Kitaifa
Maumivu zaidi gharama za ujenzi zikitarajiwa kupaa
Dar es Salaam. Kama unataka kujenga au kuendelea na ujenzi sasa unalazimika kuzama zaidi mfukoni kukamilisha au kuanza shughuli hiyo.
Hii ni baada ya kuanza utekelezaji wa Bajeti ya Serikali iliyopitishwa kwa asilimia 95 ya kura za wabunge walioshiriki kuipitisha, ikiweka ongezeko la tozo, kodi kwa baadhi ya vifaa muhimu vya ujenzi.
Kwa mujibu wa bajeti hiyo, Serikali itaanza kukusanya Sh1,000 kwa kila mfuko wa saruji, tozo ya asilimia 10 kwenye fito za plastiki zinazotumika kutengeneza fremu za milango, asilimia 10 ya ushuru wa forodha kwa mabati na bidhaa za China na asilimia 25 katika chuma.
Hatua hiyo, pamoja na tabia na hulka za wafanyabiashara bila shaka zitaongeza gharama za ujenzi kuanzia mwaka wa fedha unaoanza kesho.
Kwa uzoefu uliopo, huenda hata babla ya kesho baadhi ya wafanyabiashara wameshaweka ongezeko kwenye bidhaa hizo, huku wengine waliokuwa na mzigo walioununua kabla ya ongezeko la kodi wakisubiri hiyo kesho ili waanze kuuza kwa bei mpya yenye ongezeko.
Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya fedha wameshauri namna ya kukwepa ongezeko la gharama za ujenzi, kwa kufanya ujenzi unaotumia saruji kidogo na upatikanaji wa vifaa katika eneo la ujenzi.
Kwa mujibu wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), ongezeko la gharama hukokotolewa kupitia mchango wa kila kifaa kilichoongezeka bei, bila kuhusisha thamani ya kiwanja, lengo likiwa ni kuepuka upotoshaji wa gharama zilizoongezeka.
Kutokana na mwongozo huo, Mwananchi imefanya uchambuzi wa gharama za ujenzi wa nyumba ya vyumba viwili na sebule kabla na baada ya kuanza utekelezaji wa bajeti kwa kuzingatia mazingira ya kiwanja, mabadiliko ya tabianchi, ukubwa wa nyumba (mita za mraba) na huduma za kijamii.
Vigezo vingine ni uwiano wa gharama za vifaa katika maduka ya rejareja jijini Dar es Salaam na maoni ya wataalamu wa ujenzi, na kuonyesha kuwa huenda gharama zikaongeza kutoka Sh15 milioni hadi Sh20 milioni.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa NCC, Dk Matiko Mturi anasema “ongezeko lipo lakini si kubwa sana, ukichukua kilichoongezeka katika bati, saruji, chuma na ukakokotoa kwa kutumia vigezo vya kitaalamu, utapata asilimia zilizoongezeka ambayo inaweza kuwa zaidi au chini ya asilimia tano ya gharama.”
Mkuu wa Idara ya taaluma ya fedha, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Tobias Swai anasema, “inapoongezeka Sh1,000 kwenye mfuko mmoja wa saruji maana yake bajeti ya saruji itaongezeka kwa kiwango hicho kwa kila mfuko utakaotumika, bei za tofali pia zitapanda.
“Lakini gharama nyingine zitaongeka kwenye usafirishaji wa malighafi wakati wa ujenzi kutokana na Sh100 iliyowekwa katika mafuta. Na gharama zinaweza kuwa juu ya kiwango cha kodi, tozo zilizoongezwa. Pia tubadili ujenzi wa saruji kidogo, hydroform bricks ambayo nimeitumia mimi,” anasema.
Hata hivyo, anasema gharama hizo hazitaathiri moja kwa moja mfumo wa maisha ya Watanzania kushindwa kuendelea na ujenzi kutokana na uhusiano wa sekta zitakazonufaika kwenye bajeti hiyo kupitia unafuu uliowekwa na Serikali.
Ongezeko hilo la gharama linafanyika wakati takwimu za Sensa ya majengo ya mwaka 2022, zikionyesha uwepo wa jumla ya majengo 694,395 yanayoendelea kujengwa Tanzania Bara, ikimaanisha kuwa huenda yakaathirika kwa namna moja au nyingine.
“Gharama za ujenzi ni mahitaji ya mteja, lakini anayehitaji nyumba ya vyumba viwili na sebule kwa vifaa vya thamani ikiwamo vigae, saruji, mabati angalau anatakiwa kuwa na Sh14 milioni,” alisema Ali Kibona, mkandarasi wa ujenzi zaidi ya miaka 30.
Abdulahiman Abdulahiman, mfanyabiashara wa duka la vifaa vya ujenzi jijini Dar es Salaam jana alidai hali ya biashara kwa sasa ni mbaya, lakini bado atalazimika kupandisha bei ya mfuko wa saruji kutoka Sh15,500 hadi Sh18,000 ili kulinda faida katika biashara yake.
Naye mzalishaji wa tofali katika jiji hilo, Damiani Ngowi alisema kuanzia Julai, atabadilisha bei ya bidhaa zake kutoka Sh1,200 hadi Sh1,500 ili kuepuka athari za kibajeti. “Watu wanaojenga nyumba na haya (matofali) ndiyo tunauza sana kwa hiyo itabidi niongeze bei,” alisema.
Katika mtazamo mwingine, Bernard Matiko, mkandarasi wa majengo katika jiji hilo, anasema nyumba ikamilike kwa sasa kwa viwango hivyo vya kawaida inahitaji takriban Sh25 milioni katika ubora.