Connect with us

Kitaifa

Tukiacha propaganda tutawaelewa Watanzania

Kwa takribani wiki tatu sasa, mjadala mzito ni makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na uboreshaji wa utendaji kazi wa Bandari za Tanzania kati ya Serikali ya Dubai kupitia kampuni yake ya kimataifa ya DP World na Serikali ya Tanzania.

Bahati mbaya sana, katikati ya mjadala huu, baadhi ya viongozi wa kisiasa, wasomi, wanahabari, viongozi wa dini na wasanii, wamejiingiza kufanya propaganda, lakini kama si hivyo, tungewaelewa wananchi wanataka nini.

Hakuna Mtanzania ambaye anapinga ujio wa wawekezaji nchini, hayupo, ila kinachogomba na hofu ya Watanzania wanaokosa makubaliano hayo ni baadhi ya vifungu, lakini kwa sababu ya propaganda tunaingiza sumu hadi za udini.

Baba wa Taifa, Julius Nyerere (1922-1999) aliwahi kusema nami namnukuu, kuwa “hatuwezi kutatua matatizo yetu kwa kujidanganya kuwa hayapo” na hata katika hili la DP World, tunaanza kuingiza propaganda ili ionekane kila kitu kiko sawa.

Kwa tafsiri isiyo rasmi, propaganda ni jaribio la kimakusudi, la kimfumo la kuunda mitazamo, kudhibiti utambuzi na tabia ya moja kwa moja ili kufikia jibu ambalo linaendeleza dhamira inayotakiwa na anayeanzisha propaganda hiyo.

Propaganda ina sifa kuu nne, ambazo ni pamoja na kuwa ni jambo la makusudi linaloanzishwa, lililopangwa vizuri, linalojaribu kushawishi ili kuunda mitizamo, kama ambavyo tunataka kuhamisha mjadala wa DP World kuingiza udini.

Bahati mbaya sana, wanaojaribu kuingiza propaganda ili kufifisha maoni ya wananchi (public opinion), wameshindwa mapema sana kwa sababu ukiwatizama usoni, unabaini nyuma yao wana uwezo mdogo wa kujadili mambo.
Maoni ni msimamo unaopendeza, usiopendeza, usioegemea upande, au ambao haujaamuliwa ambao watu huchukua iwe ni sera, hatua au kiongozi na maoni sio ukweli, bali ni maonyesho ya hisia za watu kuhusu kitu fulani cha kisiasa.

Mwanafalsafa wa Ujerumani, Georg Wilhelm Friedrich Hegel anasema maoni ya umma yanaweza kuwa na ukweli na uwongo na akaongeza kuwa ni wajibu wa mtu mkuu (Mtawala) kutofautisha kati ya hizo mbili na kufafanua ukweli.

Katika hili la DP World na bandari zetu, ni wajibu wa Serikali kufafanua vifungu vile ambavyo wananchi wamevitilia mashaka kama ambavyo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alivyofafanua ukomo na kwamba ni sehemu tu ya bandari itahusika.

Nimemsoma pia Mwanasheria mkuu wa Serikali (AG), Dk Eliezer Feleshi, akisema upotoshaji unaoendelea kwa DP World na mtazamo hasi dhidi yake, hauna afya kwa maendeleo ya nchi na tunaweza kuonekana tunabagua wawekezaji.

Lakini kwa heshima kabisa, ningependa kumwambia AG kuwa hakuna Mtanzania yeyote anayebagua wawekezaji, hayupo, kinachogomba hapa ni baadhi ya vifungu vilivyopo katika makubaliano hayo na vikifutwa au kuboreshwa mjadala unakufa.

Kuna hoja nyingine inayosemwa na inapigiwa chapuo sana sasa kwamba hakuna mkataba wowote ambao Tanzania imeingia na Dubai na DP World na kwamba mikataba ya utekelezaji itakayoweka ukomo na mengine, itaingiwa baadaye.

Lakini hiki ambacho tumeambiwa tusikiite mkataba bali makubaliano, ni sawa na mtu unapojenga nyumba yako kwamba msingi utakaojenga kulingana na ramani ya nyumba yako, ndio utaonyesha kama unajenga ghorofa au nyumba ya kawaida.

Sasa magwiji wa sheria kama Profesa Issa Shivji, mawakili kupitia Tanganyika Law Society (TLS), wanasiasa wanaoheshimika kama Jaji Warioba na wanazuoni wameainisha vifungu vyenye utata, kwa nini Serikali isisikilize maoni ya umma?

Kama nilivyotolea mfano wa msingi wa nyumba, Ibara ya 2 makubaliano hayo inafafanua lengo la makubaliano ni kuweka mfumo wa kisheria katika maeneo ya ushirikiano, sasa huko mbele ni wakati gani tutarudi nyuma na msingi tayari.

Sasa kama ibara ya 22 ya makubaliano hayo inasema makubaliano hayo au mkataba unaweza kufanyiwa marekebisho wakati wowote kwa makubaliano ya pande mbili, kwa nini tusifanyie marekebisho kabla ya mikataba itakayoingiwa.

Kwa kuwa tayari makubaliano haya yameligawa taifa na kutishia umoja na mshikamano wa nchi yetu, niisihi Serikali ichukue maoni ya wananchi, TLS, wanasheria, viongozi wa dini na maoni yake yenyewe kuboresha makubaliano.

Sitaki kuamini Serikali haijui ni vifungu gani vinalalamikiwa, narudia tena sitaki kuamini haielewi ni vifungu gani vinabishaniwa, sasa ikiamua kupuuza maoni ya wananchi ijue pia madhara yake ni yapi kwa kuangalia mifano ya nchi nyingine.

Zipo tawala duniani na mifano ipo, ambazo zimeporomoka kwa kupuuza maoni ya wananchi wake. Serikali isome alama za nyakati kupitia sakata hili, iachane na kuwakumbatia wanaofanya propaganda, watawaponza.

Imeandikwa na Daniel Mjema

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi