Kitaifa
TLS yaibua kasoro sakata la bandari
Dar es Salaam. Kukosekana ushirikishwaji wa wananchi, mlolongo mrefu wa utatuzi wa migogoro na ukinzani wa kisheria ni miongoni mwa kasoro zilizotajwa kugubika makubaliano ya ushirikiano katika uwekezaji na uboreshaji wa bandari nchini kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai.
Msingi wa kasoro zote hizo zilizotajwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ni kile ilichoeleza Serikali haikutoa nafasi kwa wananchi na wadau kushiriki mchakato wa kupendekeza, kujadili na kuamua kuhusu makubaliano hayo.
Hoja hizo zimetolewa na timu ya wataalamu wa sheria iliyoundwa na TLS baada ya kuibuka kwa mitazamo tofauti kutokana na uamuzi wa Serikali kusaini mkataba huo wa awali (IGA) na Serikali ya Dubai kupitia Kampuni ya Dubai Port World (DPW).
Timu hiyo ya wataalamu iliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa TLS, Aisha Sinda akisaidiwa na Dk Hawa Sinare, huku wajumbe wengine wakiwa ni mawakili Mpale Mpoki, Stephen Mwakibolwa na Mackphason Mshana.
Katika uchambuzi huo wa kurasa nane, uliotolewa juzi na TLS, Serikali ilitakiwa kutengeneza utaratibu wa kuwashirikisha wananchi katika hatua za upangaji, majadiliano na uamuzi juu ya masuala yote yanayohusu rasilimali za nchi.
Wataalamu hao wa sheria wametoa taarifa yao kipindi ambacho tayari Bunge limeridhia mkataba huo, huku wadau wakitoa maoni tofauti.
Ilichobaini TLS
Kulingana na taarifa ya TLS kwa umma iliyosainiwa na Rais wake, Harold Sungusia, kushirikiasha wananchi ni takwa la kikatiba Ibara ya 21 inayoeleza kuwa kila mwananchi ana uhuru na haki ya kushiriki kikamilifu katika mchakato utakaosababisha uamuzi unaomuathiri yeye au ustawi wa Taifa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mchakato wa Bunge kuuridhia mkataba huo ulikuwa mfupi kiasi cha kukosekana muda wa kutosha kwa wananchi kutoa maoni.
TLS imesema Serikali ilialika wananchi Juni 6 kwa ajili ya Juni 7 mwaka huu kwenda kutoa maoni yao bungeni, muda ambao ulikuwa mdogo kufanikisha hilo.
“Tunaitaka Serikali na Bunge kuheshimu matakwa ya kikanuni na kisheria inayohusu ushirikishwaji wa wadau,” ilieleza taarifa hiyo.
Chama hicho kimependekeza maboresho ya utaratibu wa kuridhia mikataba ya kimataifa, kadhalika kanuni ya kudumu ya Bunge ya mwaka 2020, kifungu cha 18 ili kuimarisha jukumu la mhimili huo katika uridhiaji mikataba.
“TLS inaomba Kanuni za Kudumu zifanyiwe marekebisho kutoa muda wa kutosha kwa wadau kuchambua kwa kina mikataba na kuwasilisha mapendekezo yao kwa Kamati za Bunge zinazohusika,” ilieleza.
Kasoro nyingine iliyobainishwa na TLS ni katika ibara ya 20 ya IGA, inayotaka migogoro baina ya pande mbili kutatuliwa kwa njia ya usuluhishi, huku kukiwa na mlolongo wa siku lukuki zinazopaswa kufanikisha mchakato huo.
“Muda kabla ya kufanya ombi la usuluhishi ni mrefu zaidi (siku 90). Kuna haja ya kuupunguza, kipindi cha makubaliano, hakipaswi kuzidi muda wa siku 90,” ilieleza taarifa hiyo ya TLS.
Utata mwingine wa mkataba huo kwa mujibu wa TLS ni katika kifungu cha 21, kinachotaka sheria za Uingereza kusimamia na kuongoza makubaliano hayo.
Katika hilo, TLS ilisema ni kawaida kuwepo mikataba inayosimamiwa na sheria zisizo za Tanzania, lakini si masuala ya haki ya ardhi, uwekezaji, mazingira na ulinzi na usalama.
Kwa muktadha huo, chama hicho kilipendekeza kupitiwa upya kwa ibara hiyo na kutoa nafasi kwa sheria za Tanzania kusimamia makubaliano hayo.
Kulingana na TLS, ibara ya 23 (1) ya mkataba huo inaainisha dhana mbili za kusitishwa kwake, ambazo ni kusitisha shughuli zote za mradi na ile ya kuisha kwa mkataba wa miradi yote ya utekelezaji (HGA).
Aidha, TLS inasema kifungu cha 23 (2) kinaeleza nafasi ya kurefushwa mkataba unaopaswa kusitishwa kwa makubaliano ya pande mbili ili kuwezesha upande mmoja kudai haki zake.
Pamoja na hayo, kifungu cha 23 (3) kinasema mkataba huo utasitishwa kwa ridhaa ya upande mwingine na haupaswi kuzuiwa bila sababu.
“Ibara ya 23(4) inatamka nchi wanachama hairuhusiwi kushutumu, kujiondoa, kusimamisha au kusitisha mkataba huu katika hali yoyote,” ilieleza.
Katika hayo, TLS ilipendekeza, kufutwa kwa vifungu 23(3) na 23(4) vya mkataba huo, huku ikisisitiza vifungu 23 (1) na 23(2), kuhifadhiwa kwa kuwa ni muhimu.
TLS inasema vifungu vya 23 (3) na (4) vinapaswa kufutwa kwa kuwa vinaminya nafasi ya upande wowote wa nchi zilizokubaliana kuvunja mkataba, hata ikitokea hali inayoathiri masilahi ya nchi husika.
Kulingana na TLS, ibara ya 25 (1) inailazimisha Tanzania kutekeleza shughuli za kiutawala na udhibiti baada ya kusaini makubaliano ili kuhakikisha shughuli za awali za utekelezaji zinaendeshwa kisheria kwa niaba ya mwekezaji mmoja au zaidi au kampuni ya mradi.
Katika kifungu hicho, TLS inapendekeza kuondoa marejeleo yote ya mradi wa awali kutoka kwenye makubaliano ya IGA.
TLS inasema kuna hati ya kisheria inayosimamia shughuli za mradi wa awali, ambazo zinapaswa kutosha kama sheria iliyojitegemea, hivyo suala hilo liondolewe kwenye IGA.
Katika hatua nyingine, chama hicho kimebainisha ahueni na fursa ya Serikali kufanya marekebisho ya kasoro zote zinazolalamikiwa na umma kupitia ibara ya 22 ya mkataba huo inayoruhusu upenyo huo.
Kwa mujibu wa TLS, ibara hiyo inaeleza marekebisho ya mkataba huo yanaweza kufanywa wakati wowote kwa maandishi kupitia makubaliano ya pande husika.
“Zaidi ya hayo, inabainisha kuwa hakuna marekebisho yatakayofanyika bila makubaliano yaliyoainishwa kwa saini na kuridhiwa na/au kupitishwa kwa nyaraka na nchi zilizokubaliana,” inaeleza TLS.
Kuhusu hilo, TLS inasema kwa kuwa kuna mapungufu lukuki yanayozungumzwa na wananchi na wadau katika mkataba huo, Serikali inapaswa kuitumia ibara hiyo kuyashughulikia.
Serikali kusikiliza maoni
Mapendekezo ya TLS yametolewa wakati Serikali kupitia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa imeshaweka ahadi kuwa haitadharau maoni na ushauri wanaoutoa kuhusu maeneo yenye hofu kwenye mradi huo.
Majaliwa alitoa kauli hiyo Juni 20 mwaka huu, katika sherehe za maadhimisho ya miaka 40 ya chuo cha International Evangelism Centre kilichoko Sakila, jijini Arusha.
Alisisitiza bandari haijauzwa, bali Serikali inataka kubadilisha mwekezaji ili iweze kuendeshwa kwa ufanisi na tija zaidi.
“Sisi Serikali tunasikia, tunapokea ushauri, maoni, hofu walizonazo Watanzania…kumekuwa na mjadala mwingi sana, wapo wanaozungumza vizuri, wapo wanaoshauri, wa kubeza na wapo wanaotamani kuona matokeo,” alisema Majaliwa.
“Jukumu la Serikali ni kufuatilia mijadala yote na kuchukua ushauri, hofu na kutengeneza mazingira mema na mazuri kwa masilahi ya Watanzania.”
Mbali na Majaliwa, kigogo mwingine aliyezungumzia suala hilo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Eliezer Feleshi aliyesema Bunge limepitisha azimio la Ushirikiano kati ya Serikali ya Dubai na Tanzania kwenye eneo la bandari, lakini hakuna mkataba wowote ambao umesainiwa kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Kampuni ya DP World.
“Mpaka sasa TPA haijaingia makubaliano au mkataba wowote na DP World, kwani muda wake haujafika,” amesema.
Dk Feleshi, aliyezungumzia suala hilo juzi akiwa jijini Dodoma alisema, “mahusiano ya nchi yanaanza kidiplomasia hata kama kukitokea shida, lakini ikishindikana baada ya hapo lazima uingie katika njia ya usuluhishi.