Connect with us

Kitaifa

Majaji, mahakimu wamshukia Rostam

Dar es Salaam. Siku tisa baada ya mfanyabiashara, Rostam Aziz kushuku uhuru wa Mahakama ya Kisutu, Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) kimemjia juu kikimtaka athibitishe tuhuma alizotoa dhidi ya mahakama hiyo.

Rostam aliishuku mahakama hiyo Juni 26, mwaka huu alipozungumzia sakata la bandari akisema, “Hakuna mwekezaji atawekeza kwenye nchi ambayo kesi ikipelekwa hapo Kisutu kiongozi yoyote anaweza kupiga simu akaielekeza mahakama nini cha kufanya.”

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Rostam alizungumzia faida za uwekezaji wa sekta binafsi katika uendeshaji wa bandari, akirejea mkataba wa ushirikiano uliosainiwa na Serikali ya Tanzania na Dubai kuhusu uwekezaji na uendelezaji wa bandari nchini.

Hata hivyo, sakata hilo limeibua hisia tofauti za wananchi, wengine wakikosoa kutokana na kile wanachoeleza kuwa, baadhi ya vifungu vya mkataba huo vina kasoro na hatari kwa masilahi ya nchi.

Kutokana na kauli yake, iliyotafsiriwa kuwa ni kuidharau Mahakama, JMAT imechapisha taarifa kwa umma leo, Julai 4, 2023 ikimtaka mfanyabiashara huyo athibitishe kauli yake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chama hicho hakikuwahi kupokea tuhuma au lalamiko lolote kutoka kwa mtu yeyote ikionyesha maofisa wa mahakama kupigiwa simu na kuelekezwa namna ya kutoa uamuzi.

“Kutokana na maelezo hayo, tumesikitishwa na kauli ya Rostam Aziz ambaye hatukutarajia aongee mambo mazito kama hayo bila kuwa na uhakika wala uthibitisho,” imeeleza taarifa hiyo.

JMAT kupitia taarifa hiyo, imesema kauli za mfanyabiashara huyo zinahatarisha uhusiano na ushirikiano kati ya mihimili mitatu ya dola ndani ya nchi.

“Tunaomba wananchi wenye nia njema na Mahakama na mihimili mingine waendelee kuwa na imani na mfumo wa utoaji haki nchini,” imeeleza.

Aidha, chama hicho kimemtaka mfanyabiashara huyo kuthibitisha kauli hiyo na akishindwa, anapaswa kutumia jukwaa alilotolea taarifa hiyo kuomba radhi.

“Anapaswa athibitishe kauli yake akibainisha jina la Jaji na lini alipewa maagizo na Serikali kutoa maamuzi kinyume na taratibu zilizopo,” inaeleza taarifa hiyo na kuogeza:

“Akishindwa kutoa uthibitisho, tunamtaka atumie jukwaa lile lile kuomba radhi kwa uzito ule ule.”

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi