Kitaifa

Uchumi wa buluu fursa mpya kwa Watanzania

Dar es Salaam. Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Masoud Makame amesema baharini kuna fursa nyingi ambazo hazijatumika, hivyo ametoa rai kwa Watanzania kujitokeza kunufaika na rasilimali hizo.

Makame amebainisha hayo leo Juni 27, 2023 wakati wa kongamano lililoandaliwa na Chuo cha Ubaharia Dar es Salaam (DMI) kujadili mchango wa sekta ya bahari kwa uchumi endelevu nchini.

Amesema asilimia 75 ya bidhaa zote zinazoonekana zimesafirishwa kwa njia ya bahari na duniani kote zinasafirishwa kwa njia hiyo, kwa hiyo amesema bahari ni kiunganishi cha walimwengu wote.

Hata hivyo, amesema kwa bahati mbaya bado fursa zilizopo majini hazijatumiwa ipasavyo. Amesema Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi sasa wamelivalia njuga kueleza fursa zilizopo baharini ambao ndiyo uchumi wa buluu.

“Nitumie fursa hii kuwaomba Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo baharini, ni utajiri mkubwa. Baharini zipo rasilimali ambazo tunaziona kwa macho na zile ambazo huwezi kuziona kwa macho zikiwemo rasilimali kubwa za mafuta na gesi pamoja na madini mengine chini yanayopatikana baharini,” amesam ana kuongeza;

“Huko chini kuna vitu vingi ambavyo kama nchi bado hatujavifikia, tumeng’anana huku juu kwenye madini mengine lakini tukifanya utafiti, chini ya bahari kuna rasilimali nyingi za kuitoa Tanzania kwenye umasikini,” amesema Makame.

Ameongeza kuwa bado Watanzania hawajajitokeza kutumia fursa zilizopo baharini, vibali na leseni wanavyotoa kwa wageni ni vichache ukilinganisha na rasilimali zilizopo baharini hapa nchini.

‘Bado Watanzania hatufanyi uvuvi endelevu, tunayo taasisi yetu inayoongoza shughuli za uvuvi kwenye bahari kuu (Deep Sea Fishing Authority). Kazi yetu kubwa ni kuwapa mipango ya jinsi ya kuchuvuna rasilimali zetu,” amesema.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Bodi wa DMI, Kapteni Ernest Bupamba amesema chuo hicho kinajitahidi kuelimisha wananchi maana ya uchumi wa buluu na fursa zinazopatikana baharini kama utalii, uvuvi, usafirishaji, gesi na mafuta.

Ameongeza kuwa wanajiandaa kuanzisha kozi mpya ya “underwater welding” ili kuwawezesha vijana wa Kitanzania kunufaika na fursa ya ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga ambako mitambo itajengwa baharini.

“Tunajipanua zaidi ili twende mikoa mikoani ambako tutajenga tawi la DMI. Tayari Mwanza tumepata eneo, tutajenga tawi letu pale, pia kule Lindi tutajenga kituo cha ujenzi wa boti,” amesema Bupamba.

Kwa upande wake, baharia wa kike, Eliusa Haule amesema taaluma ya ubaharia ichukuliwe kama taaluma nyingine na siyo dhana iliyojengeka katika jamii hasa vijana kwamba baharia ni mtu anayefanya janja janja.

“Natoa wito kwa wasichana kujiunga na sekta ya ubaharia ili waweze kuinua uchumi wao binafsi na taifa kwa ujumla. Baharia ni mtaalamu wa usafirishaji baharini na kazi hii inaweza kufanywa na wanawake pia,” amesema baharia huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Telephone: +255 653 313 586 | Email: mhariri@chechetimes.com. | Address: 14216 Keko Magurumbasi