Kitaifa
Tozo ya mafuta yaibua mvutano
Dar es Salaam. Tozo ya Sh100 iliyotakiwa kuanza kutozwa Julai mosi, mwaka huu katika kila lita ya mafuta imeibua mvutano kati ya wadau na Serikali.
Taasisi ya Wafanyabiashara wa Mafuta ya Rejareja Tanzania (Tapsoa) inadai tayari imeshaanza kulipia tozo hiyo kwenye meli tisa za mafuta yaliyoanza kuingia jana kabla ya kuyasambaza kwa watumiaji mwezi huu, ikiwa ni baada ya kumalizika akiba iliyoishia Juni 30.
Kutokana na hilo, Tapsoa inashauri Serikali iingize tozo hiyo katika mafuta ya mwezi huu.
Hata hivyo, Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), inapinga madai ya kuishiwa akiba ya mafuta, ikithibitisha uwapo wa akiba ya dizeli na petroli kwa siku 26 yasiyoathiriwa na tozo iliyopendekezwa kuanza Julai mosi.
Wiki iliyopita, Bunge liliidhinisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2023/24 iliyoanza kutekelezwa Julai Mosi mwaka huu, inayoelekeza ukusanyaji wa tozo hiyo kwa kampuni za uagizaji mafuta.
Hata hivyo, jana Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ilitangaza kushuka bei za mafuta bila kuingiza tozo hiyo.
Bei hizo ndogo katika kipindi cha miezi 16 iliyopita zinaonyesha watumiaji wa petroli iliyopitia Bandari ya Dar es Salaam hawatakuwa na maumivu mwezi huu kwa bei ya rejareja baada ya kushuka Sh137 katika kila lita moja, unafuu huo ukigusa mikoa mingine ya Dodoma, Geita, Katavi na Kagera.
Kwa mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara), bei ya rejareja ya petroli imeshuka kwa Sh188, huku mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ikiendelea na bei za Aprili 5.
Bei hizo kwa Lindi ni Sh2,807, Mtwara (Sh2,793) na Ruvuma (Sh2,879) kwenye petroli baada ya kukosekana shehena ya mafuta iliyopokewa.
Alipotakiwa kueleza utaratibu wa kuanza utozaji wa tozo hiyo, Mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alisema: “Tutawafafanulia zaidi kwa wananchi itakavyo-operate (itakavyofanya kazi), ndiyo kwanza Bunge limemalizika hivi karibuni, kwa hiyo tutawaeleza wananchi kuhusu tozo hiyo.”
Akifafanua kuhusu madai ya tozo hiyo, Katibu Mkuu wa Tapsoa, Augustino Mmasi alisema: “Kuna meli tisa zinaingia kesho (leo) na ni mafuta ambayo tumeshalipia hiyo Sh100, haya tunayaingiza sokoni kuanzia mwezi huu, lakini Ewura haijaingiza tozo hiyo ikidhani bado tuna mafuta ya Juni.
“Kwa hiyo, sisi ndiyo tunabeba mzigo wa kulipa tozo hiyo. Leo (jana) tumeandika barua kwa Wizara ya Nishati na Ewura ili waangalie namna ya kushughulikia changamoto hii,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waagizaji na Wasambazaji wa Mafuta Tanzania (Taomac), Raphael Mgaya aliyeunga mkono kutoingizwa tozo hiyo mwezi huu, alisema kuna hoja ya msingi kwa baadhi ya wafanyabiashara wanaolalamikia kumaliza akiba ya mafuta kutokana na uhaba wa Dola ya Marekani ulivyoathiri soko.
Mgaya alisema kutokana na uhaba wa Dola, baadhi walishindwa kulipia mafuta kutoka nje ya nchi, hatua iliyowaathiri kupunguza kiasi cha kuagiza.
“Nadhani mamlaka zinapaswa tukae nazo tuangalie namna ya kufanya marekebisho ili wasio na akiba ya kuuza Julai waendelee kuuza mafuta yatakayoingia mwezi huu badala ya kusubiri kuuza Agosti ili nchi iendelee kuwa na mafuta kwenye mzunguko, badala ya kukaa kwenye maghala,” alisema Mgaya.
Akitofautiana na madai hayo ya akiba, Kaimu Mtendaji Mkuu wa PBPA, Erasto Mlokozi alisema, “kuanzia Julai Mosi, tulikuwa na lita milioni 153 za dizeli na milioni 121 za petroli zinazotosheleza siku 25 kwa mwezi huu, kwa hiyo siyo kweli kwamba asilimia 90 ya mafuta ya Juni yamemalizika.”
Kwa mujibu wa PBPA, bei za mafuta nchini huathiriwa na mabadiliko ya bei za soko la dunia chini ya mwavuli wa Jumuiya ya Wazalishaji Wakubwa wa Mafuta (Opec), gharama za usafirishaji na tozo. “Bei ziko juu kwa mafuta yaliyoagizwa Juni, pengine mafuta ya Agosti yanaweza kupanda,” alisema Mlokozi.