Connect with us

Kitaifa

Hatari ya unywaji maji kupita kiasi

Dar es Saalam. Wakati wengi tukiamini maji ndiyo kinywaji pekee kinachoweza kutumiwa na binadamu kwa kiwango chochote bila kuwa na madhara, kitaalamu hali ni tofauti.

Wataalamu wanatahadharisha kuwa unywaji maji kupita kiasi ni hatari kwa afya.
Akizungumza na Mwananchi, daktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Sadick Sizya anasema endapo maji yatakuwa mengi zaidi ya yanayohitajika mwilini, binadamu anakuwa hatarini kupata sumu inayosababisha kupungua kwa madini muhimu mwilini, ikiwemo sodium.

“Huwa tunahamasishana kunywa maji kwa wingi bila kujali kipimo. Inaweza kutokea mtu anamuona mwenzake anakunywa maji zaidi ya lita tano kwa siku na yeye akanywa kiwango hicho bila kujua kama mwili wake unaruhusu au la.

“Nasema hivi kwa sababu kila kitu kina kiasi na hata kama maji ni uhai na muhimu kwa afya ya mwanadamu, lazima yatumike kwa kiwango kulingana na uwiano wa uzito na urefu wa mtu kwa maana ya BMI, ili ujue kiasi gani sahihi cha maji unywe ni lazima ushauriwe na mtalaamu ambaye atafanya hivyo kwa kuzingatia BMI,” anasema Dk Sizya.
Anasema ili kujiondoa katika hatari kwa mtu wa kawaida asiye mwanamichezo au anayefanya kazi ngumu, angalau anywe lita tatu za maji kwa siku.

“Ndiyo maana tunasema ni muhimu kufanya uchunguzi wa afya angalau mara moja au mbili kwa mwaka. Ukienda hospitali utachunguzwa na kujua kila kinachoendelea mwilini mwako na hata BMI yako utaijua, utashauriwa kiwango sahihi cha kunywa maji kulingana na uzito wako.

“Mnaposikia pata ushauri wa daktari si lazima upewe dawa, miongoni mwa vitu vya kushauriwa ni hivi,” anasema.

Akizungumzia athari hasi za kunywa maji mengi kupita kiasi, Dk Sizya alisema husababisha kupungua kwa madini mwilini, tatizo ambalo linaweza kuwa chanzo cha mwili kujaa maji, hivyo viungo muhimu kushindwa kufanya kazi.

“Ukinywa maji mengi kupita kiasi unapata water intoxication, asilimia 75 ya mwili wa binadamu ni maji. Mwili pia una madini, sasa ikitokea ukazidisha kiwango cha maji kinachohitajika ndani ya mwili wako upo uwezekano wa kuyeyusha hayo madini hivyo yatapungua.

“Ili mwili wa binadamu ufanye kazi sawasawa una vichocheo ambavyo vinategemea uwiano wa maji na madini, hasa ya sodium, sasa maji yakiwa mengi na sodium ikapungua kutokana na kuyeyushwa unatengeneza tatizo ambalo kitaalamu tunaita Hyponatremia,” anasema.

Dk Sizya anasema hali hiyo inapojitokeza mwili huvimba na kuleta shida kwenye viungo vingine kama vile moyo na kusababisha ushindwe kufanya kazi. Pia ini, figo na ubongo hupata changamoto.

“Wakati mwingine unaweza kumuona mtu kama amechanganyikiwa, anaongea vitu visivyoeleweka, hapo ubongo wake unakuwa umeathirika. Ili kugundua kuwa chanzo chake ni maji ni hadi ubaini madini yamepungua mwilini mwake na utakapofuatilia historia ya mgonjwa ndipo utakapobaini kiini cha tatizo,” anasema.

Wakati mtaalamu akieleza hayo, wananchi wa kawaida bado hawana elimu ya kina kuhusu kiasi cha maji wanachopaswa kunywa.

Merina Chitanda, mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam anasema hafahamu kwa siku anakunywa maji kiasi gani na hajui kwamba kuna kiwango ambacho anatakiwa kunywa kulingana na uzito na urefu wa mwili wake.

“Hayo mambo ndiyo kwanza nayasikia, mimi sijawahi kupima kujua nakunywa maji kiasi gani, nakunywa pale ninapokuwa na kiu. Siwezi kunywa maji wakati wote au kuangalia nina kilo ngapi, nakunywa pale ninapohitaji,” anasema Merina.

Kwa upande wake, Hamis Kigala ambaye ni kondakta wa daladala inayofanya safari kati ya Toangoma na Tandika anasema kutokana na shughuli zake hafikirii kama ataweza kunywa maji kama inavyoelekezwa na wataalamu.

“Binafsi naona kuna vitu vingi vinanishinda kuvifuata na ikizingatiwa kwamba maelekezo yamekuwa mengi, hivi kwa kazi yangu nitaweza kweli kuzingatia kipimo cha maji? Kwa sisi tunaoshinda barabarani kuna siku jua linakuwa kali, hapo ni rahisi kunywa maji mengi, ila wakati mwingine ni vigumu.

“Unaweza kunywa maji muda wa chakula, baada ya hapo unasubiri ukirudi nyumbani halafu tusisahau kwamba kwa hapa mjini hakuna maji ya bure ambayo unaweza kunywa wakati wowote kwa kadiri unavyojisikia,” anasema Kigala.

Jesca Mnyika, mkazi wa Tabata jijini Ilala, anasema huenda akawa kundi la wanaokunywa maji kupita kiasi kwa kuwa hutumia maji na maziwa pekee.

Alisema: “Inawezekana nikawa miongoni mwa wanaokunywa maji mengi, nafanya diet na kitu ninachopendelea kunywa ni maji kwa kuwa hayana sukari na mkakati wangu ni kupunguza sukari mwilini. Hii imenifanya kuachana na chai, soda, pombe hivyo maji kubaki kama kinywaji pekee.

“Ratiba yangu ni kumaliza lita mbili hadi tatu kila baada ya saa saba. Kuanzia asubuhi hadi mchana nitahakikisha nimekunywa lita mbili hadi mbili na nusu, nikipata chakula cha mchana hadi kuitafuta jioni nitakunywa lita mbili nyingine na kuanzia saa moja hadi muda ninaingia kulala nitajitahidi ninywe lita moja na nusu.”

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi