Connect with us

Kitaifa

Bajeti 2023/24 yapita na kodi za maumivu

Dar es Salaam. Licha ya wabunge na wadau kwa wiki nzima kubainisha maumivu yanayoweza kujitokeza kutokana na nyongeza ya ushuru na tozo kwenye bidhaa muhimu, Serikali imetetea tozo hizo na bunge kuamua ziendelee.

Bidhaa ambazo zitakumbana na kodi hizo ni petroli, dizeli, saruji, mafuta ya kula, ngano na bidhaa nyinginezo na hivyo kuufanya mwaka ujao wa fedha kuwa wa kufunga mkanda.

Jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alihitimisha hoja yake kwa kujibu hoja kadhaa zilizoibuliwa na wabunge na kwa nyakati tofauti na wadau mbalimbali, akieleza dhamira ya Serikali katika mapendekezo yake kwenye bajeti ya mwaka 2023/24.

Bajeti hiyo ilipitishwa na wabunge kwa asilimia 95 ya kura ya wazi za “Ndiyo” ikiwa ndiyo ya tatu tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani Machi 19, 2021.

Maeneo yaliyoibua mjadala bungeni ni pamoja na punguzo la kodi ya uagizaji wa ngano nje ya nchi kutoka asilimia 35 hadi asilimia 10, kuongezwa kwa Sh100 kwenye mafuta ya petroli na dizeli na ongezeko la Sh1, 000 kwenye kila mfuko wa saruji.

Mjadala wa bajeti hiyo ulioanza Juni 19 baada ya Dk Mwigulu kusoma bajeti hiyo akiliomba Bunge kuiidhinishia Sh44.39 trilioni, umekamilika na sasa utekelezaji wake utaanza Julai mosi kama Serikali inavyopendekeza na kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ambayo pia ilipitishwa jana na kanuni zake.

Wakichangia mijadala kwa nyakati tofauti, baadhi ya wabunge walihoji kuongezwa kwa Sh1, 000 kwenye saruji, wakiitaka Serikali kufikiria upya suala hilo kwa sababu litawafanya watu wa chini kushindwa kumudu ujenzi wa nyumba bora.

Pia, wabunge wengine walisema kuongeza Sh100 katika mafuta ya petroli na dizeli kutasababisha ugumu wa maisha kwa Watanzania.

Kuporomoka kwa bei ya alizeti pia kuliwaibua wabunge wengi kwenye mjadala huo, wakitaka Serikali kutoshusha ushuru wa mafuta ya alizeti yanayotoka nje ya nchi ili kuwalinda wazalishaji wa ndani.

Catherine John, mkazi wa Mbagala akizungumzia hali hiyo alisema kuondolewa kwa kodi kwenye mafuta ghafi ya kupikia yanayoingizwa nchini kutarahisha upatikanaji wa bidhaa hiyo muhimu ambayo ilikuwa imeanza kushuka bei, na kuwa huenda ushindani kwa mafuta yanayozalisha ndani ukawa mkubwa na kuathiri wazalishaji.

“Unapoweka urahisi wa mafuta yanayotoka nje nchi, maana yake viwanda vilivyopo ambavyo vinatumia malighafi ya hapa nchini havitaweza kushindana sokoni kwa hiyo kuna uwezekano mkubwa Serikali ikaja kuua viwanda vyetu vya ndani,”a alisema.

Uamuzi huo unaelezwa na Bubelwa Kaiza, mchambuzi wa masuala ya siasa na maendeleo, akisema Serikali kuweka kando mapendekezo ya watu kuhusu bajeti hiyo hakulengi kuboresha maisha yao.

Alisema utetezi wa Serikali kuwa tozo hizo zinaenda kuboresha maisha ya wananchi yeye hakubaliani nao akisema kuna umuhimu wa Serikali kuzingatia matakwa ya wananchi.

Alitolea mfano mwaka uliopita kuwa Serikali ilipoweka tozo kwenye miamala ya simu lengo lilikuwa ni uboreshaji wa maisha ya wananchi lakini bado changamoto zimeendelea kuwagubika.

“Ni muhimu kuwa na bajeti ambayo inatokana na matakwa ya wananchi, mfumo uliopo haupo kwenye udhibiti wa wananchi, mambo yanafanyika kiutawala zaidi badala ya kuwa kisiasa, hivyo wanafanya chochote kwa kuwa wanajua walichokiandaa hakijatokana wananchi wenyewe,” alisema.

Maoni ya wadau hao hayana tofauti sana na ya Profesa Humphrey Moshi, mhadhiri wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), aliyesema kupitishwa kwa bajeti hiyo kunatafsiri kwamba mzigo wa gharama za maisha utaongezeka kwa wananchi.

“Hakutakuwa na ahueni katika maisha kwa mwananchi wa kawaida, bajeti itatochea mfumuko wa bei na hasa walipogusa katika eneo la mafuta. Mafuta ni kichochea kikubwa cha mfumuko wa bei, unapogusa eneo hilo unapandisha gharama za kila kitu,” alisema

Kwa sasa bado vitu vingi viko juu unapoongeza na makali kwenye mafuta ni kuzidi kumpa mzigo mwananchi kwa sababu yeye ndiye atakayebeba gharama zote. Uamuzi wa bunge kupitisha bajeti hii tutegemee mfumuko wa bei na maisha kila siku yatazidi kuwa magumu,” alisema Profesa Moshi.

Profesa Moshi anaungwa mkono na mtaalam wa uchumi, Oscar Mkude aliyesema ushuru ulioongezwa kwenye mafuta utabadili bei ya bidhaa zote kutokana na nishati hiyo kuwa muhimu katika usafirishaji.

Kuhusu saruji, Mkude alisema “Ongezeko la ushuru katika saruji kutachangia kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo na kumuathiri mwananchi wa kawaida na kufifisha sekta ya ujenzi.

“Ni wazi kuna watakaoshindwa kujenga, gharama za ujenzi zitakuwa juu na kusababisha hata nyumba za kupanga kodi iwe juu.” alisema

Tozo kwenye mafuta

Akijibu hoja kuhusu suala hilo bungeni, Dk Mwigulu alisema Serikali inafanya ufuatiliaji wa mafuta kwenye soko la dunia na kuwa ikitokea mafuta yakapanda bei, Serikali itaweka ruzuku kama ilivyofanya siku za nyuma.

“Ikitokea bei ikashuka kwenye soko la dunia, si vibaya Serikali ikakusanya tozo hizo na ikapeleka kwenye miradi ya kimkakati kwa sababu hata ikipanda kwa sababu nyingine, Rais Samia amekuwa akiwapa nafuu wananchi, kwa nini upate shida?” alihoji Waziri huyo.

“Sasa kama mafuta kwenye soko la dunia yanashuka, Serikali ikikusanya ile difference (tofauti) ikapeleka kwenye miradi, kuna shida gani? Wanasema kule mbele yatapanda tena, sasa kama yatapanda na Rais amekuwa akitoa ruzuku, hofu yako ni nini?” alihoji Dk Mwigulu.

Alibainisha kwamba miradi ambayo Serikali inatekeleza, hakuna nchi nyingine Afrika ambayo inaitekeleza kwa mara moja kama Tanzania inavyofanya, kwa hiyo hakuna haja ya kuifananisha na nchi nyingine ambazo hazina hata mradi mmoja.

“Miradi hii, mtaona faida zake ikikamilika. Tunapojenga barabara za lami, hatuna maana kwamba barabara hizo tutakwenda kukusanya hela, lakini shughuli zile zinazorahisisha maendeleo ndiyo zinatuletea tija kubwa,” aliongeza.

Kuhusu ongezeko la tozo kwenye saruji, Dk Mwigulu alieleza kwamba Tanzania imejengwa kwa misingi ya ujamaa kwa maana kwamba mwenye nacho aweze kuwasaidia wale ambao hawana uwezo hata wa kwenda shule.

Alisema watoto waliofaulu kidato cha nne wameongezeka kutoka 75,000 mpaka 192,000 na kuwa vyuo vya kati kama vile Arusha Tech na DIT vinazalisha wataalamu wanaotakiwa na uelekeo wa nchi katika kukuza sekta za uzalishaji.

“Tutatoa wapi fedha za kusomesha watoto wetu vyuo vya kati bila ada, ni lazima Watanzania tutagusana tu. Ndiyo, inaweza ikakuongezea gharama lakini ni lazima tumjali mtoto huyo,” alieleza Waziri Mwigulu.

Aliwaomba Watanzania kukubaliana na maoni ya Serikali hata kama yanawaongezea mzigo, ni kwa ajili ya watoto wao. Alisema fedha hizo zinakwenda kutengeneza Taifa lililo bora sasa na miaka inayokuja.

“Tunatambua kwamba tunapoongeza tozo mahali, kiwango kinaweza kisibaki kilekile, Tunaomba Watanzania wote tuelewane, ni lazima tutekeleze miradi ya maendeleo na ni lazima watoto wetu waweze kupata fursa hiyo,” aliongeza.

Wauza mafuta walonga

Mkurugenzi mtendaji wa Chama cha Wauzaji wa Mafuta Tanzania (Taomac), Raphael Mgaya alisema Sh100 iliyoongezwa inakwenda kukuza gharama za uendeshaji katika bishara kwa kile alichokieleza kuwa mbali na kuuza mafuta, wao pia ni watumiaji wa bidhaa hiyo.

“Kuna maeneo ambayo hayana umeme tunatumia jenereta ni mafuta, mjini pia kuna wakati umeme unakata tunatumia jenereta, hii itaongeza gharama za uendeshaji,” alisema Mgaya.

Alisema pia tozo hii inaongezwa muda ambao hakuna ustahamilivu katika soko kwa kile alichoeleza kuwa upungufu wa dola uliopo kwa sasa unafanya kampuni kukosa uhakika wa kupata mafuta katika miezi inayofuata.

“Hili linazidi kutumiiza zaidi,” alisema Mgaya.

Kitu kingine alichokigusia katika hilo alisema tozo hiyo inaongezwa wakati ambao Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) haijahuisha sheria inayosimamia gharama za uendeshaji wa mafuta kwa miaka mitatu sasa ili kuendana na mfumuko wa bei uliopo.

“Ewura inatakiwa kuhuisha sheria hii kila mwaka kuendana na mfumuko wa bei ili kuhakikisha kampuni hazipati hasara.

Hoja ya ngano

Dk Mwigulu alisema punguzo la ushuru kutoka asilimia 35 hadi asilimia 10 kwenye uagizaji wa ngano kutoka nje ya nchi, litawahusu wanunuzi wa ngano ya ndani pale ile ya ndani ikiisha, anapewa ruhusa ya kununua nje kwa bei iliyo nafuu.

“Haijapunguzwa ili anunue ngano ya nje aache ya ndani, ila anapewa nafuu pale anapokuwa amenunua ya ndani. Kwa hiyo, anapewa motisha ya kununua ngano ya ndani…mtu mwingine ambaye haagizi ngano ya ndani, hanufaiki na hiyo duty remission (punguzo la kodi),” alisema.

Alisisitiza kwamba uratibu wa uagizaji ngano nje utaratibiwa na Wizara ya Kilimo.

Kuhusu mafuta ya kula, alisema Serikali imeliangalia jambo hilo ili kutoa unafuu kwa wazalishaji wa ndani ili mafuta ya ndani yasije yakazidiwa na yale ya nje, lengo ni kutoa nafuu kwao wazalishe zaidi.

“Tumekubaliana ndani ya Serikali kwamba jambo hilo tuliangalie kwa ukaribu. Pia, tumekubaliana kudhibiti uingiaji wa mafuta kwa njia zisizo rasmi ambao ndiyo unaleta hiyo flooding (kjujaa mafuta) ambayo wabunge mmeizungumza kwa sauti kubwa,” alisema Dk Mwigulu.

Alisisitiza kwamba Serikali imepokea maoni ya wabunge na kwamba watakaa na vyombo husika kuhakikisha kwamba uingiaji wa mafuta ya kula kiholela unadhibitiwa ili kuondoa wingi wa mafuta hayo ambao unaleta tatizo la bei ya mafuta ya kula.

Mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu alisema kwa upande wa ngano Tanzania haina uwezo wa kujitosheleza kwa kugawa mbegu kwa wakulima, hali ambayo inahitaji bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi.

“Ukiweka makodi makubwa hutaweza kuvutia wafanyabiashara kuingiza bidhaa hiyo, kuwekwa kwa kodi hii kutasaidia wasiache kuagiza wakati tunaendelea na jitihada za kuongeza uzalishaji,” alisema.

Imeandikwa na Peter Elias, Elizabeth Edward, Aurea Simtowe na Baraka Loshilaa

Continue Reading
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi