Kitaifa
Serikali yapunguza tozo zaidi ya 200
Dodoma. Serikali imesema imepunguza changamoto za biashara nchini ikiwemo utitiri wa tozo 380 hadi tozo 148 katika kipindi cha mwaka 2017/18 hadi 2020/21.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Juni 28, 2023 Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Chande wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Buhigwe (CCM), Kavejuru Felix.
Katika swali lake Felix amehoji Serikali ina mkakati gani wa kuondoa changamoto za biashara za mpakani hasa utitiri wa tozo.
Akijibu swali hilo, Chande amesema utozwaji wa kodi ya forodha kwa bidhaa zinazoingia nchini kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki unasimamiwa na Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ya Mwaka 2004.
“Kodi zinazotozwa kwa bidhaa zinazoingia nchini ni pamoja na ushuru wa forodha ambayo ni ya Afrika Mashariki, kodi ya VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) ambayo hutozwa na kila nchi mwanachama,”amesema.
Ametaja tozo nyingine ni kodi ya ushuru wa bidhaa ambayo hutozwa kwa baadhi ya bidhaa na tozo ya maendeleo ya reli. Chande amesema tozo nyingine hutozwa kwa huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali za Serikali zinazohusika na uondoshwaji wa mizigo mipakani, ambazo husimamiwa kwa mujibu wa sheria zilizoanzisha taasisi hizo.
“Serikali imefanya jitihada kubwa ya kupunguza changamoto za biashara nchini hususani kupunguza utitiri wa tozo, kutoka tozo 380 hadi tozo 148 katika kipindi cha mwaka 2017/18 hadi 2020/21,”amesema.
Chande amesema Serikali itaendelea kuondoa changamoto za kufanya biashara nchini ikiwemo sehemu za mipakani.
Akiuliza swali la nyongeza, Mbunge wa Mwibara (CCM), Charles Kajege amehoji Serikali inampango gani wa kupunguza utitiri wa vituo vya ukaguzi.
Akijibu swali hilo la nyongeza, Chande amesema watazifanyia utafiti kuangalia kama zipo hizi changamoto na kuzifanyia kazi na kisha kuziondoa kuziondoa kabisa.
Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Matiko amehoji ni lini wataondoa askari wanaojihusisha na ukusanyaji wa kodi kwenye mipaka.
Akijibu swali Chande amesema askari polisi ni chombo cha usalama wa mali na wananchi na kwamba hawawezi kuwaondoa sehemu za mipakani.
“Tutafuatilia nini kinatokea katika mipaka hiyo katika biashara hiyo ya mipakani,” amesema.