutoa maelekezo yatakayokomesha suala hilo.

“Ikifanyika hivyo, vitendo hivi vitakoma, lakini yakisemwasemwa tu halafu waachwe, inajenga sifa mbaya na mwisho wa siku hata ambao hawafanyi watasema hata kama nikifanya kuna madhara gani.”

Alisema suala hilo ni baya na linaondoa uadilifu katika utumishi wa umma kwa kudhani anaweza kuhonga ili apandishwe cheo.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi