Connect with us

Kitaifa

Mabasi ruksa kusafiri saa 24

Dodoma/Dar. Serikali imeondoa rasmi katazo la mabasi kusafiri usiku kufuatia mabadiliko chanya na maoni ya wadau.

Hilo ni miongoni mwa maagizo yanayohitaji utekelezaji yaliyotolewa jana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alipokuwa akiahirisha Bunge jijini Dodoma.

Mengine ni kuwataka waajiri kuweka kumbukumbu sahihi za michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kabla ya Septemba 30, 2023 na Ofisi ya Tamisemi kuwaunganisha waraibu wa dawa za kulevya katika kundi la wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 katika halmashauri.

Kuhusu suala la usafiri wa mabasi, Majaliwa alitangaza rasmi kuanza kwa safari hizo usiku kwa sharti la wamiliki kuomba vibali vya kufanya hivyo.

Mwaka 1992 Serikali ilizuia mabasi ya abiria kusafiri usiku kutokana na matukio ya utekaji uliohusisha uporaji na udhalilishaji kwa abiria, ajali zilizogharimu maisha ya watu na wengine kupata ulemavu wa kudumu na uharibifu wa mali, ikiwemo miundombinu.
Ruhusa hiyo inakuja ikiwa imepita miaka 32 tangu lilipotolewa zuio hilo na aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa kwanza wa Rais katika Serikali ya awamu ya pili, John Malecela.

“Utekaji wa mabasi ulikuwa unafanyika kwenye maeneo yaliyokuwa na barabara mbovu ambayo hayakuwa na mawasiliano ya simu, kufuatia mabadiliko chanya na maoni ya wadau wa usafiri na usafirishaji, wakiwemo wabunge, Serikali imeamua kuondoa zuio la mabasi ya abiria kusafiri usiku lililowekwa miaka ya 1990,” alisema Majaliwa.

Aliagiza Wizara ya Mambo ya Ndani kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, hususan sekta ya uchukuzi kuweka utaratibu utakaofuatwa na wamiliki na madereva wa mabasi ya abiria, wenye nia ya kusafirisha abiria nyakati za usiku.

Akizungumza kuhusu ruhusa hiyo, Mkurugenzi wa habari wa Chama cha Wamiliki wa mabasi (TABOA), Mustapha Mwalongo alisema wameipokea kwa mikono miwili, ingawa imekuja kwa kuchelewa.

“Kwanza suala la kukimbizana halitakuwepo, mabasi yatatembea kwa starehe zaidi. Miaka yote tumekuwa tukijiuliza maswali kwamba Serikali yetu imeshindwa kudhibiti huo ujambazi, leo nasema hongera kwake Waziri Mkuu,” alisema Mwalongo.

Mwenyekiti wa Chama cha wasafirishaji kwa njia ya barabara (TAROTWU), Shukuru Mlawa alisema usafiri wa usiku ni mzuri, utaongeza mzunguko wa fedha kwenye uchumi, ingawa alitilia shaka suala la usalama kwa baadhi ya mikoa.
Hata hivyo, Mlawa alisema kuna maeneo ambayo usalama bado si mzuri na hasa mikoa yenye mapori, kwamba kupeleka magari ya abiria usiku haitakuwa jambo la maana.

Hata hivyo, aliunga mkono maeneo ambao yana usalama mkubwa kwamba mabasi yaendelee kutoa huduma ya usafiri saa 24.
Ruksa ya Waziri Mkuu inarasimisha uamuzi wa Desemba 22, mwaka jana wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), iliyoruhusu baadhi ya mabasi kuanza safari saa 9 usiku.

Licha ya hatua hiyo, wamiliki wa mabasi waliendelea kudai ruksa ya kusafiri kwa saa 24, huku Latra ikisubiri uamuzi wa Serikali.

Hata hivyo, wakati huo wa majaribio, Juni 19, mwaka huu Latra ilifuta ratiba za mabasi tisa yaliyoomba kuanza safari saa 9 usiku, yakiwamo sita ya Ally’s Star na matatu ya Katarama Express kwa kukika masharti ya ruksa hiyo.
Jana, si viongozi wa Latra wala wa Kikosi cha Usalama Barabarani waliopatikana kueleza walivyojipanga kwa safari hizo.

Hivi karibuni gazeti hili lilizunguza na wadau waliobainisha umuhimu wa mabasi kusafiri saa 24, wakisema wamiliki watapata faida, lakini uhai wa magari unaweza kuwa mfupi kutokana na kutembea mwendo mrefu kwa muda mfupi.
“Hapa unaweza kuona kama gari lilikuwa litumike kwa miaka kumi litatumika kwa miaka mitano kwa kuwa matumizi yake yatakuwa ni mengi kwa kipindi kifupi,” alisema mmoja wa wamiliki wa mabasi.

Hata hivyo, kwa upande wa wafanyabiashara na abiria, wadau walisema itakuwa na faida kwa kuwa hawatakaa vituoni muda mrefu, wataepuka gharama zisizo za lazima za kulala hotelini.

Mikopo halmashauri

Akizungumzia suala la mikopo kwa waraibu wa dawa za kulevya, Majaliwa alimwagiza Waziri wa Tamisemi kuongeza kundi hilo katika wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 katika halmashauri.

Waziri Mkuu aliiagiza mikoa yote nchini kuandaa kanzi data kwa waratibu ili waunganishwe kwenye orodha ya wanufaika mikopo ambayo hutolewa katika makundi ya vijana, wanawake na wenye ulemavu.

Serikali iliunda kikosi kazi cha wataalamu ili kifanye kazi ya kuandaa mapendekezo ya utaratibu mpya wa utoaji wa mikopo na urejeshaji wa fedha hizo za mikopo ya asilimia 10 baada ya taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kubainisha upotevu wa fedha kupitia mikopo hiyo.

Kwenye hotuba yake, Waziri Mkuu alizungumzia pia uimarishaji usalama wa chakula kwamba Serikali imetenga Sh320 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa nafaka kupitia Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA).

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi