Connect with us

Kitaifa

Stahiki za familia katika simu, laini ya marehemu

Dar es Salaam. Unajua kuwa ndugu au jamaa yako akifariki una uwezo wa kupata taarifa zake na miamala yake? Jibu la swali hili linapatikana katika kanuni mpya za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) za mwaka 2023.

Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta za 2023 (Usajili wa laini za simu) sasa zimeandikwa kwa lugha ya Kiswahili kwa lengo la kuwawezesha Watanzania wengi kuzisoma na kuzielewa kwa urahisi ili kupata urithi wa kidijitali wa marehemu wao.

Chini ya kanuni hizi ni rahisi kwa watu binafsi kupata udhibiti wa taarifa za kidijitali za jamaa zao waliofariki na kuzitumia kwa manufaa ya familia.
“Kanuni hizo ziliundwa kwa kuzingatia umuhimu wa urithi wa kidijitali wa watumiaji wa simu za mkononi na haja ya kulinda taarifa zao muhimu,” alisema Kaimu mkuu wa mawasiliano na uhusiano kwa umma wa TCRA, Rolf Kibaja alipozungumza na Mwananchi.

Kibaja alisema ili kanuni hizo zifanye kazi na wahusika wanufaike ni lazima wawakilishi walioidhinishwa na wanafamilia kufuata taratibu za kisheria ili kuhifadhi urithi wa kidijitali wa watu waliofariki.
Alisema mtumiaji wa simu ya mkononi anapofariki dunia, namba yake ya simu hurudishwa kwa kampuni husika ya mtandao wa simu.

“Hata hivyo, namba hiyo inaweza tu kupangiwa mtu mwingine iwapo msimamizi wa mirathi atashindwa kuwasilisha nyaraka muhimu zinazomtambulisha kuwa mwakilishi aliyeidhinishwa wa mirathi ya marehemu,” amesema.

Amesema kifungu hicho kinalenga kuhakikisha kuwa laini ya simu ya mtumiaji aliyefariki haiharibiwi, iwe chini ya uangalizi wa msimamizi au kupitia mipango mingine iliyopangwa.

Hata hivyo, alisema kuwa ni vema kuhifadhi taarifa za mtumiaji halisi.
“Ni muhimu kutambua kwamba laini ya simu iliyohamishwa inabaki na taarifa zinazohusiana na mmiliki halisi, hii inajumuisha kumbukumbu za kifedha, data binafsi zilizosajiliwa kwa njia ya kibayometriki,” alisema na kuongeza:

“Hata ushahidi wa uhalifu ikiwa mtumiaji aliyefariki alihusika katika vitendo hivyo unaweza kupatikana, kwa hiyo lengo la uhamisho liko kwenye matumizi ya laini ya simu, wakati umiliki na faragha ya taarifa ya mtumiaji wa awali huhifadhiwa vizuri,” amesema.

Alisema kanuni hizo pia zinashughulikia mchakato wa kubadilisha jina la mtumiaji ikiwa jina la mteja limesajiliwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Kitaifa (Nida), mabadiliko yoyote ya jina lazima yaripotiwe ili kuhakikisha uhifadhi sahihi wa kumbukumbu,” amesema.

Kwa mujibu wa kanuni hizo, laini za simu za mkononi zinazohusiana na majina yaliyobadilishwa zitahitaji usajili mpya, unaojumuisha uthibitishaji wa kibayometriki kupitia utambuzi wa alama za vidole.

Akizungumzia alivyopokea kanuni hizo, mkazi wa Dar es Salaam, Sarah Johnson alisema kanuni zimemrahisishia kuhifadhi ipasavyo urithi wa kidijitali wa baba yake.

Sambamba na miongozo hiyo, alisema aliwasilisha nyaraka muhimu kama msimamizi wa mirathi ili kuhakikisha kuwa laini ya simu ya marehemu baba yake inabaki chini ya udhibiti wao na kuwaruhusu kusimamia mambo yake kwa ufanisi.

“Ilitufariji kujua kwamba taarifa zake binafsi zililindwa na tungeweza kupata data muhimu na anwani zinazohusiana na namba yake ya simu. Ninashukuru kwa dhamira ya TCRA ya kuhifadhi urithi wa kidijitali wa watu waliofariki na uelewa wao wa hali nyeti ya mchakato huu,” amesema.

Kwa mujibu wa Kibaja, kwa kuelewa na kufuata miongozo, watumiaji na familia zao wanaweza kuhakikisha kwamba taarifa zao muhimu zinaendelea kuwa salama na kufikiwa ndani ya vigezo vya sheria.

“Ahadi ya TCRA ya kulinda haki na faragha za watu binafsi inaendelea hata zaidi ya maisha yao, ikitoa mfumo mpana wa usimamizi wa akaunti za simu za mkononi baada ya mtumiaji kufariki,” amesema.

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi